• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
WAKILISHA: Avalia njuga ‘boy-child’

WAKILISHA: Avalia njuga ‘boy-child’

Na PAULINE ONGAJI

DUNIANI kote, vita vya kutetea haki za mtoto msichana vimeshika kasi katika jitihada za kuleta usawa wa kijinsia.

Lakini katika harakati hizi mtoto mvulana amekuwa akisahaulika, na hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya Kenton Muthaura kuingilia kati.

Bw Muthaura ni mwanzilishi wa Youths For The Boy-child, mradi wenye makao yake eneo la Meru, na ambao madhumuni ni kutetea haki za mtoto mvulana kuhakikisha kwamba anawakilishwa vilivyo hata ulimwengu unavyozidi kubadilika.

“Mradi huu unanuia kukabiliana na tatizo la uvivu miongoni mwa wavulana na wanaume ili kuwaandaa kuwajibika tayari kwa siku zijazo,” aeleza

Huu ukiwa mwaka wa pili tangu ung’oe nanga, umekuwa ukiendeshwa kwa vitengo vitano; Wezesha Boy Child Program, Mind-foot to Flee Program, Fathers-and-Sons Forums, Youths for the Boy Child Leaders Program na Me-for-the- Society Program.

Katika kitengo cha Wezesha Boy Child Program, watoto wavulana wanahudumiwa kwa kupata unasihi, huku wanaotoka katika familia maskini wakipata ufadhili.

Kenton Muthaura. Picha/ Hisani

Nao mradi wa Mind-foot to Flee Program unawasaidia wavulana, vijana na wanaume wanaotawaliwa na mihadarati kujinasua kutokana na zimwi hili.

“Hapa tuna huduma za wanasaikolojia na washauri nasaha kusaidia waathiriwa,” aeleza.

Kitengo cha tatu, Fathers-and-Sons Forums, kinasaidia wavulana wanaokuzwa katika familia ambapo baba anafanya kazi mbali au hayupo, kwa kuwapa fursa ya kupata upendo wa baba. “Hapa, shughuli hii hasa huandaliwa katika maeneo ya umma kama vile makanisa na shuleni ambapo tunaalika akina baba kuja kuzungumza na wavulana wasio na mzazi huyu kutokana na sababu moja au nyingine,” asema.

Kisha, kuna kitengo cha Youths for the Boy Child Leaders Program, kinachowapa wavulana walionufaika na mipango yetu ya awali mafunzo ya kuwa viongozi wa jamii.

“Mwishowe tuna mpango wa Me-for-the- Society Program, kinachowahimiza wavulana walionufaika na huduma zetu, kuungana nasi kusaidia kuimarisha jamii,” aeleza.

Ili kuthibitisha huduma za mradi huu, wanahusisha pia wanasihi na wataalamu wa kike.

“Tumefanya hivi kwa sababu tunaelewa kwamba wanaume huwafungukia wanawake kwa urahisi, vilevile kwa kawaida wanawake huonyesha mapenzi na hivyo wanaweza washughulikia vyema wale wanaotawaliwa na mihadarati,” aeleza .

Licha ya kuwa mradi huu umekuwepo kwa miaka miwili pekee, tayari mchango wake katika jamii unahisiwa.

“Tumekuwa tukitumia spoti kukuza vipaji vya vijana, na wakati huo huo shughuli tunazohusika nazo zimetoa nafasi za ajira kwa zaidi ya vijana 50,” asema.

Pia kupitia mpango huu, mradi wetu wa unasihi na ushauri umekuza vijana na kuwaongoza kuwajibika.

“Tumefanikiwa kutoa huduma za unasihi katika shule nane za msingi na upili tokea mwaka jana ambapo tulifikia zaidi ya wavulana 1,400,” aongeza.

Ari

Bw Muthaura anasema kwamba ari ya kuanzisha mradi huu ilitokana na kifo cha babake.

“Nilimpoteza babangu mwaka wa 2010, na hivyo kama mvulana wa kipekee kati ya watoto watano, niliachiwa majukumu ya kiume nyumbani mwetu,” asema.

Wakati huo, licha ya kuwa mwanafunzi wa shule ya upili, alikumbwa na jukumu la kushughulikia mahitaji ya familia yake kifedha.

“Wakati wa likizo, nililazimika kufanya vibarua kumsaidia mamangu kulipa karo, vilevile kushughulikia dada zangu,” asema.

Ni hapa ndipo aligundua kwamba kuna wavulana wengi waliokuwa wakipitia changamoto sawa na zake bila usaidizi na hivyo akakata kauli kulivalia njuga suala hili.

Kwa sasa wako katika harakati za kuteua wanasihi kuhudumia kila shule, katika harakati za kusaidia wavulana kuimarika kimasomo na hata kitabia.

You can share this post!

Kenya yaanza voliboli ya wanaume kwa kutwanga Uganda

HANG’OKI! Liverpool kurefusha mkataba wa Klopp

adminleo