• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:50 AM
TAHARIRI: IEBC iwe makini zaidi inapojiandaa kwa uchaguzi

TAHARIRI: IEBC iwe makini zaidi inapojiandaa kwa uchaguzi

NA MHARIRI

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), inafaa kuwa makini zaidi kuanzia sasa inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wawaniaji kadhaa wana hofu kuwa IEBC haijafafanua masuala muhimu ya uchaguzi kama vile mfumo wa kuwatambua wapigakura, uchapishaji wa karatasi za kupigia kura, ripoti ya ukaguzi wa sajili ya wapiga kura, mfumo wa upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi katika maeneo yasiyo na mawimbi ya 3G au 4G, miongoni mwa masuala mengine.

Ni hivi majuzi ambapo Bw Chebukati aliwashangaza wagombeaji na Wakenya alipoongoza makamishna na maafisa wa tume yake kupokea karatasi za kupigia kura katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kabla ya majina ya wagombeaji kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali.

Si hayo tu, makamishna wa IEBC waliwaambia wanahabari kwamba walipata ujumbe kuhusu kuwasilishwa kwa karatasi hizo kutoka kwa kampuni ya Ugiriki, Inform Lykos, mnamo Jumatano usiku. Aidha, wagombeaji hawakufahamu kwamba uchapishaji wa karatasi hizo ulikuwa unaendelea kwa msingi kuwa majina yao hayajachapishwa rasmi.

Ni kinyume cha kanuni nambari 52 ya Sheria ya Uchaguzi, 2016 kwa shughuli ya uchapishaji wa karatasi za kura kuanza kabla ya majina ya wagombeaji kuchapishwa.

Kauli hii, kwa mtazamo wangu, inaashiria kuwa huenda mtu yeyote akawasilisha kesi mahakamani kuharamisha jumla ya karatasi 132,722,748 ambazo ziliwasili nchini Alhamisi wiki jana.

Hii ni licha ya kwamba chapisho la gazeti rasmi la serikali lenye majina 16,608 ya wagombeaji lilitolewa Jumapili, Julai 10. Pili, zaidi ya mwezi mmoja baada ya IEBC kupokea ripoti ya ukaguzi wa sajili ya wapigakura kutoka kwa kampuni ya KPMG, Bw Chebukati hajaisambaza kwa wadau katika uchaguzi wa mwaka huu.

Hii ni licha ya kwamba kambi za Azimio na Kenya Kwanza ziliiandikia tume hiyo barua zikiitisha nakala za ripoti hiyo ili ziweze kuichambua.

Mbali na KPMG kuondoa majina ya wapigakura 246,465 wafu, wengine 481,711 walibainika kujisajili zaidi ya mara moja huku wengine 226, 143 wakijisajili kwa kutumia vitambulisho visivyo vyao.

Mbali na wafu ambao majina yao yaliondolewa katika sajili ya wapigakura, IEBC haijaeleza hatima ya watu ambao walijisajili zaidi ya mara moja au kutumia stakabadhi zisizo zao.

Chebukati pia hajatoa ufafanuzi kuhusu madai ya mgombea urais wa chama cha UDA kwamba karibu majina ya wapigakura wapatao milioni moja, ambao ni wafuasi wake, yaliondolewa katika sajili ya wapiga kura.

You can share this post!

Silva asihi Neymar ahamie Chelsea

CECIL ODONGO: Kuongoza katika kura ya maoni si kushinda kura

T L