• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Shiney apiga abautani akiweka zingatio kwa muziki wa Injili

Shiney apiga abautani akiweka zingatio kwa muziki wa Injili

NA JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika kazi zake na kutambulika kote duniani.

Anne Samba maarufu Shiney kamwe hajabaki nyuma licha ya pandashuka ambazo amepitia. Amepania kuibuka kati ya wasanii wenye sauti duniani. Bila shaka sura na sauti yake sio geni kwa wapenzi wa muziki wa densi hasa katika Kaunti ya Mombasa.

Baada ya kuwa katika muziki wa dunia kwa muda, mapema mwaka huu amegeukia kumtumikia Mungu ambapo ameanza kughani muziki wa injili.

”Kiukweli imekuwa ndoto yangu kumtumikia Mungu kupitia utunzi wa nyimbo za injili lakini muda mwafaka haukuwa umefika,” alisema na kuongeza kuwa ndio sasa Mungu amemfungulia mwanya huo.

Binti huyu tayari ameachia kibao cha kwanza kwa jina ‘Elohim’.

Fataki hii imerekodiwa Crystal jijini Mombasa inayomilikiwa na Jean Paul Kambale.

Ingawa ndio mwanzo ameanza kutunga nyimbo za injili, anaamini kuwa anatosha mboga kutinga kiwango cha kimataifa kwa uwepo wa Mungu Muumba.

Anadokeza kuwa amepania kutinga upeo wa marehemu Angela Chibalonza. Kwa wasanii Wakenya kama yeye, analenga kutinga hadhi ya Mercy Masika kati ya wengine.

Dunia analenga kufikia upeo ya wanamuziki mahiri kama Tasha Cobbs ambaye alitunga vibao kama ‘Fill me up God’ na ‘For your Glory’.

Kwenye jitihada za kujikuza katika muziki wa injili anasema angependa kufanya kolabo na wasanii kama Solomon Mkubwa, Goodluck Gozbert, Mercy Masika na Christina Shusho.

Ana mipango kibao katika muziki wa injili anakoshikilia kuwa wacha Mungu ajitukuze.

Anadokeza tatizo analofahamu katika muziki wa injili ni kwamba wasanii hukutana na watangulizi wao ambao hujiita Wakristo ilhali wamevalia ngozi ya kondoo maana roho zao huwa chafu.

”Sio wote wasemao Bwana ambao kiuhalisia huwa na mienendo ya Ukristo,” akasema.

Kwenye muziki wa densi alijivunia kughani vibao vingi tu ikiwamo: ‘Moyo’, ‘Ongea’, ‘Deka’ na ‘Te Amor’ kati ya nyimbo nyingine.

Katika mpango mzima kibao cha ‘Te Amor’ alichoachia mwaka 2021 kilipiga hatua kubwa katika safari yake kisanaa. Hata hivyo dada huyu anasisitiza kuwa licha kibao hicho kupata mapokezi mazuri kilichangia yeye kubadilisha safari yake kimuziki kwa maana ya kutoka kwa mtazamo wa kidunia.

”Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa hakuna cha maana ninachojivunia kutokana na muziki wa kidunia isipokuwa umaarufu pekee,” anasema na kuongeza kuwa analenga kupiga hatua katika muziki wa injili.

Anashikilia kuwa muziki wa dunia ulimsadia kujulikana vyema ambapo sio vigumu kujieleza kwenye biashara zake.

Mwanamuziki Anne Samba maarufu Shiney. PICHA | JOHN KIMWERE

Anasema katika muziki wa dunia alikutana na pandashuka kibao maana waliowatangulia waliibuka kizungumkuti.

”Sina hofu kutaja kuwa wengi wao hupenda kutumia wasanii wanaokuja kujifaidi wenyewe,” akasema na kuongeza kuwa sekta ya muziki ikiendelea hivyo hakika itakuwa mtihani kwa waimbaji chipukizi.

Kuhusu masuala ya mahusiano alikuwa ameolewa ila ndoa yake ilivunjika maana kwa maneno yake mwenyewe anasema alikuwa kama mtumwa.

  • Tags

You can share this post!

EPL: Everton walaza Leicester na kujiondoa katika hatari ya...

ODM, DAP-K wazozania Nyanza, Magharibi

T L