• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Raila Odinga alivyoingia jijini Nairobi kwa staili na kuapa kuendeleza maandamano

Raila Odinga alivyoingia jijini Nairobi kwa staili na kuapa kuendeleza maandamano

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa Azimio la Umoja Raila Odinga Jumatatu, Julai 10, 2023 aliabiri matatu kuingia jijini Nairobi hatua iliyoashiria kutaka kujua changamoto wanazopitia Wakenya.

Akiandamana na baadhi ya viongozi na wanasiasa katika mrengo wa Azimio, alipotua jijini kiongozi huyo wa upinzani alitembea barabara tofauti kwa miguu.

Bw Odinga, alitumia jukwaa hilo kuhutubia wananchi waliojitokeza kumtazama ambapo alisisitiza kuhusu msimamo wake wa maandamano.

“Jumatano (Julai 12, 2023) tutarejea mitaani kuandamana kushinikiza gharama ya maisha ishushwe,” Waziri Mkuu huyo wa zamani alielezea.

Ijumaa, Julai 7, 2023 sikukuu ya Saba Saba Kenya, Bw Odinga aliongoza wafuasi wake kuandamana mitaa kadha jijini Nairobi.

Saba Saba ni siku maalum Kenya ambayo huwa kumbukumbu ya maandamano yaliyofanyika Julai 7, 1991 kupigania demokrasia na utawala wa vyama vingi.

Bw Odinga alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioshiriki oparesheni hiyo iliyozaa matunda.

Katika ziara yake jijini, kiongozi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) alilalamikia mfumko wa bei ya bidhaa muhimu za kimsingi hasa unga, sukari na mafuta.

“Kwa mfano, wanaoishi Ngong kusafiri jijini Nairobi kazi wanalipa Sh150 kuja na Sh150 kurudi. Jumla nauli inameza Sh300, na hujajumuisha chakula. Maisha yamekuwa magumu zaidi na hatutasita kutetea Wakenya,” Odinga akasisitiza.

Azimio pia inaendelea kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2023, unaopendekeza nyongeza ya ushuru (VAT), mfano inayotozwa mafuta ya petroli ikipanda kutoka asilimia 8 hadi 16.

Mswada huo hata hivyo ulisimamishwa kwa muda na Mahakama Kuu, kufuatia kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah.

Mahakama hiyo Jumatatu, Julai 10 ilikataa kuondoa marufuku ya utekelezwaji wa mswada huo tata, badala yake ikielekeza kesi hiyo kwa Jaji Mkuu Martha Koome.

Nyongeza ya ushuru wa mafuta inafasiriwa itachochea maisha kuwa magumu zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa mafuta ndiyo huamua bei ya bidhaa nchini.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Kamanda Francis Kooli: Afisa tajiri wa utu na moyo...

Maelfu ya kampuni zafungwa kufuatia hali ngumu

T L