• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAHARIRI: Mahakama ya Upeo ipewe nafasi kuamua kesi ya urais

TAHARIRI: Mahakama ya Upeo ipewe nafasi kuamua kesi ya urais

NA MHARIRI

MAHAKAMA ya Juu leo inatarajiwa kuanza rasmi vikao vya kesi ya kupinga uchaguzi wa urais uliofanywa Agosti 9.

Tangu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipotangaza matokeo ya uchaguzi huo, kumekuwa na mengi ambayo yamesemwa na pande tofauti.

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, ukiongozwa na Bw Raila Odinga, umepinga ushindi wa Dkt William Ruto, ulivyotangazwa na IEBC.

Mbali na Bw Odinga pamoja na kinara wa NARC-Kenya, Bi Martha Karua, aliyekuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa urais, pingamizi dhidi ya matokeo hayo limetolewa pia na walalamishi wengine ambao washawasilisha kesi zao mahakamani.

Kufikia sasa, wananchi wamepokea habari tele kutoka pande tofauti kuhusu madai ambayo mengine ni mazito kwa kiwango cha kuwa vigumu kuaminika.

Majaji wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, watakuwa na muda mfupi unaokubaliwa kisheria kusikiliza, kusoma na kutathmini madai ambayo yatawasilishwa mbele yao kabla uamuzi utolewe.

Ni muhimu wananchi wafahamu kuwa, yale yote yanayowasilishwa mahakamani ni lazima yafanyiwe utathmini wa kina kabla hata kuamuliwa kama yatakubaliwa kutumiwa katika kesi.

Misimamo ya wanasiasa kutoka pande zote mbili tayari inaonyesha hali ambapo wote wanataka wananchi waamini kuwa wao ndio wanasema ukweli ilhali ukweli ni kuwa, yote yaliyowasilishwa kwa sasa yatabaki kuwa madai hadi yathibitishwe kikamilifu.

Hatua hii ya wanasiasa inaeleweka kwa vile kwa mtazamo wao, hasa wanaopinga matokeo ya urais, mchakato mzima wa uchaguzi wa urais haujakamilika hadi wakati kesi zilizo mbele ya Mahakama ya Juu zitakapoamuliwa.

Ni matumaini yetu kwamba, kuelekea mbele, mahakama itaachiwa nafasi ya kufanya kazi yake kwa njia huru bila vitisho wala hatua ambazo zitalenga kuwashawishi majaji kwa njia yoyote ile.

Walalamishi na washtakiwa washapata nafasi ya kutosha kisheria kupeleka ushahidi walio nao mahakamani, na sasa kilichobaki kwao ni kushawishi mahakama kuwa ushahidi wao una uzito.

Pande zote za kisiasa zitumie vyema mifumo iliyopo kisheria kueleza ushahidi wao mahakamani bila kufuata njia ambazo zinaweza kutatiza amani ya nchi.

Hakutakuwa na faida kwao kuendelea kueneza uvumi usio na msingi kwa wananchi hadharani na kupitia kwa mitandao ya kijamii.

Wananchi hawana mamlaka ya kuamua kesi mahakamani, isipokuwa kama kuna nia mbaya ya wanasiasa kuchochea fujo nchini.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Maziwa unayotumia huenda yadhuru afya yako

CHARLES WASONGA: Migawanyiko IEBC inaweza kuleta mgogoro wa...

T L