• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
TALANTA YANGU: Rais mchoraji

TALANTA YANGU: Rais mchoraji

NA PATRICK KILAVUKA

KIONGOZI anafaa kuwa kielelezo kwa jamii.

Kujitolea kuwa kiongozi kuna maana ya kubeba mzigo wa wale unaowaongoza, japo changamoto zaweza kukunyemelea, unahitaji nidhamu na unyenyekevu.

Haya ni kwa mujibu wa Bruce Kayi, 19, Rais na mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi ya Kawangware, kaunti ndogo ya Dagoretti Kaskazini, Kaunti ya Nairobi. Licha ya kuwa kiongozi shuleni, yeye pia ni mchoraji hodari.

Rais Kayi anasema changamoto kubwa iliyomtikisa mno ni wakati alimpoteza mzazi. Kifo hiki kiliyumbisha masomo yake japo alijitia moyo kwamba, wakati wa Maulana ndio hufaa maishani kwa kila tukio limpatalo mja!

Anasema kwamba akiwa na miaka 12, alihangaika sana akitafuta namna ya kujiendeleza kimasomo hadi alipojiunga na anakosomea kwa sasa na kurudi hadi darasa la pili. Pasi kujali umri wake, alijikakamua kujinyanyua kimasomo na sasa ananawiri.

Baadaye milango ya heri ya Mola ilianza kufunguka na wakati huo ndipo nyota yake ya uongozi ilianza kumuandama kwani, amekuwa kiranja hadi sasa ambapo ni rais wa shule.

Alichaguliwa kuwa rais muhula wa pili 2021, baada ya kumshinda mpinzani wake wa karibu Warida Yumi kwa kura 21 kwa 10 katika kura zilizopigwa na makatibu wa wizara shuleni.

Anasema sera alizonadi kwa wanafunzi za maadili mema na kutetea wanafunzi wengine shuleni ndizo zilikuwa mvuto wake kwa wapigakura.

Pia, udumishaji nidhamu, usalama wa wanafunzi wengine dhidi ya dhuluma, uhimizaji wa jitihadi katika masomo na kufanya mambo kwa utaratibu ufaao, kujukumika, mazingira safi, uwiano mwema na kusaidia wanagenzi kuzingatia utiifu kwa walimu ni sera zilizomjenga msingi bora wa uongozi na kupendwa na wanafunzi pia.

Ili kuongoza baraza lake la mawaziri, yeye hukongamana nao Jumatano na Ijumaa kutunga mikakati ambayo itaimarisha utendakazi.

Nyadhifa ambazo amewahi kushikilia kabla ya kuwa rais ni kiranja na gavana.

Changamoto ambayo hupata ni kujitahidi kuleta mtagusano mwema kati ya wanafunzi wa darasa la nane ambao anawaongoza licha ya kuwa darasa moja nyuma yao.

Nia yake ni kuona shule anayoongoza inakuwa mahali salama kwa wanafunzi kujihisi kwamba ni kwao na wanastahili kusoma katika mazingira hayo na kupitia mitihani kuinua jina la shule katika viwango mbalimbali.

Mbali na kuwa kiongozi, yeye ni mchoraji stadi. Yeye hupenda kuchora michoro halisi ya vitu, wanyama, ndege na watu. Alianza uchoraji baada ya kuchochewa na mwanafunzi mwenza Simon Mutisya mwaka wa 2014 aliyekuwa akichora vibonzo.

Mchoro wake wa kwanza ulikuwa wa kocha wa kriketi wa shule na ulimwezesha kupata Sh1,000 baada ya kumuuzia.

Kwa uelekezi wa mwalimu wake Rashid Bakari, amepiga hatua si haba.

“Yakaribia mwaka mmoja tangu nianze kumuelekeza na nimeona kipaji cha ajabu na adimu ndani yake na ninapania kukichochea hadi kifike upeo wa juu,” anasema Bakari ambaye anamfunza pia namna ya kupaka rangi michoro.

Kiongozi na mchoraji hodari huyu anasema kwamba kipawa kinalipa iwapo mhusika atajihadi kwa udi na uvumba, kutafuta ushauri kwa watangulizi wake pamoja na kufukuzia ndoto yake.

You can share this post!

Wolves wang’ata Leicester City ligini

Man-United wakomoa Leeds United baada ya kuponea ugani...

T L