• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Shirika lazindua mpango kushirikisha vijana kutoa huduma za kilimo kidijitali

Shirika lazindua mpango kushirikisha vijana kutoa huduma za kilimo kidijitali

NA SAMMY WAWERU

SHIRIKA moja lisilo la kiserikali limezindua mpango utakaoshirikisha vijana kutoa huduma za kilimo kwa njia ya kidijitali.

Mpango huo, Digital Agriculture Champions (DAC) umeanzishwa na Heifer International.

Heifer hupiga jeki wakulima Afrika, ikiwa na malengo kukabiliana na janga la njaa na utoshelevu wa chakula.

Kulingana na shirika hilo, vijana watahusishwa kutoa mafunzo endelevu katika shughuli za zaraa.

DAC aidha inalenga wakulima wa mashamba madogo na yale ya kadri Barani Afrika, ili kupunguza gharama ya uzalishaji.

Kenya imeteuliwa nchi ya kwanza Afrika kuanza kutekeleza mpango huo.

Heifer inahamasisha wakulima kukumbatia mifumo ya teknolojia ya kisasa kuendeleza shughuli za kilimo, kuangazia hasara na changamoto zinazoibuka katika mtandao pana wa uzalishaji chakula.

Hatua hiyo inashirikisha huduma za kijiditali, wakulima waboreshe miradi yao.

Ukosefu wa huduma bora za zaraa hasa utoaji ushauri nasaha ni miongoni mwa mahangaiko wanayopitia wakulima wa mashamba madogo Afrika, ukumbatiaji mifumo ya kidijitali ukitajwa utawaletea afueni.

Ni kupitia mpango wa DAC, Heifer International inasisitiza vijana wataleta mchango mkubwa katika sekta ya kilimo.

“Wakipata mafunzo na kupigwa jeki, watasaidia kuboresha shughuli za kilimo kupitia njia za kidijitali. Wanaelewa kwa kina masuala ya teknolojia na wana ari kuvumbua mengi, wayasambaze shambani,” akasema Adesuwa Ifedi, makamu wa rais mkuu Heifer Africa wakati wa uzinduzi wa mpango huo.

Akiridhia uanzishaji wa DAC Africa maarufu kama Agriculture, Youth and Technology (AYuTe), Bi Ifedi alieleza imani yake mpango huo utasaidia kuangazia changamoto za wakulima.

“Utapevusha wakulima, wakumbatie mifumo na teknolojia za kisasa kufanikisha kilimo endelevu,” akasema.

Mojawapo ya mfumo wa kisasa wanaohamasishwa kukumbatia ni Bayoteknolojia, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hilo linajumuisha kupanda mbegu zilizoboreshwa na zenye ustahimilivu wa hali ya juu kwa kiangazi na magonjwa ibuka ya mimea.

“Vijana wakijumuishwa kwenye kilimo na ufugaji, wataleta mchango mkubwa katikia kuhakikisha taifa lina chakula cha kutosha,” akasema Mkurugenzi Mkuu Heifer Kenya, Bw George Odhiambo.

Naye Bw David Ojwang, Mkurugenzi Mkuu wa Mikakati, alisema matumizi ya mifumo na teknolojia za kisasa ikijumuishwa itafanya shughuli za kilimo na ufugaji kuwa na mvuto kwa vijana.

AYuTe pia ina tuzo ya Dola 1.5 milioni (sawa na Sh174, 150,000 thamani ya Kenya) kila mwaka, kwa vijana waliokumbatia mifumo na teknolojia za kisasa kuendeleza kilimo.

Heifer pia inashirikiana na Kuza Biashara, shirika la biashara za kijamii kidijitali, kufanikisha huduma za wakulima wa mashamba madogo kwa njia ya kidijitali.

You can share this post!

Gofu ya Safaricom Tour ya Karen yavutia wachezaji 280

Kamati ya Wekesa kumpokeza Raila majina matatu Alhamisi...

T L