• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
CECIL ODONGO: Kuongoza katika kura ya maoni si kushinda kura

CECIL ODONGO: Kuongoza katika kura ya maoni si kushinda kura

NA CECIL ODONGO

ZIKIWA zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, kampuni mbalimbali za utafiti zimekuwa zikitoa matokeo ya kura za maoni kuhusu wagombeaji wa urais na wale wa viti mbalimbali vya uongozi.

Mnamo Jumatatu, kampuni ya utafiti ya Tifa ilitoa matokeo ambayo yaliwaweka Raila Odinga na Naibu Rais, Dkt William Ruto sako kwa bako katika kinyang’anyiro cha urais.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Bw Odinga anayewania kwa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, alikuwa kifua mbele kwa asilimia 42 za kura huku Ruto wa Kenya Kwanza akiwa na asilimia 39, naye Prof George Wajackoyah akiwa na asilimia nne pekee.

Tangu amteue kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua kama mgombea-mwenza wake, Bw Odinga amekuwa akiongoza kwenye kura nyingi za maoni ikilinganishwa na Dkt Ruto ambaye alimpa Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua nafasi hiyo.

Hata hivyo, kuna imani hatari inayojengeka miongoni mwa wafuasi wa Bw Odinga kuwa kinara wao tayari ameshinda urais kwa kuongoza katika kura za maoni.

Mwanzo, wafuasi hawa wamekuwa wakidai Bw Odinga sasa anashirikiana na Rais Uhuru Kenyatta na huenda akasaidiwa na nguvu na mikakati ya watu walio karibu na serikali maarufu kama deep state kushinda urais.

Msingi wa imani hiyo ni madai au dhana kuwa Bw Odinga amekuwa akishinda urais kwenye chaguzi za 2007, 2013 na 2017 lakini hupokonywa ushindi kutokana na hila ya watu walioko serikalini wanaoshirikiana na Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Kulingana nao, sasa kinara wao anashirikiana na serikali na ‘atasaidiwa’ kushinda urais.

Pili, wengi wa wafuasi wa Bw Odinga wanadai kuwa kumteua Bi Karua kama mwaniaji-mwenza kutapunguza umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya na huenda wawaniaji hao wawili wakuu wakagawana kura za eneo hilo nusu bin nusu.

Hii ni licha ya utafiti wa Tifa uliotolewa Jumatatu na za kampuni nyingine kuonyesha kuwa Dkt Ruto bado ana ufuasi katika kaunti zinazojumuisha Mlima Kenya.

Tatu, wafuasi wengi wa Bw Odinga wanadai hata wapige kura au wasipige bado mgombeaji wao atashinda urais, wakifarijiwa na dhana kuwa Dkt Ruto hashabikiwi na viongozi serikalini na hakuna jinsi wanavyoweza kumruhusu ashinde urais.

Ukweli ni kuwa Bw Odinga atakuwa na kibarua kigumu kumbwaga Dkt Ruto iwapo fikira kama hizi zitaendelea kukolea ndani ya nyoyo za wafuasi wake.

Urais unapatikana kutokana na idadi ya juu ya kura ambapo mwaniaji wake hupata.

Kwa hivyo, wafuasi wa Bw Odinga wanafaa wafahamu kuwa ni kujitokeza kwao kwa wingi ndiko kutakakomwezesha kutwaa uongozi wa nchi.

Iwapo watajitokeza kwa zaidi ya asilimia 90 katika ngome zake na kupiga kura kwa makini, basi watakuwa wamemsaidia Bw Odinga sana kutimiza ndoto yake badala ya kuzubaa.

msawiri kama mwanasiasa ambaye atasaidiwa na vyombo vya utawala.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013, wengi wa wafuasi wa Bw Odinga wakati huo walikuwa na imani angembwaga Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto ambao wakati huo walikuwa wakikabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Wakati huo, Bw Odinga aliongoza kwenye matokeo mengi ya kura za maoni lakini baadaye alibwagwa uchaguzini.

Si mara ya kwanza, kigogo huyo wa siasa za upinzani anaongoza kwenye kura ya maoni ndiposa wafuasi wake hawafai kuwa na imani ya zaidi ya asilimia 100 kuwa atakuwa Urais kwa kuwekwa kifua mbele na utafiti wa Tifa.

Pia matokeo ya kura za maoni yanaonyesha kuwa karibu asilimia 30 bado hawajaamua mwaniaji ambaye watampigia kura.

Hata hivyo, kuna uwezekano kuwa wafuasi wa Bw Odinga ndio wengi kwenye kundi hili kwa kuwa ndio wamekuwa wakidai hawana haja ya kupiga kura kwa sababu mgombeaji wao amekuwa akiibiwa kura katika kila uchaguzi aliyewania.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: IEBC iwe makini zaidi inapojiandaa kwa uchaguzi

CHARLES WASONGA: Vyama vya UDA na ODM vilikosea kutunuku...

T L