• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Raila: Askari waliangamiza watu 72 wakati wa maandamano

Raila: Askari waliangamiza watu 72 wakati wa maandamano

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ameendeleza mashambulizi kwa Idara ya Polisi (NPS) akilalamikia askari kukiuka haki za kibinadamu wakati wa maandamano ya upinzani.

Akizungumzia umma Jumanne, Agosti 15, 2023 eneo la Emali, Makueni kabla kushiriki mazishi ya mfuasi wa Azimio aliyeuawa kwa kupigwa risasi na askari, Bw Odinga alidai idadi ya waliofariki kupitia ukatili wa polisi imefika 72.

Kiongozi huyo wa upinzani alishambulia NPS, akisema kila polisi wanapotumwa hawakosi kuhusishwa na visa vya unyama.

“Hawa polisi wamefanya vitendo vya kinyama, kila mahali wakienda wanapiga watu risasi na kuua. Maandamano ya Wakenya kupinga gharama ya juu ya maisha, waliangamiza watu 72,” Odinga aliteta.

Bw Odinga ndiye aliitisha maandamano ya kitaifa kushinikiza serikali kushusha gharama ya maisha inayozidi kupandana kulemea Wakenya.

Ngome za Azimio, biashara zilifungwa siku za maandamano waliojitokeza wakikabiliana vikali na polisi.

Rais William Ruto alitaja maandamano ya upinzani kuwa haramu, akisisitiza kwamba chini ya utawala wake hataruhusu umwagikaji damu, wala uharibifu wa mali na biashara.

Kufuatia tetesi za Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi (IG), Japhet Koome kuhusu upinzani kukodisha miili, kiongozi huyo wa chama cha ODM aliambia wakazi wa Emali kwamba madai ya aina hiyo yanaashiria afisa asiyepaswa kuwa kikosini.

“Kuna mwingine anaitwa Bw Koome, anasema ati tulienda kutafuta maiti kuonyesha kwenye picha wakati wa maandamano…Hapaswi kuwa afisini.”

Odinga aidha alisisitiza kwamba Wakenya wana haki kuandamana kwa mujibu wa sheria, akisema jukumu la askari ni kulinda waandamanaji.

“Maandamano yanatambuliwa na sheria yetu. Kama umekasirika, huna imani na yale serikali inafanya una haki kufanya maandamano. Polisi hawapswi kutoa ruhusa, kazi yao ni kuelezwa maandamano yanakofanyika,” alisema.

Upinzani na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, wote wamekashifu mienendo ya polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kudhibiti waandamanaji.

Maandamano hata hivyo yalisitishwa kwa muda kuomboleza waliouawa na pia kuruhusu mazungumzo ya mapatano kati ya Azimio na serikali ya Kenya Kwanza.

Vikao vya wawakilishi wa pande zote mbili vilianza mnamo Jumatatu, Agosti 14.

  • Tags

You can share this post!

Mwangaza ajipata gizani akitakiwa kuwajibikia Sh42.4 milioni

Mulamwah arejea Milele FM siku chache baada ya kuondoka

T L