• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Viongozi wataka ‘Simba Wala Watu’ warudishwe nchini

Viongozi wataka ‘Simba Wala Watu’ warudishwe nchini

NA LUCY MKANYIKA

WAKAZI na viongozi wa Kaunti ya Taita Taveta wametoa wito wa kurejeshwa kwa mabaki ya Man-Eaters of Tsavo, simba mashuhuri walioua makumi ya wafanyikazi wa reli mnamo 1898, kutoka Amerika hadi Kenya.

Walisema kuwa simba hao ambao kwa sasa wanaonyeshwa katika Makavazi ya Field Museum of Natural History, Chicago, wanaweza kuwanufaisha wenyeji na kuwa chanzo cha mapato kaunti hiyo.

Wenyeji wengi wa kaunti hiyo, ambayo inakabiliwa na changamoto za migogoro ya binadamu na wanyamapori wanaotoroka mbuga ya Tsavo, wanaishi katika hali ya uchochole.

Simba hao waliuawa na Luteni Kanali John Henry Patterson, mhandisi Mwingereza aliyekuwa akisimamia ujenzi wa daraja la reli kwenye Mto Tsavo nchini Kenya, wakati huo ikiitwa British East Africa. Patterson aliandika kitabu kuhusu uzoefu wake, kinachoitwa The Man-Eaters of Tsavo, kilichochapishwa mwaka wa 1907.

Kitabu hiki baadaye kilibadilishwa kuwa filamu kadhaa, ya hivi karibuni zaidi ikiwa The Ghost and the Darkness (1996), iliyoigizwa na Val Kilmer na Michael Douglas.

Patterson aliuza ngozi na mafuvu ya simba kwa makavazi hayo mnamo 1924 kwa zaidi ya Sh760,000 (dola5,000).

Makavazi hayo yalitengeneza mabaki ya simba hao na kuyaweka kwenye maonyesho mwaka wa 1928. Tangu wakati huo wamekuwa mojawapo ya maonyesho maarufu zaidi katika makavazi, yakivutia mamilioni ya wageni kila mwaka.

Serikali ya Kenya imekuwa ikisukuma kurejeshwa kwa mabaki yao na sasa wakazi na viongozi wa kaunti ya Taita Taveta ilipo mbuga ya wanyama ya Tsavo, wamejiunga na wito huo.

Akizungumza huko Mwatate, Diwani Peter Shambi, alisema mabaki ya simba hao ni ya Kenya na yanapaswa kuonyeshwa katika makavazi ya humu nchini au hifadhi ya wanyamapori ili kupata mapato kwa serikali na wakazi wanaotaabika na umaskini.

“Serikali ya kitaifa na kaunti inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha ilhali mabaki ya simba wetu yanaleta mapato kwa serikali ya Amerika,” alisema.

Bw Shambi alisema serikali inafaa kuhakikisha inapata mapato kutoka kwa mabaki ya simba hao wawili ili wakazi wa kaunti hiyo wanufaike.

“Watalii wengine huja Tsavo kuona mahali tukio hilo lilitokea miaka mingi iliyopita. Ingekuwa bora tungekuwa na makavazi hapa,” alisema.

Diwani huyo alikuwa akizungumza wakati wa mkutano na Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Utalii na Wanyamapori, iliyozuru kaunti hiyo kusikiliza kero za wakazi katika maeneo yenye migogoro ya wanyamapori.

Kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Alfred Mutai, alisema bunge hilo linafanyia kazi sheria ambayo itafanya serikali kunufaika kulingana na mapato yanayotokana na mabaki ya simba hao wawili.

“Tunaunda sheria bungeni kuona jinsi tunarejesha mabaki ya simba wetu. Hiyo ni kweli,” alisema.

Kwa upande mwingine wakazi katika kaunti hiyo ambao wanakumbwa na visa vya mara kwa mara vya kushambuliwa na wanyamapori , walilalamikia kutonufaika na wanyamapori.

Wakazi wa maeneo ya Alia, Landi, Kiteghe na Bungule waliotembelewa na kamati hiyo, walieleza kusikitishwa kwao na tishio la wanyamapori linalowafanya waendelee kuwa maskini.

Kaunti hiyo ambayo inapakana na mbuga za wanyama za Tsavo Mashariki na Magharibi, imekuwa kitovu cha uvamizi wa wanyamapori hasa wa ndovu na simba ambao huharibu mazao na kuua mifugo.

Aidha, wabunge Peter Shake (Mwatate) na Abdi Chome (Voi), walisema kuwa fidia ya Sh51 milioni iliyotolewa na serikali mnamo Julai mwaka huu, haijafikia waathiriwa wengi.

Pia walilaumu Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini (KWS) kwa kutokabiliana na uvamizi huo kikamilifu.

“Hawasaidii hata kidogo, ndovu bado wanatutisha. Waliharibu mazao yangu yote. Vilevile, fidia haiji karibuni,” alisema mkazi wa eneo la Landi Damaris Mwachofi.

Wakazi hao pia walilalamikia kuwa hawanufaiki na rasilimali za wanyamapori ambayo ni chanzo cha matatizo yao.

Aidha, wabunge Peter Shake (Mwatate) na Abdi Chome (Voi) walisema kuwa fidia ya Sh51 milioni iliyotolewa na serikali mnamo Julai mwaka huu haijafikia waadhiriwa wengi.

Bw Chome aliitaka serikali kuwajibika katika kulinda wenyeji dhidi ya wanyama pori ili kulinda maisha na mali zao.
Alisema ipo haja ya kujengwa kwa ua ili kuzuia wanyamapori kuvamia makazi ya wenyeji.

“Hatusemi kuwa KWS haisaidii. Ni vyema kuweka mikakati ya kuongeza maafisa wanaolinda na kuzuia wanyamapori kufika kwa makaazi na mashambani. Wenyeji wamekuwa na kilio hiki kwa muda mrefu,” akasema.

Aidha, Bw Shake alisema ipo haja ya serikali kuona kuwa fidia inayotolewa inafaidi wenyeji wengi.

Alisema kuwa fidia iliyotolewa mbeleni ilikuwa tone huku watu wengi wakisalia wakidai haki zao.

“Hatujui ni kina nani walifaidi pesa hizi. Watu wengi wanasema hawajapata pesa hizo,” akasema Bw Shake.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi kutoka Kisii watetea Nyakang’o wakidai...

Mafuriko: Rigathi asuta magavana kulalamikia athari za El...

T L