• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:10 AM
Yeye hugeuza uchafu kuwa sanaa inayolipa

Yeye hugeuza uchafu kuwa sanaa inayolipa

NA LABAAN SHABAAN

KELVIN Kilonzo, 28, hakufaulu kuendeleza kisomo chake zaidi ya kiwango cha shule ya upili.

Katika kusaka njia ya kujikimu kiuchumi, alikumbuka talanta yake ya tangu utotoni ya uchoraji na stadi ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kutokana vitu vikuukuu na taka.

Baada ya kunoa makali ya kipaji kupitia kuhudhuria warsha kadhaa, Kilonzo alianza kuunda vesi za maua na vitu vingine vya kurembesha nyumba, afisi na mazingira tofauti.

“Sanaa yangu hutumia taka kuunda bidhaa bora za kutumika tena kutumia taulo, karatasi, vibonzo, tambla, blanketi, vijiti, kauri kutaja tu baadhi,” Kilonzo anaambia Akilimali.

Kijana huyu ambaye pia amesomea udereva anasema kuwa alivutiwa kuchangamkia kazi za sanaa na baba yake ambaye alikuwa sonara na mchoraji.

“Nilijifunza kazi hii kutoka kwa baba yangu. Kipaji hiki kilinifanya maarufu shuleni kwa sababu nilikuwa nawachorea wanafunzi picha tofauti na pia hata walimu walinihitaji kuchora katika shughuli za masomo na kufunza wengine,” Kilonzo anasema.

Juhudi ya kuokoa uchafuzi wa mazingira iko katika mapigo ya moyo ya Kilonzo kwa sababu anakusanya taka kutoka kwa majaa kutengeneza bidhaa za kurembesha mazingira.

Miongoni mwa vitu anavyounda ni vesi, maua bandia, kadi za kheri, mabango ya kutani, herini, vipuli, mazulia, bendi ya nywele, vishikio vya kalamu, shashi na kadhalika. Kilonzo huunda vitu hivi kwa mikono yake pasi na utumizi wa mashini.

“Nyumba yangu ndiyo karakana yangu hapa mjini Machakos. Sina sehemu ya biashara kwa sasa lakini hali ya uchumi ilivyo biashara inafaa kuendeshwa nyumbani na kutumia mitandao ya kijamii kujiuza,” Kilonzo anaeleza.

“Kwa wiki naunda wastani ya bidhaa tano na kuuza kwa wakazi wa Machakos. Wakati mwingine nawatumia wateja vitu nilivyounda hadi kaunti tofauti kwa ada ndogo,” anaongeza.

Kwa mujibu wa sonara huyu, kuunda kitu kimoja humgharibu angalau Sh200 na bei ya kuuza ni zaidi ya maradufu ya gharama ya malighafi.

“Aghalabu mimi hufikia wateja kupitia mitandao ya kijamii. Pia huwahusisha marafiki wapakie kazi zangu mitandaoni na kunipigia debe. Kama si hivi mimi huhudhuria maonyesho ya kibiashara na talanta kutangaza kazi hii,” Kilonzo anaarifu.

Msanii huyu anakiri kuwa kazi hii pia ina changamoto zake hasa kuhusiana na gharama licha ya vitu vikuukuu kupatikana katika mazingira.

Vesi au vishikilio vya maua na mabango ya kutani yanayotengenezwa na sonara Kelvin Kilonzo Machakos. PICHA | LABAAN SHABAAN

Anasema kuwa kutengeneza kitu kipya wakati mwingine humhitaji kugharamika zaidi kwa kununua gluu na nyenzo zingine.

Ili kujiimarisha kibiashara na kiujuzi, Kilonzo yuko mbioni kutafuta mikopo na ruzuku ili kuanza karakana yake mwenyewe ambapo atapanua wigo wa biashara.

Anaamini siku moja kipaji chake kitabadilisha maisha yake na ya familia huku akiapa kufunza wengine ujuzi huu na kubuni nafasi za ajira kwa Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Mkutano ulituletea ushindi, adai Kane

Wengi wanufaika na mafunzo kutoka kwa shirika la Engage...

T L