• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
‘Wagathanwa’ aendelea kushambulia wakazi licha ya polisi kudai walishamtia mbaroni

‘Wagathanwa’ aendelea kushambulia wakazi licha ya polisi kudai walishamtia mbaroni

NA MWANGI MUIRURI

Vyombo vya kiusalama katika Kaunti ya Murang’a vimesutwa kwa kucheza sarakasi na suala la mvamizi ambaye amekuwa akishambulia wakazi na kuwaua akitumia shoka na kuwatishia moto wa petroli.

Mvamizi huyo amepewa jina la majazi la Wagathanwa, kutoka kwa jina Ithanwa ambalo kwa lugha asili ya eneo hilo humaanisha shoka.

Mvamizi huyo katika kipindi cha miezi minane sasa amevamia boma zaidi ya 20 na kuua watu wanne, kwa mujibu wa rekodi za polisi Murang’a.

Lakini cha kushangaza baadhi ya wananchi wa Murang’a ni jinsi maafisa wa usalama wamekuwa wakishughulikia hali hiyo, kwa sasa wakiwa washatangaza kukamatwa kwa washukiwa watano, lakini uvamizi huo bado ukiendelea.

Hali hii imezua maswali tele kutoka kwa wenyeji, mwenyekiti wa haki za kibinadamu katika Kaunti hiyo Bi Wangui Mbogo akitaka maafisa wa usalama wakome mzaha.

“Katika mahojiano yote yanayohusu uvamizi wa jambazi huyu ambaye hutembea akiwa amejihami kwa petroli na shoka, waathiriwa na mashahidi wamemwelezea kama mwanamume mnene, huongea Kiswahili na huvamia usiku wa manane haja yake ikiwa ni pesa na simu,” akasema Bi Mbogo.

Polisi kupitia Kamanda wa polisi Bw Mathiu Kainga mnamo Agosti 18, 2023 alijitokeza katika kikao na waandishi wa habari na akatangaza kukamatwa kwa mshukiwa huyo wa ujambazi.

“Ningetaka kutangazia watu wa Murang’a kwamba baada ya kazi ngumu ya kumsaka jambazi ambaye amekuwa akihangaisha wenyeji kwa kuwaua, kuwatisha kuwachoma moto na petroli na pia kuwagonga vichwa kwa kutumia shoka amenaswa,” akasema.

Hata hivyo, ilibainika kwamba aliyekamatwa hakuwa mvamizi aliyekuwa ameelezewa na waathiriwa na hata hakuwa na historia ya kuishi au kutembelea maeneo ambayo yalikuwa yameathirika na uvamizi huo.

Ni baada ya waathiriwa wengine kuvamiwa na wawili kuuawa katika hali iliyowiana na simulizi za awali za jambazi wa shoka na petroli ambapo maafisa wa polisi walizindua tena mikakati ya kumnasa mshukiwa mwingine.

Mnamo Agosti 31, 2023 kupitia mtandao rasmi wa Idara ya upelelezi wa jinai (DCI) serikali ilitangaza kukamatwa kwa mshukiwa mwingine wa kiume na wakamtambulisha kama aliyekuwa akihangaisha wakazi wa maeneo hayo ya Murang’a, wakiongeza kuwa shoka lililokuwa na makali ya kutisha lilikuwa limetwaliwa.

Wakichapisha hata picha ya mshukiwa huyo, polisi wa DCI walijigamba jinsi walisafiri hadi Kaunti ya Meru kumnasa mshukiwa huyo.

Kwa wakati mwingine tena, wenyeji wa Murang’a wakidhania kwamba kero hilo lilikuwa limezamishwa, watu wengine wawili waliuawa katika vijiji vya Kabuta na Muthigiriri, mashahidi wakisema aliyewavamia alikuwa amejihami kwa shoka na petroli.

Mnamo Desemba 6, 2023 Bw James Kamau alivamiwa na akauawa  na jambazi aliyeelezewa kama aliyejihami kwa shoka na petroli.

Bw Kamau alikuwa amemuuza mbuzi wake kwa Sh12,000 akipania kuzitumia kufadhili sherehe za Krisimasi lakini usiku wa manane akavamiwa na akauawa na mshukiwa aliyekuwa amejihami kwa shoka na petroli.

“Tunataka kutangaza kukamatwa kwa washukiwa watatu ambao wanakisiwa ndio walivamia na kumuua Bw Kamau nyumbani kwake katika Kijiji cha Kigoro na wakamwibia Sh12,000 na simu mbili,” taarifa ya polisi yasema.

Ripoti hiyo iliongeza kwamba kwa wakati huu mshukiwa halisi amekamatwa na ni mwanamume wa miaka 43.

“Pia, tumewakamata wengine wawili ambao wote ni wa miaka 28 na kwa sasa wamefungiwa katika kituo cha polisi cha Maragua wakingojea kufikishwa mahakamani,” ripoti hiyo yasema.

Bi Mbogo sasa anasema kwamba “ina maana kwamba jambazi mmoja ndiye anasakwa lakini polisi wameripoti kukamatwa kwa watu watano wote wakielezewa kuwa yule mshukiwa mmoja”.

  • Tags

You can share this post!

Muturi ajipata solemba mwaka mmoja baada ya kusaidia Kenya...

Mwanamume ahatarisha kunyongwa kwa kutumia simu ya kuokota

T L