• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 8:50 AM
CHARLES WASONGA: Serikali iwachukulie hatua kali walimu wakuu wanaonyanyasa wazazi

CHARLES WASONGA: Serikali iwachukulie hatua kali walimu wakuu wanaonyanyasa wazazi

NA CHARLES WASONGA

INAUDHI kuwa licha ya serikali kuonya walimu wakuu wa shule za umma za msingi na upili dhidi ya kutoza wazazi ada za ziada, onyo hilo limepuuzwa.

Alipokuwa akipigwa msasa na Bunge kubaini ufaafu wake kama Waziri wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu, aliahidi kuzima uovu huo.

Aliambia Bunge kwamba walimu wakuu watakaokaidia agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Lakini kuanzia mwaka 2022 hadi sasa, wakuu wa shule za umma wamekuwa wakitoza wazazi ada ya ziada kando na karo zilizoidhinishwa na serikali.

Kwa mfano, shule zilipofunguliwa Januari 23 wazazi wa watoto katika shule za upili walipigwa butwaa kuitishwa ada ya ziada.

Baadhi ya shule zinatoza hadi Sh6,000 kila muhula “kuwatia motisha” walimu kwa mafunzo ya ziada baada ya saa rasmi za kazi.

Hii ni licha ya masomo ya ziada kupigwa marufuku katika shule zote nchini, kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya Msingi, 2013.

Isitoshe, licha ya Waziri Machogu na mwenzake wa Biashara, Bw Moses Kuria, kuzima mwenendo wa walimu wakuu kuuzia wazazi sare shuleni au kuwaagiza waende duka fulani, wazazi wangali wanashurutishwa.

Kwa mfano, kuna baadhi ya shule ambazo zinauza seti moja ya sare mpya ya wanafunzi wa Gredi 7 kwa Sh7,000.

Katika enzi hizi za mfumo wa biashara huru, wazazi wanaweza kupata sare hizo kutoka kwa wauzaji wengine kwa bei nafuu zaidi kuliko wanayolazimishiwa.

Naomba Waziri wa Elimu na wa Biashara kutuma wakaguzi wapelelezi katika shule zote za umma ili waandame walimu wakuu wanaokaidi agizo lao, badala yake wanaendelea kunyanyasa wazazi ambao tayari wanazongwa na hali ngumu ya uchumi.

Ikiwa serikali itachelea kuchukua hatua dhidi ya walimu wakuu kama hawa, basi itachukuliwa kwamba wakuu serikalini pia hufaidi kutokana na unyanyasaji huo wa wazazi.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ibada zisigeuzwe jukwaa la kutupiana cheche...

Biden akataa kutuma ndege za kivita nchini Ukraine

T L