• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
ZARAA: Mfumo bora kuendeleza uzalishaji chakula mijini

ZARAA: Mfumo bora kuendeleza uzalishaji chakula mijini

NA SAMMY WAWERU

MWEZI uliopita, Januari na huu wa Februari, kiangazi na ukame vyote vimeonyesha makali yake huku zaidi ya kaunti 20 zikitegemea chakula cha msaada.

Taswira inayoshuhudiwa kutoka maeneo kame (Asal), kamwe si ya kuridhisha Kenya ikiwa miongoni mwa mataifa katika Upembe wa Afrika yaliyolemewa na makali ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa miaka mitatu mfululizo, hali imekuwa iyo hiyo mwaka huu ukianza kuonekana kuwa mbaya zaidi kwa sababu ya baa la njaa.

Mifumo ya teknolojia kuendeleza kilimo inapigiwa upatu kuchangia uzalishaji wa chakula.

Mbali na maeneo ya mashambani kuwa kapu la mazao, miji inalengwa pia kupitia mabustani.

Zipo mbinu ainati kugeuza mabustani hayo kuwa uga wa kilimo cha kisasa mojawapo ikiwa matumizi ya shamba garden units. Ni mfumo wa paipu za plastiki zilizounganishwa, na kupandwa mseto wa mboga, viungo vya mapishi na matunda. Zile tajika zikiwa vertical gardens.

Wilson Njuguna mwasisi wa Lavington Herbs amevumbua muundo ulioboreshwa. Kampuni yake inashughulika na uzalishaji wa miche ya matundaasilia, viungo, na vifaa tamba vya kisasa kuendeleza kilimo mijini.

Akitambua muundo aliovumbua kama semi-permanent tower garden, anasema nafasi mbadala ya shamba inayohitajika ni kidogo, matumizi ya maji yakiwa yamedhibitiwa na rahisi kukabiliana na wadudu na magonjwa.

“Isitoshe, muundo huu mpya mkulima anavuna kiwango cha mazao anayohitaji kula au kuuza. Hivyo basi, unapunguza utupaji na uharibifu wa chakula,” Njuguna adokeza.

Mfumo huo aidha unawafaa wakazi wa mijini, vifaa hivyo vikiwekwa kwenye kuta, kando kando ya njia za magari na kwenye maegesho.

Kando na kuwa bora kukuza mseto wa mboga, Njuguna ambaye pia ni mkulima anasema ni faafu kulima matunda kama vile matikitimaji, stroberi na karakara.

Hali kadhalika, nyanya, vitunguu, biringanya, dania na pilipili mboga.

Ikiwa imeundwa kwa paipu aina ya PVC, semi-permanent tower garden huunganishwa kwa nyaya kusaidia kusitiri mimea inayotambaa kuelekea juu.

Mvumbuzi huyo anasema miundo yake inapatikana kwa saizi ndogo; yenye urefu wa futi 4.5, ya kadri 5 na kubwa 7, yote ikiwa na upana wa futi 1 mraba sakafuni.

 

Wilson Njuguna, mwanzilishi Lavington Herbs, akionyesha mseto wa mboga na viungo vya mapishi vilivyopandwa kwenye semi-permanent tower garden. PICHA | SAMMY WAWERU

Kulingana na Njuguna, ndogo inakuzwa kati ya mimea 15 – 18, kadri 24 na kubwa 30.

“Ni mfumo unaodhibiti matumizi ya maji kwa kiwango kikuu. Mfano, muundo mmoja unaweza kutumia lita moja kwa siku badala ya 20 mimea iliyopandwa eneo tambarare shambani,” aelezea, akitaja mboleaasilia, ya mifugo, pumice (unga unaotokana na mawe ya Volkeno) na udongo, kama kipandio baada ya kuchanganya vyema.

Kwenye bustani, vifaa hivyo vinawekwa umbali wa futi moja.

Joash Njani, mtaalamu wa masuala ya kilimo anataja mifumo ya aina hiyo kama mbinu bora zaidi kujumuisha maeneo ya miji kuchangia uzalishaji chakula.

“Mabadiliko ya tabianchi ambayo yamechangia janga la ukame, yametufunza tugeuze miji kuwa kijani. Mifumo ya mabustani ya plastiki ni kati ya mbinu tunazopaswa kukumbatia kuongeza kiwango cha chakula nchini,” mdau huyo ashauri.

Hali kadhalika, teknolojia hiyo inasaidia kwa kiasi kikuu kugeuza miji kuwa kijaani, yaani greening the cities kwa Kiingereza.

  • Tags

You can share this post!

Waliojenga madarasa ya CBC wasaka malipo miezi saba...

MAZINGIRA: Mchango wa kilimo-bustani katika kuimarisha...

T L