• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
Kwa nini Uhuru huenda awe mwokozi wa Gachagua mashambulizi kuhusu ‘wenye hisa’ yakichacha

Kwa nini Uhuru huenda awe mwokozi wa Gachagua mashambulizi kuhusu ‘wenye hisa’ yakichacha

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameeleza uwezekano wake kumtafuta Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta “kujadili umoja wa ukanda wa Mlima Kenya.”

Bw Gachagua alisema wamekubaliana na viongozi wote wa kisiasa katika ukanda huo kukoma kumshambulia na badala yake kumheshimu Bw Kenyatta kama rais mstaafu.

“Ninapanga kufanya mazungumzo naye [Kenyatta]. Nimemwagiza kila mmoja kumheshimu, na anafanya vizuri kuendelea kufurahia amani yake,” akasema Bw Gachagua, Ijumaa, Oktoba 6, 2023, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Kwa karibu mwaka mmoja tangu kuapishwa kuwa Naibu Rais, Bw Gachagua amekuwa akimshambulia vikali Bw Kenyatta, akimlaumu kwa “kumhangaisha” kutokana na uamuzi wake kumuunga mkono Rais William Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais) kwenye kampeni za 2022.

Kauli ya Bw Gachagua ilijiri siku moja tu baada Rais Ruto kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri Jumatano usiku, hatua iliyozua midahalo kuwa  baadhi ya mawaziri kutoka ukanda huo “wameshushwa ngazi kimamlaka”.

Baadhi ya mawaziri walioonekana “kushushwa ngazi” ni Bi Alice Wahome (aliyehamishiwa katika Wizara ya Ardhi kutoka Wizara ya Maji) na Bw Moses Kuria (aliyehamishiwa katika Wizara ya Utumishi wa Umma na Uratibu wa Utoaji wa Huduma za Serikali, kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda).

Ijumaa, Bw Gachagua aliondoa hofu yoyote kwamba eneo hilo limetengwa, akisisitiza kuwa “mgao wake serikalini bado upo.”

“Ni mabadiliko tu yalifanywa. Nafasi tulizokuwa nazo kama Mlima bado zipo mikononi mwetu. Hivyo, nawarai watu wetu kutokuwa na wasiwasi wowote,” akasema.

Hata hivyo, juhudi za Bw Gachagua “kutetea maslahi” ya ukanda huo zimeonekana kuwakasirisha baadhi ya viongozi nchini, akiwemo Rais William Ruto, ambapo alisisitiza kuwa kila sehemu ina mgao katika serikali ya Kenya Kwanza, bila kujali ikiwa ilimpigia kura au la.

Katika kauli iliyoonekana kumlenga Bw Gachagua, Rais Ruto alitaja matamshi hayo kama ya kipuuzi na yaliyopitwa na wakati. Rais Ruto alisema hayo Ijumaa, katika Kaunti ya Siaya, alipoanza rasmi ziara ya siku nne katika eneo la Nyanza, ambalo ni ngome ya kisiasa ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga.

“Watu wa Nyanza, ningetaka kuwaambia msikubali mtu yeyote kuwaeleza kwamba mko nje ya serikali. Hii ni serikali ya Kenya. Nyinyi mnalipa ushuru, na nyinyi ni Wakenya. Hii ni serikali yenu. Tutahakikisha kwamba hakuna sehemu ya Kenya itabaguliwa kimaendeleo kwa misingi ya kisiasa. Tunataka kuhakikisha kuwa Kenya ni moja na tutaungana sote kama viongozi kuhakikisha Kenya inaendelea mbele. Ni jambo la kipuuzi kwa yeyote kudhani kuwa eneo fulani nchini haliwezi kupata maendeleo kwa msingi wa vile lilipiga kura. Hilo halifai. Ningetaka kuwahakikishia watu wa Kenya kuwa tutaenda pamoja kama nchi moja,” akasema Rais Ruto.

Mnamo Jumatano, Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Sylvanus Osoro, alimkosoa vikali Bw Gachagua kwa kuilinganisha serikali ya Kenya Kwanza kama kampuni yenye hisa, ambapo baadhi ya maeneo yatavuna huku mengine yakitengwa.

  • Tags

You can share this post!

Naondoka Wizara ya Biashara baada ya kufufua uzalishaji wa...

Serikali kuomba Uchina mikopo licha ya kuahidi kwenye...

T L