• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 9:59 AM
BENSON MATHEKA: Serikali izingatie utumizi bora wa hela hata inaposambaza chakula cha msaada

BENSON MATHEKA: Serikali izingatie utumizi bora wa hela hata inaposambaza chakula cha msaada

NA BENSON MATHEKA

MWISHONI mwa juma lililopita, Rais William Ruto na mawaziri wake walikuwa maeneo tofauti kuongoza shughuli ya kugawa chakula cha msaada kwa Wakenya walioathiriwa na njaa.

Serikali ilitaka kuonyesha kwamba inawajali raia na pengine kuzima mishale ya lawama ambayo upinzani ulikuwa umejiandaa kurusha.

Huenda mkakati wa Rais Ruto ulifaulu kwa kuwa tuliona makundi ya wazee na wanawake waliodhoofika kwa njaa inayosababishwa na ukame wakifurahia kupata nyama, mchele na maharagwe kuwafaa angalau kwa siku kadhaa.

Hata hivyo, kinachoweza kuponza juhudi hizi ni gharama ambayo mawaziri na viongozi wengine wanatumia kuzuru maeneo tofauti kwa shughuli ambayo inaweza kuongozwa na maafisa wa vyeo vya chini katika maeneo husika.

Kila ziara ambayo kiongozi wa nchi anaifanya eneo fulani humu nchini, huwa inagharimu pesa ambazo zinaweza kulisha wakazi wa tarafa kwa wiki kadha.

Hii ni kwa sababu kuna mahitaji ya kimsingi kama usalama ambayo huwa yanagharimu pesa. Hali huwa sawa anakotembea Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri Mshirikishi Musalia Mudavadi na mawaziri ambao huwa wanaandamana na maafisa kadhaa wa wizara na idara husika.

Japo ni muhimu kwa Rais na maafisa wakuu wa serikali kuongoza kwa vitendo ikizingatiwa kuwa baadhi ya raia wamekuwa wakihisi serikali inawapuuza, hatua zote za kupunguza gharama zinafaa kutiliwa maanani.

Hakuna haja ya kukusanya Sh40 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo kusaidia Wakenya na chakula na kisha Sh20 bilioni zitumiwe kwa shughuli za usimamizi.

Hivyo basi, maafisa wa serikali wanafaa kupunguza gharama ya kugawa chakula cha msaada ili pesa zinazotengwa na kukusanywa ziweze kufaidi kikamilifu Wakenya 4.5 milioni walioathiriwa na baa la njaa.

  • Tags

You can share this post!

JIJUE DADA: Kinachosababisha ngozi inayozingira macho kuwa...

Mradi wa nyumba wa Buxton kuingia awamu ya pili

T L