• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
TAHARIRI: Covid: Matumizi ya pesa yaanikwe

TAHARIRI: Covid: Matumizi ya pesa yaanikwe

KITENGO CHA UHARIRI

WAKATI taifa la Kenya lilipoanza kushuhudia maambukizi ya virusi vya corona mwaka uliopita, mojawapo ya mikakati iliyoekwa ilihusu kuboresha miundomsingi katika hospitali za umma kila kaunti.

Rasilimali tele zilitumiwa kutekeleza mpango huo ambao ulihitaji serikali za kaunti kuongeza vyumba vya kulaza wagonjwa, vitanda, vyumba vya kutibu wagonjwa mahututi na kununua vifaa maalumu ambavyo vingetumiwa katika vyumba hivyo.

Hata hivyo, wakati huu ambapo maambukizi ya corona yameanza kuongezeka tena, tumesikia serikali ikitoa wito kama ule ule uliotolewa mwaka uliopita, kwamba hospitali ziimarishwe.

Swali linaloibuka ni kuhusu kama kweli mipango tuliyoona ikitekelezwa mwaka uliopita ilifaulu, ama yote yalikuwa ya kuvisha wananchi miwani za mbao. Tunasema hivi kwa kuwa, serikali kuu ilituma maafisa wake wengi kuzunguka katika kaunti mbalimbali ili kujionea jinsi maandalizi yalifanywa kuepusha uhaba wa vifaa endapo kungekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi.

Ripoti ya maafisa wa serikali wakati huo ilikuwa kwamba, kaunti zilikuwa zimejiandaa kwa kiwango cha kuridhisha pengine isipokuwa kaunti chache tu. Hii ni licha ya kuwa kulikuwepo ufichuzi wa mashirika mbalimbali yakiwemo ya habari ambapo ripoti zilitilia shaka kiwango cha maandalizi yaliyoekwa na serikali za kaunti.

Miongoni mwa ufichuzi ulikuwa kwamba kuna kaunti ambazo zilichukua vitanda vya shule na kuvipeleka katika hospitali wakati maafisa wa kaunti walipojua wakuu wa serikali walikuwa njiani kwenda kukagua mipango ambayo walikuwa tayari wametekeleza.

Lengo kuu la serikali lilikuwa ni kuepusha hali ambapo kaunti zingekosa miundomsingi bora wakati janga hili la Covid-19 lingelipuka zaidi, na hivyo kufanya wagonjwa kujazana jijini Nairobi. Hivi sasa, idadi kubwa ya wagonjwa ambao bado wanamiminika Nairobi kutoka kaunti za nje wakitafuta matibabu ya Covid-19 ni ishara kuwa kaunti hazikujiandaa jinsi ilivyodhaniwa.

Kwa msingi huu, inahitajika magavana wajitokeze wazi kueleza umma jinsi walivyotumia rasilimali zote ambazo walikuwa wamepewa kupambana na ueneaji wa virusi vya corona. Itakuwa ni aibu na ukatili usio kifani ikiwa itafichuka kwamba, kwa mara nyingine tena, kumetokea sakata ya ubadhirifu wa fedha kuhusu janga hili linaloangamiza maelfu ya watu nchini.

You can share this post!

Kenya Airways yatangaza hasara kubwa ya Sh36.6b

NGILA: Uhuru amuige Magufuli kutumia data kuzuia wizi