• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
ZARAA: Teknolojia ndio itaokoa kilimo nchini, afisa asema

ZARAA: Teknolojia ndio itaokoa kilimo nchini, afisa asema

NA SAMMY WAWERU

MARY Nzomo ni Waziri wa Kilimo, Mifugo, Samaki na Vyama vya Ushirika Kaunti ya Trans Nzoia na alizungumza na Akilimali kuhusu mianya tele iliyoko wakulima wakikumbatia teknolojia na mifumo ya kisasa, hususan kwa vijana.

SWALI: Baadhi ya mashirika hasa yasiyo ya kiserikali (NGO) yanayopiga jeki shughuli za kilimo nchini, yamekuwa yakihimiza wakulima kukumbatia teknolojia na mifumo ya kisasa. Kama mmoja wa maafisa wanaoshikilia sekta ya kilimo, unahisi hatua hiyo ni mojawapo kuiboresha?

JIBU: Ninaungama, teknolojia za kisasa kuendeleza kilimo ndio msingi kukuza sekta hii yenye mchango mkubwa kwa uchumi. Kuna mifumo chungu nzima, na tukiikumbatia itakuza kilimo na ufugaji. Kenya haijatekeleza vilivyo matumizi ya teknolojia na bunifu katika kilimo.

SWALI: Tunapotaja nyenzo hizo, tunamaanisha nini?

JIBU: Kwanza, ni teknolojia za kisasa kuboresha mazao, kama vile; mifereji ya kunyunyizia mimea na mashamba maji. Mfumo huo unaenda sambamba na kuwepo kwa visima, vidimbwi na mabwawa kuvuna maji. Hivyo basi, ni muhimu serikali kuu na zile za kitaifa, zitengee mgao wa kutosha sekta ya kilimo. Mifumo mingine, ni matumizi ya mashine na mitambo na Bayoteknolojia. Pili, karibu kila mmoja ana simu ya kisasa (smartphone) na ni chombo muhimu kusaidia kuboresha kilimo. Apu za kutoa ushauri bora kitaalamu, kuunganisha wakulima na masoko, pembejeo na mahitaji mengine zimezinduliwa na baadhi ya kampuni za kibinafsi na asasi za serikali kama vile Kalro. Isitoshe, matumizi ya teknolojia yanapunguza gharama ya uzalishaji na pia hasara zinazoibuka baada ya mavuno.

SWALI: Hamasisho kuhusu shughuli za kilimo zinaendeshwa kisasa, ni tija zipi zinatokana na hatua hiyo?

JIBU: Dhana kuwa kilimo kinapaswa kuendeshwa na waliostaafu, waliofikisha umri wa miaka 60 inaturejesha nyuma. Hatutaki sekta ya kilimo isheheni wazee, tunataka vijana wawekeze. Vijana wana ari, nguvu na hawaogopi changamoto ibuka. Si lazima wawe shambani na majembe. Mtandao wa kilimo ni mpana, kuanzia utoaji wa ushauri kitaalamu (wataalamu wa kilimo), usafirishaji wa bidhaa, kuzitafutia soko na kuziongeza thamani. Kimsingi, nafasi za ajira ni tele katika utandawazi wa kilimo.

SWALI: Umetaja umuhimu wa vijana kushiriki shughuli mbalimbali za kilimo, lakini wengi wanalalamikia ukosefu wa fedha (mtaji). Kwa mtazamo wako, suala hili litatatuliwa vipi?

JIBU: Hakika mtaji ni mojawapo ya vikwazo vinavyowazuia kuingilia kilimo kikamilifu. Kibarua ni kwa serikali kuu na zile za kaunti kuongeza mgao kwa sekta ya kilimo, na hilo litasaidia kuwapiga jeki. Ni muhimu pia kuweka wazi serikali ina mipango mbalimbali inayolenga vijana, hususan programu za utoaji mikopo ya riba ya chini. Kilimo kinaweza kuendelezwa kitaalamu. Mfano, ufufuzi wa Mpango wa 4 – K Club katika shule zote za umma nchini, unalenga kukuza wanafunzi katika kilimo. Hao ndio vijana na viongozi wa kesho, watakaoshikilia sekta. Baadhi ya mashirika yameibuka na miradi kutuza vijana wanaoshiriki kilimobiashara, na wamekumbatia teknolojia na bunifu. Heifer International, ni mojawapo, na kupitia mpango wa AYuTe, Africa Challenge awards, na Digital Agriculture Champions and Tractors 4 Africa Project, ni mashindano kuwatia motisha ambapo watakaoibuka bora watazawadiwa na kupigwa jeki.

SWALI: Ni changamoto gani teknolojia na mifumo ya kisasa itatatua?

JIBU: Kwa muda mrefu, wakulima wamekosa fursa ya ushauri nasaha na kuendeleza kilimo kitaalamu, wanaopata huduma hizo ni ghali. Teknolojia zitasaidia huduma hizo kuwafikia na kwa bei nafuu, kila mmoja akimiliki simu ya kisasa. Ni kupitia hilo, gharama ya uzalishaji itashuka, taifa liwe na chakula kingi na cha kutosha. Hatutaendelea kuwa mateka kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.

SWALI: Trans Nzoia inategemea kilimo cha nafaka pekee haswa mahindi na maharagwe. Athari za tabianchi zinaendelea kusambaratisha ratiba ya hali ya hewa. Wakazi watazidi kutegemea mazao hayo pekee?

JIBU: Kama kaunti, tumezindua mikakati kuhimiza wenyeji kukuza mimea mbadala, kama vile ndizi zilizoimarishwa (tissue culture), macadamia, na avokado za Hass. Vilevile, tunawahamasisha kuingilia ufugaji wa kuku wa mayai na ng’ombe wa maziwa, badala ya kutegemea mahindi na maharagwe pekee.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Raila sasa akimbilia mahakama

MITAMBO: Bailers za kisasa zinazotumia GPS

T L