• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Thamani ya kofia za vito si mzaha!

Thamani ya kofia za vito si mzaha!

NA KALUME KAZUNGU

KILA Ijumaa utawapata wanaume wa Kiislamu wakivalia kanzu na kofia za vito kuelekea msikitini kwa sala.

Uvaliaji wa kofia hizi hushuhudiwa sana pia wakati wa sherehe na hafla nyingine muhimu za Kiislamu.

Lakini, je, ushawahi kufikiria kwa nini kofia hizi huwa bei ghali, kuanzia Sh8,000 hadi zaidi ya Sh40,000?

Uchunguzi wa Taifa Leo katika Kaunti ya Lamu ambapo ndipo kitovu cha ushonaji kofia za vito humu nchini, umebainisha kuwa thamani yao si ya kawaida, huenda ikawa ndio maana zikapewa jina ‘vito’.

Bw Ali Ismael, anaeleza kuwa ufundi au ujuzi wa kutengeneza kofia za vito, ambao sio rahisi, chimbuko lake ni visiwa viwili vya Lamu ambavyo ni Pate na Kizingitini. Ujuzi huo baadaye ulisambaa hadi kwenye visiwa vya Siyu, Shella, Matondoni, Tchundwa, Rasini na Ndau. Pia utapata wajuzi kadha wa kutengeneza kofia za vito mjini Mombasa na Zanzibar.

Gharama ya kutengeneza kofia hizi hadi kukamilika kwake hutegemea mtindo au upekee ambao mteja anataka, na hii ndiyo huamua bei itakayouzwa. Ushonaji hufanywa kwa ustadi kwa mkono, na hivyo basi kofia moja huchukua muda mrefu kukamilika.

“Hizi ni kofia za asili ya Lamu. Mababu zetu walioanza kuzitengeneza miaka ya 1730 walipitisha ujuzi huo kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine,” anasema Bw Ismael.

Kulingana na Bw Yusuf Salim, kofia za kisawasawa huchukua kati ya miezi miwili au mitatu kukamilika. Ni katika muda huo ambapo kofia hupitia mikono mingi na awamu tofauti za washonaji wenye ujuzi mbalimbali, ambapo kila mmoja hushona sehemu yake na kujipatia riziki kivyake.

Lingine linalochangia bei ya juu ya kofia za vito ni muda wa kudumu wa kofia baada ya kuuzwa. Bw Salim anasema kofia ya kisawasawa ukiitunza vyema huenda ukaivalia na kudumu nayo kwa kati ya miaka 10 hadi 20.

“Yote yatategemea namna utakavyoivalia, kuifua, kuihifadhi na kuitunza kofia,” akasema Bw Salim.

Abdulqadir Omar Banyenye, ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza, kufua na kutunza kofia za vito mtaani Mkomani kisiwani Lamu, anaeleza kuwa, ushonaji huanza kwa mshadhari. Mshonaji huanza kwa kuchora maua kwa mkono akitumia kalamu.

Mbali na sindano, vifaa vingine vinavyoambatana na ushonaji wa kofia ya vito ni mwiba wa nungu au kidungumaria na dondo.

Mwiba wa nungu hutumiwa kutoboa vishimo vidogo vinavyojulikana kama vito.

“Ili kofia ipendeze, sharti ishonwe kwa mkono. Kila nafasi inajazwa kwa kuufuata mshadhari. Baada ya hapo kila kipande cha kofia kinapigwa dondo ili isifurefure. Kuzuua ndio hatua ya mwisho inayovitoboa vito vya kofia au kuvizibua kwa kutumia mwiba wa nungu,” akasema Bw Banyenye.

Anasema nakshi za mshadhari hutegemea ujuzi na ubunifu wa mshonaji.

“Kuna awamu ya kutia uzi ambayo huipa kofia ugumu na umbo zuri. Uzi wenyewe ni mahsusi kwa nakshi na ni wa rangi tofauti tofauti. Uzi unaotumiwa huwa ni wa kitambara kifahamikacho kwa jina lasi. Kuna sindano yake itumiwayo kushonea kito ili kipendeze,” akasema Bw Banyenye.

Ujuzi wa kutengeneza vazi hilo umekuwa kitega uchumi kwa wengi katika jamii.

Bi Khadija Hakofa Dawa, 63, mkazi wa mtaa wa Kandahar ambaye amekuwa fundi wa kushona kofia ya vito kwa zaidi ya miaka 40, anasema ili kuthibitisha kuwa kofia iliyokamilika haijavaliwa, mara nyingi mshonaji humkabidhi mteja wake kofia hiyo ikiwa vipande viwili ili aunganishe mwenyewe.

“Hatimaye mteja ataunganisha mshadhari na kahafu mwenyewe, hivyo kofia kuwa tayari kuvaliwa,” akasema Bi Dawa.

Kofia hiyo haifuliwi kwa kutumia maji ya kisima au kufikinywa kama nguo za kawaida.

Mwenye kofia ya vito anapaswa kutumia maji safi, ikiwezekana iwe ni yaliyosafishwa ambayo huuzwa kwa chupa kwa matumizi ya kunywa.

Hatua ya kwanza katika kuifua ni kuiloweka kwa maji hayo safi kwa kutumia sabuni ya unga au majimaji kwa kati ya saa nane au hata siku nzima ili iwe chepechepe.

Mtaalamu wa kofia za vito Lamu, Abdulqadir Omar Banyenye akionyesha mojawapo ya kofia za vito na baadhi ya vifaa vinavyotumika kutengenezea aina hiyo ya kofia. PICHA | KALUME KAZUNGU

Baadaye unatumia maji hayo kuifua kwa kupapasa ukitumia viganja au dondo badala ya kufikicha kama nguo za kawaida.

Ifahamike kuwa mara nyingi kofia ya vito unapoivalia huchafuka kwenye sehemu ya ukingo wa chini, hivyo kuna haja ya mfuaji kuipinda kwa ndani na kuisafisha kwa viganja vyake au kwa kutumia dondo. Kisha unaimwagia maji safi, uikunje kwa ustadi na kuiweka katikati ya viganja, ambapo utaibana itoke maji.

Kofia ya vito haianikwi juani bali husimamishwa kwenye sinia safi na kuwekwa kwenye chumba, kibaraza au chini ya mti penye hewa safi, ambapo itakauka kwa utaratibu.

“Ukifuata njia hizi za kuitunza kofia ya vito basi utadumu nayo kwa zaidi ya miaka 20. Yaweza hata kurithiwa na watoto na wajukuu wako,” Bw Faiz Abdallah, mtaalamu anaeleza. Ukubwa wa kofia ya vito huanzia saizi 20 na hadi 24.

Kaunti ya Lamu kila mwaka huandaa mashindano ya washonaji, ambapo washindi hutuzwa kwa kati ya Sh3,000 hadi Sh20,000 ili kudumisha desturi ya ushonaji.

“Huwezi kumuona mtu amevaa kofia ya vito ovyo ovyo. Ni kofia ambayo hata kukiwa na msako wa polisi mitaani waweza kuachwa uendelee na shughuli zako kwani kofia hukupa mwonekano wa mtu wa heshima na mtulivu,” anaeleza Bw Ahmed Omar.

  • Tags

You can share this post!

‘First Choice’ yasema dili zake za kutafutia...

MKU yawatafutia ajira ya ng’ambo wahitimu 15

T L