• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 12:33 PM
Vidosho Akorino walionengulia walevi viuno wawaka moto

Vidosho Akorino walionengulia walevi viuno wawaka moto

NA MWANGI MUIRURI

WAREMBO watatu wa dini ya Akorino walionaswa wakinengua viuno katika baa moja mjini Ruiru sasa wanawataka wadaku wa mitandao wakome kuwahukumu kwa kuwa mbinguni sio kwa mama ya yeyote, ni kwa wote.

Wakijitambulisha kama Mary, Ciru na Nyambura, wameteta kwamba kunao wanaoandika mitandaoni wanapaswa kuvuliwa vilemba vyao na vichomwe.

“Utuvue vilemba kwani wewe ndiye ulituvisha au tulikuvalia wewe? Vichomwe kwani umesikia vilemba vimeisha kwa soko? Si ni kwenda na kununua kingine cha Sh500 na nikivae tena?” akazusha Bi Nyambura.

Walisema kwamba hadi sasa wametambua walikosea kuitikia mwito wa kimwili na ushawishi wa anasa, ambapo walishiriki raha visivyo kwa mujibu wa kanuni za dini yao.

“Lakini hata wakati tumekubali makosa yetu, tunazidi kusutwa mitandaoni tukiambiwa etu kuna uwezekano tulikuwa walevi na tulikuwa tumepewa kazi na wasimamizi wa baa hiyo tutumbuize wateja wake wa ulevi. Hiyo ni porojo, tulikuwa tumehudhurie sherehe ya siku ya kuzaliwa ya mmoja wetu na tukaingia jukwaani na tukasakata ngoma,” akasema Bi Ciru.

Kwa pamoja, walisema kwamba bado wao ni wokovu, wanasafiri hadi mbinguni kukutana na Maulana mwenye nguvu zote “na iwapo wewe unaona hatutoshi mboga kujumuika kwa hiyo mbinguni kwa kuwa unahisi ni kwako, wewe enda tu ufunge lango ili tukifika tunyimwe nafasi ya kuingia”.

Watatu hao walijumuika pamoja na mwanaharakati wa kidini Bw Karangu wa Muraya pamoja na Essy wa Willy katika hafla hiyo ya kuomba msamaha na kutishia kuombea klabu hiyo ya Ruiru maangamizi ya mvua ya moto.

Aidha, watatu hao wamekuwa wakiandaliwa mahojiano na vituo kadha vya utangazaji na ambapo wameshikilia kuwa “licha ya kuomba msamaha, hatutakubali kushikwa mateka na wanaotushutumu na kutulinganisha na Ibilisi”.

Bw Muraya alisema kwamba “sisi wote ni watenda dhambi lakini neema za Mungu ndizo hutuweka huru na kutufungua minyororo ya maangamizi bora tu tutubu kwa kweli na tunyenyekee kiti cha enzi katika kuomba msamaha”.

Warembo hao wanashikilia kwamba walikuwa wanasaka utulivu wa nyoyo zao katika mazingira hasi ya ukosefu wa kazi na maisha kuwa magumu.

“Badala ya kukaa hapo ukiwazia kuhusu maneno ya kuturushia, tusaidie tupate kazi…Ukiona hatufai kusakata densi kwa baa tukiwa wokovu, basi tuite sehemu ambayo unaona tunafaa tusakate na utulipe,” akateta Bi Ciru.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Raila: Utawala wa kimikoa ufutiliwe mbali

Raila aonya siasa isiingiziwe usimamizi wa Mumias

T L