• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Uongezaji thamani kwa maziwa unaimarisha kipato, wafugaji wahimizwa

Uongezaji thamani kwa maziwa unaimarisha kipato, wafugaji wahimizwa

NA SAMMY WAWERU

SEKTA ya ufugaji ni pana, kuanzia ufugaji wa mbuzi, kondoo, kuku na nyuni, hadi ng’ombe, listi hii ikiwa fupi kuorodhesha.

Mazao ya kuku na ng’ombe hata hivyo ndiyo yenye mashabiki wengi, yaani mayai na maziwa mtawalia.

Katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, wapo wanaouendeleza kukithi mahitaji ya familia na wengine ufugajibiashara.

Huku lita moja ikichezea kati ya Sh33 – 40, bei ya langoni anayouza mkulima, wataalamu katika masuala ya uongezaji thamani wanahoji bidhaa za kinywaji hicho zilizosindikwa zina soko lenye ushindani mkuu.

Hellen Kamba, mtaalamu katika uzalishaji wa bidhaa za mifugo, anasema bidhaa za maziwa soko lake haliwezi kulinganishwa na yale freshi.

Mdau huyu anataja mianya tele ya ajira hasa kwa vijana inayotokana na kusindika maziwa.

“Kando na maziwa ya mtindi (yoghurt) na yaliyochacha (lala), jibini (cheese), siagi (butter) na krimu ni kati ya bidhaa za maziwa zenye mashabiki wengi. Hivyo basi nafasi za kazi katika mtandao huo wa uongezaji thamani, kuanzia wanaozisindika, usafirishaji na kuuza, ni tele,” aelezea mdau huyo.

Hellen ni mtaalamu wa masuala ya uzalishaji maziwa na kuyaongeza thamani, aliyesomea katika taasisi inayoangazia Masuala ya Maziwa ya Ng’ombe Nchini (DTI).

“Aliyeanza kwa kusindika lita 50 za maziwa kwa siku, akakwea hadi 100, 500 na sasa anafanya lita 1, 000, ina maana kuwa biashara yake imekua. Kazi ni nyingi na atahitaji wafanyakazi zaidi,” afafanua.

Hellen anasisitiza sekta ya maziwa ina mianya chungu nzima ya ajira, wanachohitajika wahusika kikiwa hamasisho na kupigwa jeki kupata mtaji na mashine za kuongeza thamani.

Comrade Dairy and Food Enterprises, ni kampuni inayomilikiwa na vijana watatu: Gabriel Kwendo, Emmanuel Ogise na Joseph Bosire kutoka Njoro, Kaunti ya Nakuru, ambayo huunda maziwa ya mtindi na lala.

Maziwa ya mtindi yanayoundwa na Comrade Dairy and Food Enterprises. Bidhaa za maziwa ya ng’ombe zilizosindikwa zinateka soko lenye ushindani mkubwa. PICHA | SAMMY WAWERU

Wafanyabiashara hao wanataja ukosefu wa fedha za kutosha kuwekeza katika mashine na mitambo ya kisasa kuongeza thamani, kama baadhi ya changamoto wanazopitia.

“Tukipata vifaa na mashine zilizoboreshwa, tutarahisisha kazi, kuongeza kiwango cha uzalishaji ikiwa ni pamoja na kubuni ziaidi nafasi za ajira,” vijana hao wasema, wakiomba wasamaria wema kujitokeza kuwapiga jeki.

Wajasirimali hao kwa sasa wameajiri vijana kumi.

Ukosefu wa mtaji miongoni mwa vijana ni kati ya changamoto wanazopitia, hali hiyo ikiwazuia kuanzisha biashara.

Licha ya serikali kudai ina mipango ya kuwapa mikopo isiyotozwa riba, na nyingine yenye riba ya chini, vijana wanalalamikia mikakati iliyowekwa kuifikia kuwa kikwazo kikuu.

 

  • Tags

You can share this post!

Joylove FC yapigwa jeki vifaa vya kuchezea

Hofu baadhi ya karatasi za kura zikikosekana

T L