• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Ningali simba wa siasa za Pwani, Raila asisitiza

Ningali simba wa siasa za Pwani, Raila asisitiza

WINNIE ATIENO Na VALENTINE OBARA

KINARA wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, amepuuza dhana za wapinzani wake wanaodai kuwa anazidi kupoteza umaarufu katika ukanda wa Pwani ulio ngome yake kwa miaka mingi.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliopita ambapo idadi ya kura za urais alizopata ilipungua ikilinganishwa na miaka ya awali, baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza walidai ni ishara kwamba nyota yake inazimwa eneo hilo.

Rais William Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza wamekuwa wakijitahidi kuvutia wafuasi na viongozi wa ODM upande wao wakidai mawimbi ya kisiasa yanabadilika Pwani.

Akiwa katika ziara ya kaunti za eneo hilo tangu Jumapili, Bw Odinga alisema anaamini bado ana ufuasi mkubwa huko.

Akizungumza katika mkutano na wajumbe wa ODM Mombasa, alisema matokeo ya uchaguzi uliopita hayafai kutumiwa kutathmini umaarufu wake wa kisiasa kwa vile, kulingana naye, kulikuwa na wizi wa kura.

“Wakifungua sava wataona vile kura ilibadilishwa hapa Mombasa, Kwale na hata Kilifi. Katika kila kituo waliiba kura zetu wakapeleka upande wao. Ukifungua sava utaona kituo kwa kituo vile walibadilisha,” akadai.

Mbali na mkutano huo wa wajumbe Mombasa na kuhudhuria ibada kanisani mjini humo, Bw Odinga alifanya mkutano wa hadhara Likoni kisha jana Jumatatu akaelekea Mtwapa, Kaunti ya Kilifi.

Mikutano hiyo ya hadhara ni ya kuhamasisha wafuasi wake kuhusu maandamano ambayo Azimio inapanga kufanya dhidi ya serikali mnamo Machi 20.

“Tunataka kutoa shukrani kwenu kusimama nasi unyo kwa unyo. Mlifanya vizuri sana na yale mlifanya yote yalienda sawa,” akasema.

Licha ya hayo, umati mkubwa uliokuwa ukivutiwa wakati aliyekuwa gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, alipokuwepo yalikosekana.

Bw Joho ambaye ni naibu kiongozi wa ODM hajakuwa mstari wa mbele katika siasa za Pwani tangu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, ambapo kampeni nyingi alizoongoza zilikuwa nje ya ukanda huo.

Katika kipindi hicho, ODM imekuwa ikiepuka sana kufanya mikutano ya hadhara katika uwanja mkubwa wa Tononoka ambao umekuwa ukitumiwa kama kipimo cha uwezo wa wanasiasa kuvutia umati mkubwa.

Bw Odinga alisema waliamua kufanya mkutano wao wa hadhara katika uwanja wa Caltex, Likoni, kwa vile washaenda Tononoka mara nyingi awali.
Mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Babu Owino, alimsifu mwenzake wa Likoni, Bi Mishi Mboko, kwa kufanikisha mkutano huo ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa.

“Leo hii nataka nimshukuru mama Mishi Mboko. Leo umetutendea kazi nzuri sana,” akasema Bw Owino.

Bw Odinga aliandamana na vinara wenzake wa Azimio katika ziara hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wapoteza bunduki wakijipiga ‘selfie’

SHINA LA UHAI: Changamoto za wanaosikia kupitia kwa sikio...

T L