• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kampuni ya Kadmus Freight yaokoa timu kwa ligi ya FKF

Kampuni ya Kadmus Freight yaokoa timu kwa ligi ya FKF

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KAMPUNI ya Kadmus Freight inayosimamia utoaji mizigo katika Bandari ya Mombasa, imesaidia pakubwa kuokoa hatima ya timu ya Mombasa Olympics Ladies FC kubanduliwa nje ya ligi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Timu hiyo ilishuka ngazi kutoka Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake hadi Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza, sio kwa sababu ilikosa pointi za kutosha ila ni kutokana na kukosa kucheza mechi tatu.

Mombasa Olympic iliteremshwa ngazi na FKF baada ya kushindwa kucheza mechi tatu za ugenini, hivyo ikapata kipigo cha sheria ya ligi ya kubanduliwa nje ya ligi na kuteremshwa ngazi msimu ufuatao.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, timu hiyo ilikodolewa macho na marudio ya kisa aina hiyo, kwani ingelikosa kwenda kucheza ugenini jijini Nairobi kwa mechi yao dhidi ya Sunderland Samba jana (Jumapili).

Ni kutokana na kujitokeza kwa kampuni ya Kadmus Freight kupitia kwa Mkurugenzi wake Musa Mbira, iliiokoa timu hiyo kutotoa alama tatu za bwerere kwa wapinzani wao wa Sunderland kwa kuwapa kitita cha Sh75,000 kwa ajili ya timu kusafiri hadi Nairobi.

Katika hafla fupi ya kutoa hundi ya msaada huo iliyofanyika ukumbi wa Makande Estate mnamo Ijumaa iliyopita, Bw Mbira aliwaambia wachezaji wa timu hiyo kuwa wamejitolea kuwasaidia kutokana na kuwaona wasichana hao wana hamu na wanapenda kuendeleza vipaji vyao.

“Nimevutiwa zaidi kuona wachezaji pamoja na maafisa wenu wanashirikiana na wana nidhamu za hali ya juu. Ninaamini kama mtaendelea hivi, tutasimama nanyi kuwasaidia na pia kuwatafuta marafiki zangu wapate kuwasaidia ili muondokewe na matatizo yenu,” akasema.

Mkurugenzi huyo wa Kadmus Freight alisema atafanya bidii kuona timu hiyo inajitegemea ili ikamilishe mechi zake zote za ligi zikiwemo zile za ugenini.

Afisa wa huduma za bandarini na mauzo katika kampuni hiyo, Bw Oliver Ouma, aliwasifu wanasoka na viongozi wao kwa kushikamana na kuvumilia matatizo yanayowakabili. Aliwapa moyo kuwa utafika wakati matatizo hayo yatakuwa historia.

Aliyekuwa kiongozi wa soka wa Mombasa na Pwani zamani, Bw Raghib Kassim, alimtaka Meneja wa Benki ya Equity tawi la KPA, Bi Irene Kanati aliyekuwako katika hafla, awe mlezi wa timu hiyo na kuisaidia kwa njia ambazo ataweza.

“Naamini ukiwa mwanamke, utawasaidia hawa wasichana wapate kuinua vipaji vyao vitakavyowafanya waajiriwe hata kucheza soka huko ng’ambo,” akasema.

Mweka Hazina wa Mombasa Olympic FC, Aziz Bobby, kwa niaba ya maafisa wengine, aliishukuru kampuni hiyo ya Kadmus kwa kuiokoa safari yao.

“Naamini Kadmus itaendelea kusimama nasi. Hawa wasichana wanataka kucheza soka na kujiimarisha lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa udhamini, nina imani sasa tutapata usaidizi zaidi,” akasema.

Mkurugenzi wa Kadmus Freight, Musa Kadmus (kushoto) akiwahutubia wachezaji na maafisa wa Mombasa Olympic Ladies FC. PICHA | ABDULRAHMAN SHERIFF

Klabu hiyo imetoa wachezaji kadhaa wenye vipaji wakiwemo wale wanaochezea timu ya taifa ya Harambee Starlets wakiwemo kina Mwanahalima Adam na Mbeyu Akida ambao wanapiga kigozi huko barani Ulaya.

Maafisa wa klabu hiyo waliokuwako katika hafla hiyo ni meneja wa timu Harun majied, naibu katibu ambaye pia ni naibu kocha Jumanne Masika, afisa wa nidhamu Elizabeth Owira, kocha mkuu Christine Nanjala, trena wa makipa Michael “Wenger” Kalume na trena wa misuli Ustadh Musa.

  • Tags

You can share this post!

Chai ya muasumini na manufaa yake kwa binadamu

TALANTA YANGU: Favour ni nyota katika uigizaji

T L