• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 7:50 AM
MAZINGIRA: Mchango wa kilimo-bustani katika kuimarisha tabianchi

MAZINGIRA: Mchango wa kilimo-bustani katika kuimarisha tabianchi

NA PAULINE ONGAJI

VIONGOZI wa kimataifa na wataalam wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi walipokusanyika kwenye kongamano la 2022 la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, al-maarufu COP 27, Novemba 2022, kwa upande mwingine kuna baadhi ya vijana ambao tayari walikuwa wanafanya mambo yao madogo madogo ili kukabiliana na janga hili.

Mmoja wao ni Caroline Mukuhi Mwangi, mwanzilishi wa Kimplanter Seedlings and Nurseries Ltd, kampuni iliyoko eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, na ambayo imekuwa ikijihusisha na shughuli za kilimo cha bustani, vile vile upanzi na uzalishaji wa miche ya matunda.

Caroline alikuwa miongoni mwa washiriki kumi bora wa shindano la YouthAdapt lililowatuza vijana hapa barani ambao miradi au uvumbuzi wao ulikuwa na mchango katika kuimarisha tabianchi. Washindi hawa walipokea ufadhili wa kifedha ili kuendeleza miradi yao.

Carolyne Mwangi, mwanzilishi wa kampuni ya Kimplanter Seedlings and Nurseries akionyesha tuzo anavyokuza aina mbalimbali za miche ya mboga na matunda. PICHA | LUCY WANJIRU

Kabla ya hapa, alikuwa ametambuliwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwenye maonyesho ya kimataifa ya kilimo mwaka wa 2019, na pia kutawazwa kama balozi wa kilimo wa vijana wa Kaunti ya Kiambu.

Kwa sasa, Mukuhi anamiliki nyumba mbili za vioo (za kuhifadhi mimea) eneo la Ruiru na tisa eneo la Makuyu, huku akizalisha miche ya mboga na matunda na kuwauzia wakulima katika sehemu mbali mbali nchini.

Kampuni hii inasambaza miche katika sehemu mbali mbali nchini.

“Kwa kawaida sisi husambaza bidhaa hizi katika maeneo ya Mombasa, Lodwar, Kisumu lakini hasa wateja wetu wengi ni kutoka eneo la Kati. Miongoni mwa mimea tunayozalisha ni kabichi, sukumawiki, nyanya, koliflawa, brokoli, paipai, karakara na miche ya nyanya miongoni mwa mingine.”

Kulingana na Caroline, wateja wake ni wa aina mbili.

“Kuna wale wanaoingia madukani mwetu na kununua aina moja ya miche. Kisha kuna wale ambao tayari wana miche na mbegu zao ila tu wanahitaji wasaidiwe kuzizalisha.”

Kwa kawaida, uzalishaji wa miche ni shughuli inayohitaji uangalifu ambapo mkulima asipotilia maanani, huenda asipate matokeo mazuri. Na hivyo, kwa kufanya hivi, Bi Mukuhi asema kwamba wanaokoa muda wa wakulima na kazi ngumu inayohitajika katika shughuli hizi za uzalishaji.

“Endapo mkulima ataamua kujifanyia kazi hii basi atakumbwa na changamoto nyingi ambazo zitaathiri ubora wa mimea yake,” aeleza.

Anasema kwamba kwa kawaida ili kuzalisha miche yao wao hutumia mbegu mpya kutoka kampuni za mbegu zinazojulikana na kutambulika.

“Sisi pia hutumia mbinu maalum ya uzalishaji inayoitwa coco peat ambayo inakubalika na aina mbalimbali za udongo, na ndiposa uwezekano wa miche yetu kukua ni asilimia 95.”

Kulingana na Caroline, kwa kawaida, miche hiyo huzalishwa kwenye sinia za plastiki ili kuhakikisha ulinganifu.

“Na hivyo kila mche unakua katika kiwango kimoja.”

Alipojitosa alianzisha shughuli yake kwenye kipande cha ardhi cha robo ekari eneo la Ruiru, alichokuwa ameazimwa na rafikiye.

Penzi lake liliimarika zaidi aliponza kuchapisha picha za bidhaa zake kwenye ukurasa wake wa Facebook, suala lilimomfanya kunasa macho ya wengi.

“Kutokana na sababu kuwa nilikuwa mwanamke tena barubaru, wengi walionekana kuvutiwa na penzi langu kwa kilimo.”

Haikuwa muda kabla ya jitihada zake kuanza kunasa macho ya vyombo vya habari.

“Mwaka huo huo nilihojiwa na stesheni mbili za televisheni ambapo kazi yangu ya kilimo iliangaziwa.”

Anaendelea kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu kilimo cha miche na kutazama kampuni yake ikiendelea kukua.

“Mwanzoni niliwaelekeza kwa mkulima aliyekuwa akiniuzia, lakini tatizo ni kwamba hakuwepo. Kwa hivyo kukawa na pengo kwenye soko la miche ya pesheni na mboga, suala lililonisukuma kuanza kupanda bidhaa hizi.”

Haya yalijiri huku naye akijipiga msasa kwa kupokea mafunzo zaidi kuhusu kilimo cha miche.

Lakini hata alipokuwa akiendelea kufanya hivi, mahitaji ya miche hiyo yalikuwa mengi hasa baada ya kuanza kupokea simu kutoka kwa kampuni za kuunda juisi.

“Changamoto ingine ilikuwa kwamba shamba langu lilikuwa dogo sana kutimiza mahitaji hayo.”

Kufikia hapa ilikuwa Juni 2016 na huku mahitaji yakiendelea kuongezeka, alifanya hesabu zake na kugundua kwamba angepata mapatao mengi kutokana na mauzo ya miche, ikilinganishwa na mshahara wake.

Papo hapo, aliamua kuacha kazi na kujitosa kikamilifu katika kilimo.

Lakini haikuwa rahisi kuacha kazi ambayo ilikuwa ikimpa mshahara na kujitosa katika ulingo ambao haukuwa na uhakika wa mapato.

“Pia, mwanzoni babangu alishindwa kuelewa ni vipi niliamua kuacha ajira ilhali nilikuwa nimehitimu na Cpa-K na hata kabla ya kutumia ujuzi ambao nilikuwa nimepokea, nilikuwa nang’atuka.”

Aidha, Bi Mukuhi asema alihitajika kuwashawishi marafiki zake ambao walishindwa kuelewa uamuzi wake.

“Hii ilinifanya niachane na baadhi yao.”

Hata hivyo, kwa bahati nzuri kunao waliomuelewa huku mamake akishabikia uamuzi wake, suala lililompa moyo zaidi.

Kwa sasa anaendelea kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu kilimo cha miche na kutazama kampuni yake ikiendelea kukua.

Makala haya yamechapishwa kama sehemu ya ushirika wa uanahabari wa Mabadiliko ya Tabianchi, mafunzo ya uanahabari yaliyoandaliwa na Internews Earth Network na The Starnley Center for Peace and Security

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Mfumo bora kuendeleza uzalishaji chakula mijini

MITAMBO: Hiki hapa kipima ubora wa kahawa

T L