• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Serikali kuomba Uchina mikopo licha ya kuahidi kwenye kampeni kuepuka madeni

Serikali kuomba Uchina mikopo licha ya kuahidi kwenye kampeni kuepuka madeni

Na LABAAN SHABAAN

Ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi, serikali ya Kenya Kwanza iliahidi kuepuka madeni na kushusha viwango vya utozaji kodi katika juhudi za kufufua uchumi.

Rais William Ruto alitoa mapendekezo haya wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2022.

Wakati huo walilaumu serikali ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kwa ukopaji kupita kiasi na kuzidisha ushuru.

Lakini, Kenya imekopa kiwango kikubwa zaidi cha pesa ndani ya mwaka mmoja afisini Rais Ruto alipochukua hatamu za uongozi.

Kulingana na takwimu za Hazina ya  Kitaifa, angalau Sh1.43 trilioni zilikopwa katika kipindi cha miezi tisa ya serikali ya Kenya Kwanza.

Hii ni tofauti na mwaka wa kwanza wa Rais Uhuru Kenyatta ambapo takwimu za Hazina ya Kitaifa zimenakili alikopa Sh437 bilioni.

Mfuko wa madeni utaendelea kuvimba baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kutangaza hatua za kusaka mikopo bado inaendelea.

Akizungumza katika kituo cha redio cha Inooro, Bw Gachagua alisema bosi wake ataenda Uchina kuomba Sh150 bilioni kukamilisha miradi iliyokwama.

“Katika mashauriano hayo, Rais ataomba serikali ya Uchina itathmini masharti ya huduma ya mikopo ambayo haijalipwa na pia kutupa fedha zaidi ya kukamilisha miradi ya barabara iliyokwama,” alisema akisisitiza Kenya inanuia kuwa mdeni mzuri na kuomba wakopeshaji wawe na subira na kuzidi kusaidia nchi wakati wa uhitaji.

Naibu Rais aliendelea kumponda Bw Kenyatta akimlaumu kwa kile alichosema kuanzisha miradi mingi ya barabara ambayo ilikwama.

Bw Gachagua alidai makataa ya kulipa mikopo ya serikali iliyopita ilifika wakati wa uongozi wa serikali ya sasa.

“Tulienda kushauriana na Uchina na kukubali kuwa wanatudai. Tukawaambia tuna barabara ambazo hazijakamilika na hazitusaidii kwa hivyo tunahitaji mkopo zaidi ili tulipe madeni ambayo yamefadhili miradi iliyokamilika,” alisema.

Vile vile bw Gachagua amepinga ripoti zinazoonyesha serikali yao imekopa zaidi akieleza kuwa madeni hayo huhesabiwa kwa sarafu ya Dola ya Amerika ambayo ina nguvu zaidi ya shilingi ya Kenya.

Gachagua ameeleza msukosuko wa uchumi ulioathiri thamani ya shilingi ni chanzo cha kupanda kwa kiwango cha riba.

“Tutatoka kwenye mtego wa deni kwa neema. Hatutapigwa marufuku ya kupewa deni kama nchi zingine Afrika. Tutalipa madeni yote na kuanza kuwaondelea Wakenya mzigo wa gharama ya juu ya maisha,” alieleza akiwaomba wananchi wawe na subira.

Takwimu zinaonyesha takriban nusu ya mapato ya taifa la Kenya hutumika kulipa madeni ambayo makataa yake ya malipo yamefika.

Serikali inakumbana na presha ya kuzidisha mapato kulipa mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma pamoja na kugharamia miradi ya maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

Kwa nini Uhuru huenda awe mwokozi wa Gachagua mashambulizi...

NCIC yadai mauaji Lamu yanatokana na wenyeji kukerwa na...

T L