• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
SHINA LA UHAI: Vidimbwi vya chumvi vyavuruga wanakijiji

SHINA LA UHAI: Vidimbwi vya chumvi vyavuruga wanakijiji

NA PAULINE ONGAJI

KWA umbali chaonekana kama kisiwa cha kijani kilichozingirwa na jangwa.

Hapa ni nyumbani kwake David Juma Kadenge na mkewe, Kahaso Charo Karisa, wakazi wa kijiji cha Garithe B, Marereni, Kaunti ya Kilifi.

Hapa, wawili hawa wanaonyesha mnazi ambao miaka michache iliyopita ulikuwa umenawiri na kuzaa matunda, ila kwa sasa unaoza na kukauka.

Kando ya kipande chao cha ardhi ni dimbwi kubwa la maji ya chumvi linalomilikiwa na kampuni moja ya kusafisha chumvi eneo hilo.

Miaka michache iliyopita, Kadenge asema kwamba walikuwa na zaidi ya minazi 300, lakini katika kipindi cha hivi majuzi miti hiyo imekuwa ikitoweka.

Picha ya minazi iliyokauka kwenye shamba lake Bw David Juma Kadenge eneo la Garithe B, Marereni, Kaunti ya Kilifi. PICHA | PAULINE ONGAJI

Siku zinapoendelea kusonga, ndivyo miti hii inavyoendelea kukauka ambapo mkulima huyu anaamini kwamba ni kutokana na viwango vya chumvi ambavyo vimeendelea kuongezeka sio tu shambani mwake, bali eneo hili lote.

“Kwa miaka sasa tumeshuhudia mimea ikiacha kuota, kukauka na kuoza kuanzia mizizini hadi juu na hatimaye kuangamia.Nimepoteza miembe na mikorosho ambayo pia ilianza kuonyesha ishara hizi hizi hapo awali,” aeleza.

Ni tatizo ambalo limeathiri pakubwa mapato ya familia ya Kadenge.

“Mwanzoni ningepata mapato ya kujikimu kutokana na mauzo ya mazao yangu ya nazi, maembe na korosho, lakini kwa muda mrefu sasa mimea yangu imeangamia na sina kipato kwani ardhi yangu imegeuka na kuwa jangwa,” aeleza.

Sasa amegeukia uchomaji makaa ili kukimu mahitaji ya familia yake.

“Sasa nalazimika kusafiri kilomita kadhaa hadi katika shamba langu lingine ili kupata miti ya kuchoma makaa na kuuza,” aongeza.

Kwa miaka sasa kumekuwa na maswali kuhusu athari za kimazingira zinazotokana na shughuli za viwanda vya usafishaji chumvi eneo la Pwani ya Kenya, huku tafiti kadhaa zikionyesha masaibu ambayo yameendelea kuwakumba wakazi wa sehemu zilizoathirika.

Mwaka wa 2017, Tume ya kitaifa kuhusu haki za kibinadamu KNCHR ilifanya ukaguzi wa hali ilivyo katika maeneo haya, ambapo lengo lilikuwa kutambua hatua ambazo zilikuwa zimechukuliwa na kitengo cha Chama cha watengenezaji bidhaa (KAM), kinachohusika na usafishaji chumvi na wahusika wengine, ili kutekeleza mapendekezo kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za kibinadamu na viwanda vya chumvi eneo la Magarini, Malindi.

Ukaguzi huo ulinuiwa kukagua mafanikio tangu uchunguzi wa mwaka wa 2006 kuhusu viwanda vya chumvi eneo hili, kunakili yaliyoafikiwa katika kutekeleza mapendekezo ya wahusika, na kutoa mapendekezo zaidi ya suluhisho.

Patrick Ochieng, ni mtetezi wa haki za kibinadamu ambaye alikuwa mojawapo ya wadau wakuu katika utaratibu wa kuimarisha mjadala baina ya kampuni za chumvi na jamii eneo hili kuanzia Juni hadi Agosti 2014.

Pia wakati huo alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Ujamaa Center, shirika lililojumuisha muungano wa mashirika yasiyo ya kijamii yaliyoshiriki katika mabaraza ya uchunguzi huo.

Kulingana naye, katika kamati ya rais chini ya usimamizi wa Kamishna wa eneo hilo na Halmashauri ya Kitaifa ya Kudhibiti Mazingira NEMA, kubaini mapengo yaliyoangaziwa na jamii za hapa kuambatana na mapendekezo ya ripoti ya uchunguzi huo, kulikuwa na madai ya uaharibifu wa mazingira.

Nickson Kaindi Charo, mwenyekiti wa kamati ya vijijini kuhusu uhifadhi wa misitu (Village Development Forest Conservation committee) inayowakilisha zaidi ya vijiji 13 katika eneo la Marereni, asema ni bayana kwamba shughuli za uvunaji chumvi eneo hili zimekuwa na athari kubwa kimazingira.

“Mabirika ya maji ya chumvi yameendelea kupanuka na kuongezeka, na hii imekuwa na athari kubwa kwa wakazi wa eneo hili,” aongeza.

Matokeo ya makadirio ya matumizi ya ardhi ambayo yalikuwa sehemu ya ripoti ya 2019 chini ya amri ya baraza la haki za kibinadamu la eneo la Malindi (Malindi Rights Forum), yaonyesha kwamba idadi ya mabirika ya chumvi katika ukanda wa uzalishaji chumvi eneo la Magarini, Kaunti ya Kilifi, imekuwa ikiongezeka.

Kati ya mwaka wa 1986 na 2000, ardhi iliyo chini ya mabirika ya chumvi iliongezeka kwa hekta 1159.38, na kati ya 2000 na 2018, iliongezeka kwa hekta 860.58.

Ripoti kwa jina Environmental Issues and Socio-economic Problems Emanating from Salt Mining in Kenya; A Case Study of Magarini District, iliyochapishwa na the International Journal of Humanities and Social Science Februari 2013, ilionyesha kwamba shughuli za uzalishaji chumvi huhusisha utoaji wa moja kwa moja wa maji ya chumvi kali kwa mazingira na kwenye mito pasipo kutibiwa.

Maji haya ya chumvi huathiri udongo, miongoni mwa athari nyinginezo.

Lakini kulingana na Kibiti Kirimi, mwenyeketi wa kitengo cha Chama cha watengenezaji bidhaa (KAM) kinachohusika na usafishaji chumvi, hayo hayajatendeka, na hakuna kemikali zinazotumika katika uvunaji chumvi.

“Chumvi huvunwa kupitia mvukizo wa miyale ya jua (solar evaporation). Miyale ya jua husaidia kuvukiza maji ya bahari kutoka kwa vidimbwi vyenye kina kifupi, na kuacha chumvi iliyoganda mle chini.”

Mbali na hayo, asema, viwanda vya kusafisha chumvi vimedumisha kinga ya kimazingira (buffer zones) katika maeneo ya uendeshaji shughuli zao kuambatana na mahitaji ya sehemu husika.

Aidha, aongeza kwamba viwanda vya kusafisha chumvi hufanya ukaguzi wa mazingira kila mwaka na kuwasilisha ripoti zao kwa NEMA.

“Athari zozote zingeonekana kwenye ripoti hizo, lakini kufikia sasa hatujapokea malalamishi yoyote,” aongeza.

Juhudi zetu za kutaka kuzungumza na NEMA kuhusu ripoti hizo hazikufaulu kwani hawakujibu barua pepe.

Kulingana na Sillus Oduor, mwanasayansi wa mchanga katika Idara ya mimea, ukulima wa bustani na udongo katika Chuo Kikuu cha Egerton, ongezeko la kiwango cha chumvi mchangani laweza kusababisha uharibifu wa mimea na hatimaye kuiangamiza kabisa.

“Chumvi huongeza kiwango cha pH mchangani na hivyo kuathiri kiwango cha virutubisho vinavyosambaa kwenye mmea,” asema.

Ishara za hali hii asema ni pamoja na mimea kudumaa, kukauka kwa majani, kupungua kwa kipenyo cha shina (shina kugeuka na kuwa nyembamba) kutokana na sababu kuwa haupokei maji.

“Ishara za kupungua kwa virutubisho pia zaweza ashiria athari za chumvi nyingi mchangani, vile vile mimea kunyauka na hatimaye kuangamia. Endapo viwanngo vya chumvi mchangani vitaongezeka zaidi basi kipande cha ardhi kilichoathirika kitabadilika na kuwa jangwa kwani kimepoteza kabisa uwezo wa kuhimili mimea,” aeleza Oduor.

Anasema kwamba kurejesha hali ya kawaida ni vigumu na ghali mno, na huenda ikachukua miaka kadhaa.

“Endapo mambo ni mabaya zaidi huenda ikawa haiwezekani kabisa kurejesha ardhi hii katika hali ya awali.”

  • Tags

You can share this post!

Mshindi wa EPL msimu huu huenda akapatikana katika wiki ya...

Mbunge ashinikiza Naibu Rais ajiuzulu

T L