• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Man-United wakomoa Leeds United baada ya kuponea ugani Elland Road

Man-United wakomoa Leeds United baada ya kuponea ugani Elland Road

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United walihimili makali ya Leeds United na kuondoka ugani Elland Road na alama tatu kutokana na ushindi wa 4-2 ulioweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora.

Ingawa Man-United walijivunia uongozi wa 2-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Leeds walirejea mchezoni mwazoni mwa kipindi cha pili baada ya kufunga mabao mawili ya haraka kupitia kwa Rodrigo Moreno na Raphinha Belloli.

Awali, Man-United walikuwa wamefungiwa mabao yao na Harry Maguire na Bruno Fernandes kutokana na michango ya Luke Shaw na Jadon Sancho mtawalia.

Ingawa Leeds walivamia zaidi lango la Man-United baada ya kusawazisha, chombo chao kilizamishwa haraka na mabao kupitia kwa Fred na Anthony Elanga.

Mabingwa hao mara 20 wa taji la EPL sasa wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 46, nne nyuma ya Chelsea ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi 26 ambazo tayari zimesakatwa na Man-United.

Leeds kwa upande wao wanakamata nafasi ya 15 jedwalini kwa alama 23, mbili zaidi kuliko Everton na Newcastle United.

Chini ya kocha mshikilizi Ralf Rangnick, Man-United sasa wapo pazuri kupiga kumbo West Ham United, Arsenal na Tottenham Hotspur ambao pia wanapigania fursa ya kukamilisha kampeni za EPL muhula huu ndani ya orodha ya nne-bora.

Mashetani wekundu wa Man-United walikuwa wamecharaza Brighton 2-0 katika pambano la awali la EPL, siku chache baada ya Middlesbrough kuwadengua kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA na kuzima kabisa ndoto yao ya kujizolea taji lolote msimu huu.

Baada ya kuwakomoa Leeds, Man-United sasa wanajiandaa kuwa wageni wa Atletico Madrid kwenye mkondo wa kwanza wa gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 23, 2022 nchini Uhispania.

Mabingwa hao mara 20 wa EPL hawajaangushwa katika mechi saba zilizopita ligini. Wameshinda michuano minne kutokana na sita iliyopita na hawajapoteza gozi lolote la EPL ugenini tangu Watford wawapige 4-1 mnamo Novemba 20, 2021. Aliyekuwa mkufunzi wao, Ole Gunnar Solskjaer alitimuliwa baada ya kichapo hicho kutoka kwa Watford.

Leeds wanaotiwa makali na kocha Marcelo Bielsa wameshinda mechi tano, kuambulia sare mara nane na kupoteza michuano 11 kati ya 24 iliyopita ligini. Sasa wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi msimu huu iwapo watashindwa kuhimili presha kali kutoka kwa Everton na Newcastle United.

Kikosi hicho kilikamata nafasi ya tisa katika EPL mnamo 2020-21 kiliporejea ligini baada ya kuwa nje kwa miaka 16. Licha ya kuangusha Burnley na West Ham United mnamo Januari, Leeds wamejizolea alama moja pekee kutokana na mechi nne zilizopita.

Pointi hiyo ilitokana na sare ya 3-3 baada ya Newcastle kuwapepeta 1-0 na kabla ya Everton kuwatandika 3-0. Wana mtihani mgumu zaidi dhidi ya Liverpool na Spurs katika mechi mbili zijazo ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TALANTA YANGU: Rais mchoraji

Muturi azindua rasmi azma ya urais, akataa miungano kabla...

T L