• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wanafunzi wa Kabarak wahofia huenda kifo cha mwenzao mikononi mwa polisi kikafunikwa

Wanafunzi wa Kabarak wahofia huenda kifo cha mwenzao mikononi mwa polisi kikafunikwa

NA MERCY KOSKEI

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kabarak wanalilia haki baada ya mwanafunzi mwenzao kugongwa na gari la polisi alipokua anaelekea nyumbani.

Joshua Plimo, mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa somo la Famasia aligongwa na gari Jumamosi Novemba 18, 2023 nje ya lango la shule kabla ya gari hilo kutoroka.

Plimo alifariki saa chache alipokuwa akipokea matibabu katika kituo cha afya cha shule.

Kulingana na mwanafunzi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuhofia kuandamwa, alisema kuwa walikua pamoja wakisubiri kuvuka barabara wakati gari hilo lilimgonga.

Alisema kuwa gari hilo lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi,  lilikuwa linatoka Nakuru likielekea upande wa Mogotio, lakini baada ya kugonga matuta lilipoteza mwelekeo na kumgonga Plimo aliyekuwa amesimama kando ya barabara.

Mwanafunzi huyo aliomba msaada kutoka kwa waendesha bodaboda na walinda lango wa shule hilo. Alikimbizwa katika kituo cha afya cha shule.

Katika kituo cha afya, muuguzi huyo alidai uthibitisho kuonyesha kuwa alikuwa mwanafunzi katika taasisi hiyo kabla ya kumhudumia.

Hata hivyo, aliaga dunia huku madaktari na wauguzi wakijaribu kuokoa maisha yake.

“Tulikuwa tumeketi kwenye meza moja wakati wa chakula chetu cha jioni. Alikula ugali na omena nami nikala chapati na ndengu. Baada ya kumaliza, sote tulitoka na kuelekea nyumbani. Alikuwa na furaha wakati wote, hata alituhimiza tufanye haraka kabla lango la shule halijafungwa kwani sote tunaishi nje ya shule,” alikumbuka.

Mwanafunzi mwingine alisema walifanya maandamano Jumapili usiku na kulemaza usafiri katika barabara kuu ya Nakuru-Kabarnet kabla ya maafisa kutoka kituo cha Polisi cha Menengai kutumwa kutuliza hali.

Rais wa Shirika la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kabarak (KUSO) Karen Cheptoo, katika taarifa alikashifu kitendo hicho akisema kuwa wana wasiwasi mkubwa kuhusu maisha ya wanafunzi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Rongai Wilberforce Sicharani, alisema kuwa afisa huyo alitoka kwa kasi ili kuepuka kushambuliwa na wananchi na kuchoma gari hilo.

Kulingana naye askari huyo alitoa ripoti katika kituo cha Polisi cha Menengai na kukabidhi gari hilo ambalo linafanyiwa uchunguzi.

Alisema kuwa matokeo yatatolewa baada ya siku 14.

Kwa sasa wanasema wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kuongeza kuwa bado hawajaandikisha taarifa kutoka kwa wanafunzi na mashahidi.

“Mwili ulihamishwa hadi hospitali ya Nakuru Level five. Baada ya ukaguzi wa maiti, tutabaini kama kweli alikosea na hatua zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mradi wa magazeti shuleni ulivyoipa shule Eldoret...

Wanamitandao wahisi hadaa baada ya Sakaja kukutana na...

T L