• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
SHINA LA UHAI: Teknolojia ya ‘3D printing’ yaleta afueni kwa upasuaji

SHINA LA UHAI: Teknolojia ya ‘3D printing’ yaleta afueni kwa upasuaji

NA PAULINE ONGAJI

MIAKA saba iliyopita Bw Christopher Muraguri alivumbua teknolojia ya kusaidia madaktari wa upasuaji kutekeleza kazi zao sio tu kwa urahisi, bali pia kwa usahihi na hivyo kuwezesha wagonjwa kupona upesi.

Hii ilikuwa kupitia Micrive Infinite, kampuni ya kuunda maumbo mifano ya sehemu za mwili inayosaidia madaktari kujiandaa kabla ya upasuaji na kutumia vipimo kamili.

Hivi majuzi teknolojia hii ilitambuliwa na shirika la kudhibiti dawa na vyakula nchini Amerika FDA, kumaanisha kwamba lililosalia kwao ni kuonyesha kwamba bidhaa hii ni salama kwa matumizi na kwamba wana uwezo wa kuizalisha kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu.

Teknolojia hii inahusisha ufinyanzi wa viungo vya mwili na hasa kichwa kwa kutumia aina spesheli ya plastiki, mifano ambayo inafanana kabisa na viungo kamili vya mgonjwa mhusika, kimaumbile na hata kwa vipimo.

“Hasa, teknolojia hii inatumika katika visa vya kipatholojia vinavyohusisha mifupa ya uso, uvimbe wa kansa, majeraha ya uti wa mgongo na hitilafu za kuzaliwa kama vile (scoliosis, kyphosis) na majeraha ya nyonga.”

Kazi huanza kwa kutumia data kutokana na picha za CT scan, kisha taarifa hizi zinatumika kuunda mfano wa sehemu husika.

“Hii hufanyika kwa kutumia aina maalum ya plastiki ya Z-PETG, sehemu bandia za mifupa au vipande vya chuma kisha umbo hili linafanywa kuwa ngumu na kuwekwa meno na hivyo kufanana kabisa na sehemu ya mwili. Viungo hivi vyaweza undwa kuambatana na vipimo kamili vya mgonjwa husika,” aongeza Bw Muraguri.

Shughuli hii hufanyika kwa awamu ambapo mgonjwa anamtembelea daktari ambaye anatambua maradhi, kisha Bw Muraguri (Micrive) anahusishwa ili kuchukua kipimo cha mwili na kiungo husika, kwa mwongozo wa mpasuaji.

Baadaye, kwa kutumia printa maalum ya kimatibabu ya grade 3D, mfano wa umbo la sehemu iliyoathirika unatumika kuunda umbo kamili kwa kutumia plastiki.

Mbali na kusaidia kuandaa madaktari kabla ya upasuaji, teknolojia hii inachangia pakubwa katika shughuli za kuumba upya sehemu za mwili zilizoondolewa kutokana na maradhi kama vile kansa, majeraha na udhaifu wa kimaumbile.

Kulingana na Profesa Symon Guthua, mtaalam wa upasuaji anayehusika na kutibu maradhi, majeraha na kasoro sehemu za kichwa, shingo, uso, taya na tishu mdomoni, katika Chuo Kikuu cha Nairobi, kutokana na teknolojia hii, yeye pamoja na wataalam wengine wa upasuaji sasa wanaweza kutambua tatizo, kujua mbinu za kutumia kufanya upasuaji na hata kupanga kabla ya shughuli hiyo kuanza.

Ni suala ambalo asema linaimarisha usalama wa wagonjwa hasa ikizingatiwa kwamba kabla ya kuanza shughuli hii wana ufahamu kuhusiana na sehemu halisi zilizoathirika, kumaanisha kwamba uwezekano wa kufanya makosa ni finyu sana.

Mbali na hayo, Prof Guthua asema kwamba shughuli za kuelimisha wagonjwa zimerahisishwa kwani kabla ya upasuaji kuanza wanaelezwa kuhusu utaratibu utakaohusika, huku wakiwa wameshika umbo sawa na sehemu ya mwili wao iliyoathirika, ikilinganishwa na kuwaeleza kwa kutumia picha.

“Pia hauhitaji kumsumbua mgonjwa kwa ziara za kila mara hospitalini kwani pindi baada ya kupata umbo la sehemu iliyoathirika tunaweza jiandaa kabla ya upasuaji, pasipo mgonjwa kuwepo,” aongeza.

Kwa upande mwingine, aongeza, pia wagonjwa wanaridhika kabla ya upasuaji kwani wanaweza pata picha kamili ya utaratibu huo hata kabla ya kuanza, suala linalopunguza wasi wasi.

Bw Muraguri asema teknolojia hii inawawezesha kuunda viungo bandia vitakavyochukua nafasi ya vile halisi vilivyoathirika, hata kabla ya upasuaji.

“Hii inamaanisha kwamba shughuli yote ya upasuaji na kuweka viungo bandia inafanywa wakati mmoja katika chumba cha upasuaji. Awali, shughuli ya kuunda viungo bandia ilichukua muda kwani ilikuwa lazima tuanze kufanya mipango ya kuvisanifu baada ya upasuaji, kumaanisha kwamba mgonjwa alihitajika kukaa muda mrefu kabla ya kumaliziwa upasuaji, suala lililofanya ichukue muda mrefu kabla ya kurejelea hali yake ya kawaida,” aeleza.

Bw Muraguri alipata msukumo wa kuvumbua teknolojia hii Novemba mwaka wa 2015, baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani iliyoacha mguu wake wa kushoto na majeraha mabaya.

“Picha za skani hazikutoa maelezo kamili kuhusiana na kiwango cha majeraha niliyopata, na hivyo upasuaji ambao ungechukua muda wa saa mbili pekee uliishia kuchukua saa sita. Pia, nilitakikana kukaa na plasta kwa wiki sita pekee lakini nikadumu nayo kwa miezi miwili. Hii ni kando na kuwa bili ya hospitali ilikuwa imeongezeka,” aeleza.

Swali lililomjia lilikuwa ni lipi angefanya kuimarisha usahihi na hivyo kupunguza muda wa upasuaji na gharama za matibabu? Na hivyo alianza kufanya utafiti, na majuma kadha baadaye alikuwa ashakamilisha kufinyanga muundo wa mguu wake.

“Nilipomuonyesha daktari wa upasuaji muundo wa mguu wangu alifurahi na kunitambulisha kwa wenzake. Muundo huu uliwarahisishia kazi walipokuwa wakiushughulikia mguu wangu na matokoeo yalikuwa mazuri,” asema.

Baada ya hapa alijitosa katika utafiti wa ziada uliochukua miaka miwili, mara hii akishirikiana na Prof Guthua.

Kulingana na Bw Muraguri, uvumbuzi huu umepunguza muda unaotumika mgonjwa akiwa kwenye thieta na hivyo kuondoa kabisa uwezekano wa hitilafu wakati huu. Hii, hatimaye inapunguza gharama kwa mgonjwa.

Mwanzoni, suluhu zote za aina hii zilitoka bara Ulaya na mara nyingi wagonjwa wangelazimika kusubiri hadi mwezi mmoja ili kupokea kiungo wanachohitaji, huku wakati huu wote wakiwa na uvimbe unaosababisha kansa.

“Kwa wastani ingemgharimu mgonjwa zaidi ya Sh300,000 kupokea kiungo hiki, na gharama hii ya juu iliwafanya wengi washindwe kumudu,” asema Bw Muraguri.

Kwa hivyo kutokana na sababu kuwa huu ni uvumbuzi wa Kenya, asema, bila shaka inamaanisha kwamba raia watanufaika kwa kulipia pesa kidogo ikilinganishwa na zile zinazoagizwa kutoka nje.

“Pia, bidhaa inapatikana kumaanisha kwamba wagonjwa wa humu nchini hawatahitajika kusubiri kwa muda mrefu.”

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Wabunge wa Kenya Kwanza wafaa kujua wao si...

MUME KIGONGO: Kunywa kahawa kunasaidia wanaume wenye kansa...

T L