• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
UJASIRIAMALI: Kilimo Msitu kinavyohifadhi mazingira na kuwaletea riziki

UJASIRIAMALI: Kilimo Msitu kinavyohifadhi mazingira na kuwaletea riziki

NA LABAAN SHABAAN

JULIUS Waweru, mtaalamu wa kilimo, ni mkulima wa miche ya miti eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a na huuza miche 20, 000 kwa mwaka mche mmoja ukigharimu Sh150.

Mwanaagronomia huyu anasema ili uanze kitalu cha miche ya miti huna budi kumudu angalau Sh200,000 na miaka mitatu hadi mitano ya kazi kustawisha kijishamba.

Hata hivyo, gharama ya kukita kitalu itategemea vigezo kama vile umiliki wa shamba na ukubwa, aina ya miti, ufikiaji wa maji safi na gharama ya kazi shambani miongoni mwa vipengele vingine.

Julius Waweru akiwa katika kitalu chake cha miche katika Kaunti ya Murang’a. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Kilimo mseto wa miti, mimea na mifugo maarufu agroforestry hutoa kivuli kwa mimea na wanyama pamoja na kudhibiti hali ya joto shambani. Miti ya matunda ni chakula kwa binadamu na mingine ni chakula kwa wanyama,” Waweru anaarifu.

“Wateja wetu ni wenye nia ya kuwekeza katika biashara ya matunda, bustani nyumbani na mashirika kununua miti ya vivuli katika kipindi cha kukabili mabadiliko ya tabianchi na kukumbatia kilimo kinachokwenda sambamba na hali ya anga maarufu Climate Smart Agriculture,” anaongeza.

Kupitia Kampuni ya Ukulima Modern Seedlings and Agro-based Consultancy, Waweru huuza miche na kuhamasisha wakulima kuhusu umuhimu wa kupanda miti shambani na pia kujihusisha na kilimo cha miche ya miti.

“Biashara hii ina faida na kinachotia moyo zaidi ni kuwa inasaidia kuhifadhi mazingira na kukabili mabadiliko ya hali ya hewa. Ukulima ni utamaduni mzuri na unafaa kukumbatiwa na kila mtu,” anadokeza akitabasamu.

Mkulima mwingine anayekumbatia kilimo msitu ni Kennedy Ngoma anayepanda miti ya kiasili, ya matunda na mimea mingine pamoja na kufuga kuku na ng’ombe katika shamba moja Kaunti ya Nakuru.

Kilimo hiki kinaendelezwa na kuhamasishwa na Shirika la Usimamizi Shirikishi wa Ardhi ya Kiikolojia (PELUM).

Shirika hili kwa ushirikiano na lile la ViAgroforestry kutoka Uswidi linahimiza makumi ya maelfu ya wakulima wadogo katika maeneo kame na nusu kame kama vile Kajiado, Siaya, Bungoma, Samburu, Laikipia na Nyeri kugeuza maeneo kame kuzalisha mazao kwa kuhusisha miti shambani.

Wakulima katika mpango huu wamepanda miti ya kiasili na ya kisasa zaidi ya 500, 000 ili kusaidia kudhibiti naitrojeni katika udongo.

“Wakulima wengi wanaonizingira wana miti shambani mwao ambayo wanaweza kutumia kama kuni hivyo kupunguza uwezekano wa kuingilia misitu,” Ngoma anaambia Akilimali.

Shadrack Obura hupanda miche na miti ya mianzi, grevillea, ciala, Senna Siamea na mingine katika shamba lake Suna Mashariki Kaunti ya Migori.

“Nilianza upanzi huu ili kudhibiti mmomonyoko wa udongo na kuongeza rutuba katika shamba la baba yangu,” Obura anasema.

Shadrack Obura katika shamba la mipapai na vitalu vya miche Migori. PICHA | LABAAN SHABAAN

Mkulima huyu wa mtama, ndizi, mahindi na mimea mingine huuza miche 70,000 kila mwaka kwa wakulima wengine, shuleni, makundi ya maendeleo ya jamii na Kaunti ya Migori katika juhudi za upandaji miti.

Mche mmoja wa mwanzi hununuliwa kwa Sh250 mingine ikiuzwa katika ya Sh 5 na Sh 20.

Wataalamu wanasema kilimo mseto hufanya shamba kuvutia, kupunguza athari ya kasi ya upepo, chanzo cha mbolea mbali na kuwa kitega uchumi.

Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kilimo mseto, usimamizi wa ardhi na maji ni miongoni mwa mikakati muhimu itakayopunguza ufukaji wa gesi chafu hewani.

Licha ya kuwa na umuhimu pia kuna changamoto ya ukuzaji wa miti sambamba na mimea na mifugo.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa kilimo hiki huchukua muda kuleta faida, huwa na kazi nyingi, ufinyu wa masoko na ukosefu wa maarifa miongoni mwa wakulima.

Pia kuna ushindani wa virutubisho shambani na miti huvutia vimelea zaidi ambao huweza kuathiri mimea na kuongeza gharama ya kuwadhibiti.

You can share this post!

ZARAA: Ukuzaji wa matunda wazima ‘ushawishi’ wa zao la...

MITAMBO: Hii ‘honey press’ itakukamulia asali...

T L