• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
WANDERI KAMAU: Jamii imefeli ila ijikakamue kuelekeza watoto kimaadili

WANDERI KAMAU: Jamii imefeli ila ijikakamue kuelekeza watoto kimaadili

Na WANDERI KAMAU

KATIKA jamii, msingi wa kizazi cha baadaye huanza kuwekwa mara tu watoto wanapozaliwa. Msingi huo unaweza kuwa mbaya au mzuri.

Unaweza kuwa wa kukifaa kizazi hicho, kukielekeza ama kukipotosha. Msingi ambao kizazi husika hulelewa nao huja kujitokeza katika siku za usoni, hasa kwenye ukubwa wacho. Ni katika kiwango hiki ambapo maadili mema, sawa na maadili mabaya hudhihirika.

Vile vile, ni kwenye ukubwani ambapo mbivu na mbichi huonekana.Natoa urejeleo huu kufuatia ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi, hasa kwenye shule za upili, ambavyo vimeshuhudiwa kwa majuma mawili sasa baada yao kurejea shuleni.

Visa ambavyo vimeripotiwa kwa majuma hayo ni vya kusikitisha. Ni matukio ya kuatua moyo, kuhusu ikiwa yanafanywa na wanafunzi au watu razini waliogeuka kuwa wahalifu.

Katika siku za hapo nyuma, ilikuwa nadra kusikia kisa kuhusu mwanafunzi anayemshambulia mwalimu au mlinzi hadi akamuua. Visa vya wanafunzi kuwavamia wazazi wao vilikuwa matukio ambayo hayangesikika hata kidogo.

Hata hivyo, hali imebadilika.Sababu kuu ni kuwa vizazi vya wanafunzi wa hapo awali viliongozwa na maadili. Vilizingatia miiko na miongozo ya kijamii. Vilifahamu kuhusu umuhimu wa kuwaheshimu wakubwa wao. Vilielewa kwa undani athari za kutozingatia miongozo vilivyopewa na walezi wao.

Miongoni mwa athari hizo ni laana ambazo ziliaminika kutoka kwa “miungu.”Kimsingi, lengo kuu la tahadhari hizo lilikuwa kujenga uwepo wa kizazi ambacho kingeifaa jamii baadaye.

Lengo lake pia lilikuwa kuwajenga watu ambao wangeweza kupitisha maadili hayo kwa watoto, wajukuu, vitukuu na hata vilembwekeza wao.

Matokeo ya ulezi huo mzuri ulikuwa ni uwepo wa mashujaa waliopigania uhuru wa kwanza na wa pili, wasomi maarufu, wanamichezo wa kuheshimika, waalimu waadilifu, madaktari wasio wabinafsi kati ya wanataaluma wengine wenye utu na ubinadamu.

Enzi hizo, shule zilikuwa jukwaa nzuri lililoheshimika na kila mmoja kwani kando na wanafunzi kufaidika kimasomo, zilitoa mazingira mwafaka ya kimalezi kwa wanafunzi na jamii nzima.

Wazazi walikuwa huru kumwadhibu mtoto yeyote waliyempata akikosea. Chini ya mwelekeo huo, watoto kwenye vijiji waliwaheshimu wakubwa wao kwani waliwachukulia kama wazazi waliowalea.Hata hivyo, hali ni tofauti sasa. Badala ya mahali pa hekima na maadili, shule zimegeuka kuwa ngome za maafa, umwagikaji damu na utovu wa nidhamu.

Badala ya wanafunzi kuwa kioo chema cha maadili kwa wadogo wao, wamegeuka kuwa mifano ya kuogopwa kutokana na nyendo zisizofaa. Wanaogopwa na kila mmoja katika jamii.

Wakubwa kwa wadogo na vijana kwa wazee. Hawajali wala hawabali. Hawaambiliki wala hawasemezeki. Wamejifanya ‘wajuaji’; ‘wajuaji’ wasiojua watokako wala waelekeako.Kwa mkasa huu, nawalaumu wazazi, walimu na jamii ya sasa. Nawalaumu kwa kutoweka msingi ufaao kwa wanao.

Nawalaumu kwa kuwapa uhuru ambao sisi hatukupewa.Nawalaumu kwa kutowadhihirishia kuwa njia ya maisha si rahisi. Ni ndefu na yenye kujitolea kwingi. Ili kuokoa jahazi na kizazi chetu, ni wakati turejelee kanuni za awali kuhusu ulezi mwema.

[email protected]

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Museveni amesaidia Uganda licha ya utawala...

Nairobi kunoma, asimulia rapa Majirani