• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 11:13 AM
MUTUA: Serikali isithubutu kutoza ushuru raia walio ng’ambo

MUTUA: Serikali isithubutu kutoza ushuru raia walio ng’ambo

Na DOUGLAS MUTUA

BUSARA za Wakamba zinanikumbusha kila mara kwamba sifai kumgusa nyati sehemu nyeti ikiwa ninataka kuendelea kuwa hai.

Mswahili naye ananikanya kumtomasa simba.

Zote mbili ni tahadhari kwamba nisichezee kitu chochote hatari ikiwa siko tayari kukabiliana na matokeo mabaya ya mchezo huo.

Serikali ya Kenya, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisifia mchango wa Wakenya walio ughaibuni katika uchumi wa nchi, imeamua kumgusa nyati sehemu nyeti.

Imepanga kuanzisha vita na Wakenya wanaoishi nje ya nchi kwa kuandaa mswada ambao utatoza ushuru pesa ambazo wao hutuma nchini Kenya.

Hilo halijawakaa vyema Wakenya hao; kabla ya kutuma pesa hizo huwa tayari wametozwa ushuru, hivyo mpango huo wa Kenya utahalalisha haramu ya kuwatoza ushuru mara mbili.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya, pesa ambazo hutumwa na Wakenya hao nchini ni thuluthi moja ya jumla ya pesa za kigeni ambazo taifa letu hupata.

Hii ina maana kwamba hicho ni kiungo muhimu sana katika makuzi ya uchumi wa nchi hasa wakati huu ambapo umelemazwa na madhara ya janga la corona na deni la kigeni.

Benki Kuu yenyewe inakiri kwamba Wakenya wanaoishi ughaibuni huchangia pakubwa kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuwa kila unapopata matatizo, pesa zinazotumwa kutoka nje huongezeka.

Kisa na maana ni kwamba thamani ya shilingi ya Kenya ikiwa hafifu, wanaoishi kwenye chumi imara hutuma pesa nyumbani kwa kuwa kiwango cha ubadilishanaji mzuri kwao, hivyo hufika nchini zikiwa nyingi zaidi.

Kwa mfano, mwaka jana pekee ambapo chumi za dunia nzima zilipata pigo kutokana na janga la corona, Wakenya hao walituma nchini jumla ya Sh341 bilioni! Hilo ni ongezeko la asilimia 10.7 kutoka Sh308 bilioni zilizotumwa mnamo 2019.

Mijadala kwenye makundi ya Wakenya wanaoishi ughaibuni inasema kuwa iwapo mswada wa kuwatoza ushuru mara mbili utaidhinishwa kuwa sheria, watazua mbinu za kukataa kunyanyaswa.

Mathalan, wanaozuru Kenya mara mbili kwa mwaka ili kufuatilia miradi yao ya kibiashara wanatishia kuiuza na kuwekeza wanakoishi ambako kuna mazingira rafiki ya kufanyia biashara.

Hiyo ina maana kwamba hawatatuma pesa zozote nchini Kenya, na nafasi za kazi ambazo wamekuwa wakibuni nchini miaka hiyo yote zitakwisha kabisa.

Na kwa kuwa wengi tayari ni raia wa mataifa wanakoishi, wanasema watakuwa wakizuru Kenya mara moja-moja kama watalii ili kuonana na jamaa zao.

Wapo wanaotishia kutumia mbinu ya kutotuma pesa kabisa na kusubiri hadi watakaposafiri nchini ili waje na pesa taslimu wafadhili miradi yao.

Sheria za kimataifa zinamruhusu kila mtu kusafiri na kiasi cha Sh1.5 milioni, hivyo familia kubwa zinaweza kuamua kuzuru Kenya, kila mmoja akiwa na zake bila kutozwa ushuru ili kuwekeza wakifika Kenya.

Hii ina maana kwamba yale matarajio ya Benki Kuu ya Kenya kujumlisha kila mwezi madola ambayo humiminika nchini kila siku yatakwama. Uchumi utapata pigo.

Aliyetoa pendekezo hilo la kuwatoza Wakenya ushuru mara mbili, kwa kosa la kuishi ughaibuni pekee ambako wanazumbua riziki, anapaswa ama kuliondoa au kukomeshwa kabisa.

Wakenya hao wameanzisha harakati za kulishawishi Bunge ili liondoe mswada huo, lakini wamesisitiza ukijadiliwa na kupita watamhimiza rais asiuidhinishe kuwa sheria.

Hata hivyo, hawana matarajio makubwa kwa sababu Kenya ina mazoea ya kuwaonea wanaovuka mipaka na kuishi nje.

Mfano, Bunge linaishinikiza Serikali imfute Balozi wa Kenya nchini Korea Kusini, Mwende Mwinzi, kwa kuwa ana uraia wa Kenya na Marekani lau sivyo aukane huo wa Marekani.

Lakini kuna watu mashuhuri kama Bw Kalonzo Musyoka, Balozi Maalum wa Kenya nchini Sudan Kusini, na mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale, ambao pia wana uraia wa Cyprus na Somalia katika sanjari hiyo.

[email protected]

You can share this post!

Trump kuhutubia mkutano akilenga kuwania tena 2024

TAHARIRI: Dawa ya tatizo la michezo ni ufadhili