• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
SHINA LA UHAI: Changamoto za wanaosikia kupitia kwa sikio moja

SHINA LA UHAI: Changamoto za wanaosikia kupitia kwa sikio moja

NA WANGU KANURI

MWENDWA Mbaabu,41, alipozaliwa sikio lake la kushoto halikuwa linasikia.

Hata hivyo, wazazi wake waligundua kuwa alitatizika kusikia alipokuwa na umri wa chini ya miaka mitano punde tu alipokuwa karibu kuanza shule.

Anasimulia ilikuwa baada yake kuweka sauti ya juu ya televisheni au redio ndio alianza kubaini kuna tatizo.

“Pili, nilipojiunga na shule nilikuwa ninaongea kwa sauti ya juu na watu nikidhani kuwa tuliokuwa tukizungumza nao pia walikuwa wakiongea kwa sauti ya juu. Vile vile, nilikuwa nahama kutoka upande wa kushoto hadi kulia kulingana na mawimbi ya sauti,” anaeleza kama alivyoelezwa na mamake.

Alipopelekwa hospitalini, madaktari walimshauri kuwa vipandikizi (implants) havitamsaidia kwani sikio hilo lilikuwa na uziwi kamili.

Mwendwa Mbaabu ambaye ana tatizo la kusikia kwenye sikio la kushoto. PICHA | HISANI

Bi Mwendwa anasema kila shule aliyoenda, mamake aliwaeleza wakuu wamruhusu mwanawe kuketi mbele ya darasa na upande wa kushoto ili aweze kusikia wanachofunza walimu.

Anaeleza kupata changamoto akiongea na mtu aliyeketi upande wake wa kushoto na mazingira aliyomo yakiwa na kelele au muziki.

“Nikifanya kazi ofisini, wafanyikazi wenzangu wanaokaa upande wa kushoto wanaponiita huwa sisikii huku wengi wao wakidhani ninajitia hamnazo.”

Huku watu wengi wakitembea wakiwa wamebandika vidude vya kusikiliza muziki masikioni, Bi Mwendwa hawezi sababu ya uziwi kwa sikio moja na kuhofia kugongwa na magari barabarani.

“Sina uhuru wa kupokea simu kwa kutumia masikio yote mawili, kusikiza redio, au televisheni. Lazima nifanye jambo moja kwa wakati,” anasema.

Vile vile, kwa kuwa Bi Mwendwa husikiza muziki, televisheni au redio kwa sauti ya juu, wengi huudhika na kumshangaa.

Naye Leonard Onyango, alipoteza uwezo wake wa kusikia akiwa na umri wa miaka 15.

Anasema kuwa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo (meningitis) ulimpokonya uwezo huo.

Bw Onyango ambaye ana uziwi kwa sikio lake la kulia anasema kuwa changamoto anazokumbana nazo ni sawia na alizoeleza Bi Mwendwa.

“Ninatatizika kujua sauti inakotoka kwa hivyo wakati mwingi ninapoitwa mimi huzunguka nikimtafuta anayeniita,” anaeleza.

Anasema kuwa yeye huhofia kutopata taarifa au habari muhimu wakati wa mazungumzo na wenzake huku wengine wakimlaumu kwa kutosikiliza kwa makini anapowaomba kurudia.

Hata hivyo, ili kulinda sikio lake la kushoto, anasema kuwa hupenda kuandikiwa ujumbe kuliko kupigiwa simu.

Bi Mwendwa kwa upande wake, hupendelea kukaa upande wa kulia wa watu ili aweze kusikia wanachosema bila kuwaomba warudie.

Wote wawili wanaungama kuwa masikio yao yenye tatizo la kusikia hutoa sauti zinazowiana na milio ya nyuni.

Hata hivyo, Bw Onyango anasema kwake huwa kila mara ilhali Bi Mwendwa anaeleza kuwa lake huwa mara moja kwa muda mrefu.

Mtu husemekana kuwa na matatizo ya kusikia iwapo hawezi kusikia kiwango cha sauti cha desibeli 20 au zaidi kwenye masikio. Desibeli ni kitengo kinachopima sauti.

Homa ya uti wa mgongo ni mojawapo ya magonjwa yanayomfanya mtu kupoteza uwezo wa kusikia. Vile vile, magonjwa kama surua, matumbwitumbwi (mumps) na rubela.

Madaktari wanasema kuwa kuwapatia watoto chanjo dhidi ya magonjwa haya kunaweza kukapunguza idadi ya visa vya uziwi.

Isitoshe, kuwachanja kina mama wajawazito dhidi ya rubela na maambukizi mengine kunaweza kukapunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na uziwi kamili au wa wastani.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kuwa asilimia 60 ya visa vya uziwi vinaweza vikatatuliwa kwa urahisi na mapema.

Hata hivyo, WHO inasema kuwa zaidi ya watu bilioni 1.5 (asilimia 20 ya wanadamu duniani) wanaishi na matatizo ya kusikia huku wakionya kuwa nambari hii itaongezeka kwa bilioni 2.5 ifikapo 2050.

Hii ina maana kuwa mtu mmoja kwa watu wanne atakuwa na shida ya kusikia.

Watu milioni 430 ni walemavu kutokana na kutosikia huku wengine milioni 34 wakiwa watoto. Hata hivyo, angalau asilimia 30 ya watu walio na umri wa miaka ya zaidi ya 60 wakiwa na matatizo ya kusikia.

Zaidi ya hayo, vijana bilioni moja wapo kwenye hatari ya kupoteza uwezo wao wa kusikia. Hii ni kutokana na kusikiza muziki wenye sauti ya juu kupitia vidude vya masikio

Isitoshe, kuwa kwenye mazingira yenye kelele kama vile kilabu, baa na hata kutia vitu kama pamba za kutoa nta masikioni.

WHO inasema kuwa vijana hawa wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 34, wapo kwenye hatari ya uziwi aidha wa sikio moja au yote mawili.

Kwa mujibu wa watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Carolina Kusini nchini Marekani, wanaotunga sera katika nchi zote duniani, wanapaswa kuhakikisha kuwa kuna masharti ya viwango vya sauti katika maeneo ya burudani.

Ulimwengu uliadhimisha Siku ya Kusikia mapema mwezi huu, watu walio na uziwi wa sikio moja wanahisi kuwa matakwa yao hayazingatiwi sana ikilinganishwa na wale wenye uziwi wa masikio yote mawili.

  • Tags

You can share this post!

Ningali simba wa siasa za Pwani, Raila asisitiza

Nassir adai ipo njama mpya ya kuuza bandari

T L