• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
SHINA LA UHAI: Kisonono chaweza sababisha utasa na athari nyingine

SHINA LA UHAI: Kisonono chaweza sababisha utasa na athari nyingine

NA WANGU KANURI

WIKI jana Wakenya walikabiliwa na hali ya mfadhaiko na wasiwasi baada ya kuripotiwa kwa mkurupuko wa ugonjwa wa kisonono unaogomea dawa za kukabili maradhi za antibiotic (super gonorrhoea) jijini Nairobi.

Licha ya ripoti hiyo kutolewa baada ya kuchunguza makahaba, kuwepo kwa ugonjwa huo kuliibua hofu.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya Nchini Dkt Patrick Amoth alieleza kuwa mmoja kati ya makahaba 400 waliopimwa katika kliniki mojawapo jijini ndiye alikuwa na ugonjwa huo.

Hata hivyo, kulingana na wanasayansi, angalau watu 270 walikiri kushiriki tendo la ndoa bila kutumia kondomu ili kupata pesa nyingi.

Kwenye ripoti hiyo, makahaba wengine walifanya ngono na angaa wateja 29 chini ya wiki mbili bila kutumia kondomu.

Ugonjwa wa kisonono huenezwa kupitia ngono huku ukiwepo duniani kutoka miaka ya 1800. Ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa za antibiotic mbalimbali na hugomea dawa nyakati zingine huku wanasayansi wakifanya juhudi za kutengeneza aina nyingine ya dawa hizo znye nguvu zaidi.

Kwa mfano, miaka miwili iliyopita, ugonjwa huo ulishinda kutibiwa kwa kutumia dawa za antibiotic aina ya ya azithromycin baada ya kutumika tangu 2010. Kwa sasa madaktari huwadunga wagonjwa wa kisonono sindano za antibiotic zilizo kwenye kundi la cephalosporins.

Kwa mujibu wa Dkt Semu Lagdera, mtaalamu katika hospitali ya RFH Healthcare, ugonjwa wa kisonono huenezwa kingono kupitia uke wa mwanamke, uume, makalio au mdomo wa mtu aliye na ugonjwa huo.

“Dalili za ugonjwa huu huwa tofauti kulingana na jinsia na muda wa uambukizaji,” anasema.

Wanaume wengi wanaopata aina hii ya kisonono huonyesha dalili kwa kipindi cha chini ya siku 14 baada ya kuambukizwa.
Wagonjwa hao huhisi uchungu wanapokojoa huku wakitokwa na majimaji yenye rangi nyeupe, manjano au kijani kibichi.

“Ugonjwa huo unaweza ukaenea hadi kwa tezi dume na kusababisha maumivu,” anasema Dkt Lagdera.

Nyakati zingine, kisonono cha aina hii kinaweza enea kwa damu na kuathiri viungo vya mwili na kumfanya mtu kuhisi joto, kuwa na mwasho wa ngozi, akavimba moyo na hata usaha ukajaa kwa ini.

“Ugonjwa huu usipotibiwa huenda ukaathiri viungo vya uzazi na kusababisha utasa kwa wanaume na wanawake, kiini cha utasa nchini,” anaeleza.

Dalili za kisonono cha aina hii kwa wanawake huwa chache huku nyakati nyingi wagonjwa wakijulishwa kuwa wanaugua maambukizi ya mfumo wa kupitisha mkojo (UTI) ilhali ni kisonono.

Mwanzoni, mwanamke anayeugua ugonjwa huu huhisi uchungu anapokojoa, anatokwa na majimaji yasiyokuwa ya kawaida, anahisi uchungu kwa fupanyonga na kutokwa na damu anaposhiriki katika tendo la ndoa.

Zaidi ya hayo, ugonjwa wa kisonono unaweza ukaathiri utando wa uke huku mgonjwa akihisi uchungu na kutatizika anapoenda haja.

Macho yake yanaweza yakawasha wakati wa mwangaza na kutoa usaha kwa jicho moja au yote mawili.

“Koo la mgonjwa wa kisonono linaweza likafura huku akahisi maumivu kwenye viungo vya mwili anapotembea. Viungo hivi vilivyoathiriwa huwa vimefura na kuwa rangi nyekundu,” anasema.

Huku wanaume na wanawake wanaoshiriki ngono wakiwa kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu, Dkt Lagdera anaeleza ugonjwa huu hutambulika kwa kuchunguza mkojo na mrija wa mkojo kwa wanaume na kuangalia sehemu ya ndani ya uzazi wa mwanamke.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linaonya kuwa kwa mwanamke mjamzito aliye na kisonono, mimba yake inaweza ikakosa kukua inavyofaa, ikaharibika au hata akaaga dunia.

Ikiwa mwanamke mjamzito ameambukizwa ugonjwa huu, anaweza akaambukiza mtoto kwani hupitia kwa njia ya uzazi anapozaliwa.

Mtoto huyo anaweza kuwa kipofu, akapata maambukizi kwa viungo mwilini au hata kwenye damu na kutishia maisha yake.

Hata hivyo, mwanamke huyo hushauriwa kupokea matibabu mapema ili kupunguza hatari.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu milioni 1 hupata magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono (STIs) kila siku duniani.

Magonjwa haya ambayo yamehusishwa na athari kwa viungo vya uzazi, yanaweza pia yakasababisha ugonjwa wa kansa.

Kulingana na takwimu za 2020, WHO ilirekodi visa milioni 82 vya ugonjwa wa kisonono.

Kituo cha Kutafiti na Kudhibiti maradhi (CDC), kinapendekeza uchunguzi wa kila mwaka kwa watu ambao hushiriki tendo la ndoa na watu wengi na wale walioambukizwa ugonjwa huo.

Madaktari wanawashauri wagonjwa wa kisonono kushiriki ngono siku saba baada ya kumaliza dawa walizokuwa wamepewa.
Subira hii huzuia uenezaji wa ugonjwa huu na hata hupunguza hatari ya kupata kisonono tena.

“Wagonjwa hawa pamoja na wapenzi wao wanapaswa kufanyiwa uchunguzi tena miezi mitatu baada ya kupokea matibabu,” CDC inasema.

Wataalamu wanashauri kuwa kutumia mipira ya kondomu ni njia mojawapo ya kupunguza uenezaji wa kisonono.

“Njia yenye uhakika ya kupunguza uenezaji wa ugonjwa huu ni kuwa mwaminifu kwa mpenzi wako mmoja ambaye amepimiwa na hana kisonono zaidi ya kutoshiriki katika tendo la ndoa.”

Pamoja na hayo, wapenzi hawa wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa wawili wakamatwa kwa kuuza pombe haramu na...

MUME KIGONGO: Wanaume wanene hatarini kuathiriwa na maradhi...

T L