• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
VITUKO: Pengo atua kijijini na kutumwa na kanisa jijini kuomba Famba msaada

VITUKO: Pengo atua kijijini na kutumwa na kanisa jijini kuomba Famba msaada

Na SAMUEL SHIUNDU

DUNIA rangi rangile.

Kama pangetokea mtu miaka michache iliyopita amwambie Pengo kuwa siku kama hii ingemkuta mahali kama hapa akihitaji msaada wa mtu kama huyu, mwalimu wa watu angebisha kwa kinywa kipana, na si kubisha tu, mwalimu angeapa kwa jina lake na kwa roho yake kuwa hakutaka kukutana na mtu huyu kabisa.

Enzi hizo, huyu mhisani wake mtarajiwa alikuwa mtu wa kuepukwa kama mgonjwa wa ukoma chambilecho wajuao tashbihi za uswahilini. Lakini sasa pesa na mamlaka yalikuwa yamemtengenezatengeneza akawa mtu wa kutamanika.

Mtu huyu hakuwa mwingine ila ndugu Famba.Shule zilipofungwa, Pengo alitua kijijini ili akaupumzishe mwili.

Lakini kama mwalimu huyu alidhani kuwa anakuja kupumzika na kuipunga hewa safi ya kijijini, basi alikuwa kakosea sana.

Alipotua tu, alijuzwa na waumini wake kuwa kanisa lao lilihitaji ukarabati.

“Tumejaribu kutuma maombi kwa wahisani kadhaa lakini hakuna hata mmoja miongoni mwao ambaye yu tayari kutufaa.Mmoja tu aliyesalia ni huyo ndugu Famba. Tumetuma watu kuongea naye akatwambia tumtumie ‘proposo’. Sisi hatujui kitu hicho alichokiita proposo. Tukaona tukusubiri utufae kwa mambo hayo mawili. Kwanza ututegulie hicho kitendawili cha proposo na pili uongee na huyo binamu yako kwa niaba yetu,” mwenyekiti wa wazee wa kanisa alimjuza.

Alipowafafanulia kuwa proposo ni pendekezo tu la kuomba msaada na kuwa kwa muktadha huo wao, ilikuwa tu sawa na barua rasmi ya kuomba msaada, wazee walimtwika jukumu la kuiandika barua hiyo na kusimamia mchakato mzima wa kuomba msaada kutoka kwa ndugu Famba.

Na ndiyo maana leo karauka kuja kujikunyata nje ya lango moja jijini akisubiri saa ifike akaonane na Bwana mkubwa.

Ombi la miadi lilikuwa limetumwa kwa bwana mkubwa wiki moja iliyopita.

Ombi likakubaliwa ila leo hii alipofika hapo langoni akakutana na utaratibu mwingine.

Alihitajika kutuma ombi la kuonana na bwana mkubwa.

Akatuma ombi kupitia kwa bawabu, ujumbe ukarejea kuwa bwana mkubwa alikuwa na habari kuhusu majilio ya mwalimu ila alikuwa angali kitandani.

“Waheshimiwa hawapendi kukatiziwa usingizi. Wanahitaji kulala ili waote mambo makubwa ya kuendeleza jamii,” bawabu alimfafanulia Pengo.

Kwa hivyo asubiri.

Aidha, Pengo alijuzwa kuwa si kawaida ya bwana huyo kuchelewea kitandani, lakini siku hiyo hawajui kilimjia nini.

“Labda ni kiburi tu cha kunifanya nisubiri hapa langoni ili nijue yeye ni nani,” Pengo aliwaza, ila kwa vile alihitaji msaada, basi hakuwa na budi ila kusubiri.

You can share this post!

USWAHILINI: Turathi ya Misitu ya Kaya na manufaa yake kwa...

TAHARIRI: Ukora katika kusajili wapigakura uzuiwe