• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
TALANTA YANGU: Favour ni nyota katika uigizaji

TALANTA YANGU: Favour ni nyota katika uigizaji

ANASEMA kukipenda unachokifanya ni njia ya kukuza hamu na ari ya kukifanya kwani kipendacho roho hula nyama mbichi.

Kukitilia maanani kipaji chako ndiko kukipalilia kwani, kila kitu ambacho kinafanikishwa, huhitaji kukuzwa kwa njia moja au nyingine.

Msanii mwigizaji Favour Chepchumba mwenye umri wa miaka sita, anasema uigizaji ni jukwaa la kutoa jumbe na hoja ambazo zinaweza kuburudisha, kupumbaza, kuelimisha na kukuza maadili mema katika jamii kwani mwigizaji ni kielelezo cha jamii.

Mwanafunzi huyu wa Gredi ya pili katika shule ya msingi ya Junel, Kabete, Kaunti ya Kiambu na mwanambee katika familia ya watoto wawili wa Bw Phelmon Ngeno na Bi Beartrice Chebet Ngeno, anasema alianza kuuenzi uigizaji akiwa Gredi ya Kwanza baada ya kuonesha nia, hamu na ghamu ya kujua na kujitambua kitalanta.

Hii ilikuwa baada ya mwalimu Josephine Akatu kuwajaribu katika uhusika na kubainisha mbivu na mbichi kwamba, ana kipaji cha usanii wa fani ya uigizaji na kilikuwa kimeota ndani mwake ingawa kilihitaji tu kutiwa makali kwa kuchochewa zaidi.

Alimhusisha katika michezo kama Hyiene, Three Wishes na Birth of Jesus ambapo alishiriki kwa weledi akiwa mhusika mkuu.

Kwa mfano, aliigiza nafasi ya Maria – mama wa Yesu na kuonyesha ukomavu katika kuigiza uhusika huo sawa na mwigizaji mzoefu – aliuigiza kwenye hafla shuleni.

Ni kupitia uigizaji ambapo anasema amepata uzoefu wa kukariri mashairi. Ujasiri huo ambao yeye hupata mbele ya hadhira umemfanya kuwa na ukakamavu katika kufanya mambo na masomoni pia. Kwa sasa, haogopi na ana uwezo wa kuuliza maswali darasani kama njia ya kujifunza zaidi.

Isitoshe, ametambua kwamba, kupitia uigizaji amefunguka sana kimasomo na hata kiwango chake cha masomo kimeinuka.

Si kwamba tu anaigiza bali ameanza kuwa na kiu ya kuandika mashairi na kupenda kufanya na mazoezi ya kuigiza kutokana na vile ambavyo anawaona waigizaji mahiri kwenye runinga wanafanya makeke ya sarakasi kama njia ya kujiongezea maarifa katika fani hii.

Macho yake hayakosi uhondo wa vipindi vya Akili Kids na Ubongo Kids runingani kwani, ni kupitia vipindi hivyo ambapo yeye hupata pia mbinu zake za uigizaji.

Favour asema kuwa, yeye hupenda kufanya mazoezi ya kila siku katika fani hii kama njia ya kujiimarisha zaidi kwa sababu mazoezi ni kiungo thabiti cha kukufanya uwe imara zaidi.

Katika kuigiza, anasema mwalimu wake humuonesha pia jinsi ya kukonyeza jicho na kumfaa kwa stadi za sauti za uigizaji kama njia ya kuboresha na kufanya uigizaji wake kuwa wa kuvutia na kutia fora hali ambayo imemkuza zaidi.

Zaidi ya hayo, amempa uhusika na nafasi ya kujiangazia katika hafla ainati shuleni kama njia yae kujipatia uzoefu katika majukwaa ya uigizaji.

Mbali na kuigiza shuleni, anasema yeye hushiriki pia katika kanisa la Deliverance, Nairobi na huwa radhi kushiriki katika michezo ya kuigiza na kukariri mashairi.

Chepchumba angependa kuwa mwalimu siku za majaliwa kwa sababu anaamini kwamba mwalimu ni mtu ambaye ana mwito wa kulea wanajamii walio bora katika jamii na taifa.

Aidha, anasema umuhimu wa mwalimu ndio unamwezesha kuweko kwa wanataaluma mbalimbali ambao wamepitia mikononi mwake.

Wazazi wake wamekuwa mhimili mkuu katika kumwezesha kufaulu katika ndoto ya kuigiza kwani wamempa kila msaada na kumtia motisha wakijua kwamba, uigizaji pia ni fani ambayo inaweza kumzolea riziki.

Ushauri wake ni kwamba, uigizaji humwezesha mja kuwa na njia ya kufanya maamuzi kwani uamuzi bora huleta mafanikio na maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni ya Kadmus Freight yaokoa timu kwa ligi ya FKF

Washukiwa 8 washtakiwa kwa wizi wa mikopo ya Fuliza

T L