• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
TALANTA: Gwiji wa zumari

TALANTA: Gwiji wa zumari

NA PATRICK KILAVUKA

ALIONESHA kwamba uwezo wa kutumia mikono waweza kuwa wa heri katika kutimiza ndoto alipoibuka bora katika mashindano ya Tamasha za Muziki za shule za msingi kaunti ndogo ya Dagoretti.

Mashindano haya yaliandaliwa katika shule ya msingi ya Kinyanjui na ya Kanda ya Nairobi ambayo yalifanyika shule ya msingi ya Westlands kwa kuzoa alama 80 na 85 mtawalia na kufuzu kwa awamu ya kitaifa itakayoandaliwa Kisumu.

Akiwa mweledi wa kucheza zumari au Chivoti, Broline Oketch,11, ana matamanio na kiu ya kuwa mwanamuziki kwa kujitolea zaidi ili afanikishe azma yake kitaaluma.

Oketch ni mwanafunzi wa gredi ya tano katika shule ya msingi ya Gentiana, Dagoretti.

Yeye ni mwanambee katika familia ya watoto wawili wa Bw Humphrey Coath na Bi Merciline Anyango.

Ushawishi wa kucheza chombo hiki ulitokana na kiini cha kuwa na mshawasha wa kucheza zumari na mwalimu wake wa somo la muziki katika mtaala mpya wa Umilisi.

“Naona kama ni rahisi kupuliza chombo hiki huku nikitumia vidole vya mikono yangu pamoja na kudhibiti ala hii kutoa sauti na tyuni mbalimbali kuvutia au kusisimua hadhira,” anasema Oketch.

Anaongeza kwamba, ametiwa mori zaidi na mwalimu wake ambaye amemuandaa pia kwa mashindano na ameona akisonga hatua kwa hatua hadi anapoenda kupeperusha bendera ya gatuzi la Nairobi katika mashindano ya kitaifa.

Mchezaji stadi wa chivoti Broline Oketch. PICHA|PATRICK KILAVUKA

Alijua kupuliza chivoti baada ya muda wa wiki moja.

Kwa mujibu wa mwalimu wake Patrick Agunda ambaye analea kipaji chake kwa kumshirikisha katika mashindano, amejizatiti sana kujiongezea umahiri katika muziki huu.

Mambo ambayo anamkuza kwayo ni yale ambayo waamuzi waliyagusia katika ukaguzi wakati wa mashindano ya mwaka huu na yamemwezesha kupata sifa sufufu na kuwa na mwanzo wa mvuto katika kucheza toni nzuri na udhibiti mwema wa steji mbali na kuhimizwa atie juhudi katika kuwa na tyuni nyingine.

Mchezaji stadi wa chivoti Broline Oketch (kulia) akiwa na Mwalimu Patrick Agunda. PICHA|PATRICK KILAVUKA

Aidha, amechochewa na mawaidha ya mkufunzi wake, kutia bidii ya mchwa na kutazama video ambazo zina mafunzo kuhusu uchezaji wa ala.

Yeye hula vyakula vyenye wanga na kunywa maji mengi kumpa nguvu za kupuliza ala.

Changamoto yake kuu ni nafasi finyu ya kujinoa wakati huu ambapo mtaala wa masomo umembana.

Ushauri wake ni kwamba mwenge ambao unawasha katika kutekeleza wajibu wowote haufai kuuzima badala yake unafaa kutia bidii na kujinyanyua pasi na kukata tamaa.

You can share this post!

Gachagua aingia Harambee House Annex kwa kicheko na tabasamu

Brighton waajiri kocha Roberto de Zerbi kujaza nafasi ya...

T L