• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
SAUTI YA MKEREKETWA: Heko tolatola kwa Baraza la Magavana kuthamini Kiswahili

SAUTI YA MKEREKETWA: Heko tolatola kwa Baraza la Magavana kuthamini Kiswahili

Na HENRY INDINDI

HUSEMWA chanda chema huvikwa pete.

Katika jamii yenye mazoea ya kusema na kusema bila haja ya kusema na kutenda, unapopata wanajamii ambao wanasema na kutenda, huna budi kuwapongeza na kuwahongeza kwa juhudi hizo.

Hii ndiyo sababu leo katika Sauti ya Mkereketwa tunateua kupongeza Baraza la Magavana kwa kuonesha mfano bora wa kuigwa na taasisi na asasi nyingine za serikali nchini. Na sababu hasa ya kuwapongeza magavana ni kwamba kuanzia sasa watakuwa wakitumia lugha ya Kiswahili kila siku ya Alhamisi katika shughuli zao zote ofisini.

Ilinisadifu kukutana na mmoja wa wafanyakazi wa Baraza hili, Bi Jacque Migide, ambaye kwa hakika alipobaini mapenzi yangu kwa Kiswahili alifurahi sana. Ilinibainikia kwamba Mkurugenzi wao, Bi Jacqueline Mogeni, ameifanya kaida siku ya Alhamisi kuwa siku maalum ya kutumia Kiswahili ofisini. Kusema la haki, Bi Mogeni anastahili kupongezwa na kuhimizwa na wazalendo wa taifa hili. Siku ya Alhamisi si memo, si baruapepe za kuwasiliana bali hata mazungumzo ya hapa na pale huendeshwa kwa Kiswahili.

Mwaka jana tuliwasherehekea sana wabunge wetu walipoiteua siku ya Alhamisi kuwa siku ya kutumia Kiswahili bungeni. Tuliwaona kama wanaoanza kupiga hatua za kuukubali uzalendo na kuliheshimu taifa letu na amali zake. Laiti wangeendelea kuhamasika na shughuli za bunge Alhamisi ziendeshwe kwa Kiswahili bila kusita wala kugutia. Laiti usimamizi bungeni ungetia mkazo ufanisi wa jambo hili sawa na anavyofanya Bi Mogeni katika Baraza la Magavana nchini. Hivi Kiswahili kingelipigisha taifa letu hatua kubwa ya kizalendo maanake uzalendo hauhitaji watu wa kusema na kusema, bali wa kusema na kutenda au kutenda na kutenda.

Kilichonipunga pia ni kwamba wamekwishaziruwaza akili zao, wafanyakazi wa Baraza hili kwamba siku ya Ijumaa ni siku ya mavazi asili ya humu nchini. Hatua hii inatokana na agizo lililotolewa na Rais Kenyatta kuhusu haja ya kununua bidhaa za humu nchini kwa manufaa ya kunyanyua uchumi wa taifa letu maarufu kama ‘Buy Kenya, Build Kenya’. Sawa na linavyotekelezwa kikamilifu agizo hili ikuluni, ndivyo linavyofanya Baraza la Magavana vilevile. Kwa hivyo, Ijumaa hupambwa kwa mavazi ya Kiafrika na Kikenya katika ofisi za Baraza hili. Hii ndiyo mifano bora ya kuigwa katika kuuandama uzalendo.

Taifa letu linawahitaji wananchi wazalendo kama Bi Mogeni. Tukiwa na wakurugenzi wanaofuata mkondo huu wa utendakazi, sina shaka mizizi ya uzalendo tutaikita katika ardhi ya taifa letu. Kila mmoja wetu ataona heri ya kujivunia uraia na utaifa wetu. Makala na machapisho yanayopatikana kwa Kiingereza katika ofisi hizi za umma yatapatikana kwa Kiswahili pia.

Sina shaka kwamba baada ya muda mfupi kuanzia sasa hatutaona haja tena ya kuwa na lugha za kigeni na hivyo tutakuwa na kila kitu katika lugha yetu ya taifa ambayo pia ni ya kwanza rasmi nchini.

You can share this post!

Mwenyekiti wa Juventus akiri kwamba ndoto ya kuwepo kwa...

KINA CHA FIKRA: Asilan usikubali kushindwa hata kabla ya...