• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
ZARAA: Ukuzaji wa matunda wazima ‘ushawishi’ wa zao la mahindi

ZARAA: Ukuzaji wa matunda wazima ‘ushawishi’ wa zao la mahindi

NA JOHN NJOROGE

BAADA ya kutembea hatua chache kutoka kwa barabara kuu ya Molo kwenda Njoro karibu na mji wa Elburgon katika Kaunti ya Nakuru, tunaelekea kwa Charles Ngaruiya, ambaye ni mkulima mdogo na kumpata akiwa ndani ya shamba lake la matundadamu au tree tomato.

Ngaruiya alikuwa akiyavuna matunda huku akiandamana na mkewe.

“Kwa Sh3,500 nilizokuwa nazo mfukoni, nilitayarisha sehemu yangu ya upanzi, nikanunua miche, nikaajiri wafanyakazi wa kawaida na kupanda miche 70 kwenye sehemu hiyo mnamo Machi, 2021. Niliacha nafasi ya futi tano kutoka kwa mche moja hadi mwingine kwa vile nafasi hii iliniwezesha kupanda vyakula kwa mseto vilivyo na naitrojeni kama vile maharagwe ambayo pia huwezesha treetomato kukua vizuri na kwa hali nzuri,” akasema Ngaruiya, na kuongeza kuwa alichimba kila shimo kwa kina cha futi tatu.

Akiongea na Akilimali, Ngaruiya alisema kuwa alitoa udongo wa juu kutoka kwa kila shimo na kuuchanganya na samadi ya shamba (mbolea) kwa muda wa mwezi mmoja.

Kulingana na mkulima huyu, mchanganyiko huo huwa na joto ambalo husaidia kwa kuua wadudu wanaojificha ndani ya mchanga.

Baada ya muda huo wa mwezi mmoja, miche huwa tayari kupandwa iwapo mkulima ana maji ya kutosha.

Kwa upande wake, Ngaruiya hutumia maji ya mfereji ama kuteka kutoka kwa mto ulio karibu na shamba lake.

Baada ya muda wa miezi mitatu au minne, mkulima huyu alinyunyizia dawa ya kuua magugu na wadudu kabla ya kukata ncha ya treetomato ilipofika futi nne ili kuzuia kuinama kutokana na urefu wake. Matawi yakidhibitiwa kwa njia inayofaa, mkulima huvuna matunda mengi.

“Ikinenepa kuliko kimo chake, mazao huwa duni ikilinganishwa na ile imekua kwa urefu wa wastani ambapo matawi huwa mengi na mazao kuongezeka,” akasema, na kuongeza kuwa baada ya miezi sita, matundadamu huhitaji kunyunyiziwa dawa zaidi ifikapo wakati wa kutoa maua.

Charles Ngaruiya akikagua matundadamu aliyopanda katika shamba lake mjini Elburgon, Nakuru. PICHA | JOHN NJOROGE

Baada ya mwaka mmoja, wakulima huvuna mavuno ya msimu wa kwanza iwapo mvua ilikuwa ya kutosha na mmea kutunzwa vizuri.

Mkulima huyu alisema kuwa siri kubwa ya kunawiri ni kutumia njia inayofaa wakati wa upanzi, kunyunyizia mazao yake maji ya kutosha, kutumia mbolea ya wanyama na pia kutumia mbolea ya nitrogeni (CAN) ili kuongeza mavuno.

Anapanga kuongeza sehemu ya ardhi na kupanda zaidi ya miche 400, akisema ukulima wa matunda una faida kubwa isiyokuwa na madalali ikilinganishwa na mazao mengine kama mahindi.

“Kazi nyingi hufanyika wakati mkulima anapanda mahindi hasa kwa kutumia fedha nyingi wakati wa kukodisha shamba, kununua mbegu na mbolea ambayo bei yake imeongezeka zaidi ya matarajio ya mkulima. Madalali pia ni changamoto kubwa inayokumba wakulima wa mahindi katika sehemu hii,” akasema.

Ngaruiya huuza mazao yake Nakuru mjini kwa Sh60 kwa kilo. Licha ya matunda kuwa mojawapo ya mazao ya muda mrefu, mtumiaji huyatumia kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kupogoa ama kufanya mzunguko wa mazao.

Yeye huvuna matunda yake baada ya juma moja kulingana na hali ya anga.

Wakati wa baridi ama mvua, huyavuna matunda yake baada ya majuma mawili. Anasema kuwa upungufu wa maji na kuvamiwa na fuko ni baadhi ya changamoto mkulima wa tree tomato hupitia.

Kwa upande wake, hutumia mtego au chambo cha sumu kuwaua fuko hao.

Anakiri kuwa wakulima katika sehemu hii wanaendelea kujitenga na ukulima wa mahindi na kukuza matunda kwa njia kubwa kama vile parachichi, machungwa baadhi ya nyinginezo.

Katika siku zijazo, anasema sehemu hii itakuwa imetambulikwa kwa ukulima wa matunda kwa kuwa wengi wametilia maanani ukulima huo.

Afisa wa kilimo katika kaunti ndogo ya Molo, Emma Mwangi amewaomba wakulima kununua miche kwa wahusika waliosajiliwa ili kupata mazao yanayofaa kama vile Kephis.

“Magonjwa mengine kama vile bakteria hujificha ndani ya mchanga, ndio maana tunawashauri wakulima kupima mchanga kabla ya kupanda mimea kwa ili kuongeza virutubisho na kuyafanya mazao kunawiri na kutoa mapato mazuri,” akasema Bi Mwangi.

Aliwasihi pia kuhudhuria semina na maonyesho ya kilimo mara kwa mara ili kupata maarifa na ujuzi zaidi ua ukulima na pia teknololja mpia za ukulima bora.

([email protected])

  • Tags

You can share this post!

Atalanta yapiga AC Milan breki kali ligini

UJASIRIAMALI: Kilimo Msitu kinavyohifadhi mazingira na...

T L