• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Urais milele: Siri kali ya Ruto dhidi ya Azimio

Urais milele: Siri kali ya Ruto dhidi ya Azimio

NA BENSON MATHEKA

INGAWA Rais William Ruto anasemekana kukanusha kwamba ananuia kubadilisha katiba ili kuongeza muhula wake wa kuhudumu kama rais, pendekezo hilo linaendelea kuzua mjadala mkali huku wadadisi wakisema ajenda ya sheria ya muungano tawala itafuatiliwa kwa makini.

Mbunge wa Fafi, Bw Salah Yakub alizua mjadala huo kwa kusema kuwa chama cha Rais Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) kinaandaa mikakati ya kubadilisha katiba kwa lengo la kuondoa mihula miwili ya rais kuhudumu huku kikiweka umri wa juu wa rais kustaafu kama kigezo cha kuwania wadhifa huo mkuu nchini.

Ingawa UDA kupitia kwa mwenyekiti wake Johnson Muthama ilitaja matamshi ya mbunge huyo kama ya kibinafsi, kuna minong’ono kwamba mipango hiyo imekuwa ikisukwa chini kwa chini na washirika wa karibu wa Rais Ruto wanaohisi kwamba hata baada ya kuhudumu kwa mihula miwili, atastaafu akiwa na umri mchanga wa miaka 65.

Dkt Ruto alichukua muda kabla ya kuzungumzia suala hilo na alipofanya hivyo Jumatano iliyopita, ilikuwa katika mkutano wa kundi la wabunge wa muungano tawala wa Kenya Kwanza aliponukuliwa akisema lengo lake sio kukwamilia mamlakani bali ni kuhudumia Wakenya.

Kwa kiongozi anayefahamika kwa kujibu hadharani masuala yanayoibua joto la kisiasa, uamuzi wake wa kutoangazia suala hilo katika hafla nyingi za umma anazoongoza umeacha wadadisi wa siasa na maswali hasa baada ya kusemekana kuwa aliwaambia wabunge wa muungano wake wavuruge muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Kulingana na duru kutoka katika mkutano wa wabunge wa Kenya Kwanza uliofanyika Ikulu ya Nairobi Jumatano, Rais aliwaagiza wawinde angalau wabunge 59 wa Azimio ili kurahisisha ajenda ya sheria ya Kenya Kwanza. Hii, kulingana na duru katika mkutano huo, inanuiwa kuupa mrengo wa Rais idadi ya kutosha ya wabunge kufanikisha mageuzi ya katiba.

Mswada wowote wa kubadilisha katiba, ukiwemo wa kuondoa muhula wa rais kuhudumu, ni lazima uungwe mkono na wabunge 233 ili uweze kufaulu.

“Hii inaweza kuwa sehemu ya ajenda za baadhi ya wakereketwa katika muungano wa Kenya Kwanza lakini inaonekana Rais amewakanyagia breki baada ya pendekezo la Bw Yakub kuzua joto,” asema mbunge mmoja wa Muungano Tawala kutoka Magharibi mwa Kenya.

Kulingana na mwanaharakati Boniface Mwangi, pendekezo la mbunge huyo halikuwa lake binafsi jinsi UDA inavyotaka Wakenya kuamini.

“Juhudi zote za kubadilisha katiba kumfanya Ruto kuwa rais milele zitagonga mwamba,” asema Mwangi.

Kuna minong’ono kwamba pendekezo hilo halikuwafurahisha baadhi ya washirika wa Rais Ruto kutoka Mlima Kenya na Magharibi wanaohisi kwamba litaua demokrasia na kurejesha Kenya katika enzi za utawala wa giza.

Hofu yao ni kwamba UDA inaweza kuchukua mkondo uliochukuliwa na Kanu miaka ya sabini na thamanini wa kubadilisha katiba kutimiza maslahi ya watu walio na ushawishi.

“Wanaongea kuhusu mambo mengo lakini, wakati akili zao zitatulia, watagundua wana kazi ya kufanya na kukomesha vitimbi vyao,” Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed alisema.

Mbunge mmoja wa Mlima Kenya anasema wanafuatilia kwa makini yanayojiri katika muungano tawala na akaongeza kuwa “hatutakubali yeyote kumpotosha rais wetu au kumfanya aonekane anataka kukwamilia mamlakani”.

  • Tags

You can share this post!

Mageuzi IEBC kuibua joto kati ya Ruto, Raila

Rais aonya wauzao mihadarati, aahidi minofu Pwani

T L