• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
CECIL ODONGO: Mudavadi ataingia ikulu rahisi kupitia kwa Raila

CECIL ODONGO: Mudavadi ataingia ikulu rahisi kupitia kwa Raila

Na CECIL ODONGO

MSIMU wa kampeni kali za kisiasa umewadia huku viongozi mbalimbali wa kisiasa wakimezea viti mbalimbali. Kinara wa ANC Musalia Mudavadi amesema mara si moja kwamba, wakati huu atawania urais hadi mwisho. Hii ni licha ya takwimu kuonyesha kwamba, kwa sasa kinyang’anyiro ni kati ya Naibu Rais na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Ukweli ni kwamba, njia rahisi ya Mudavadi kukaribia lango la Ikulu iwe ni mwaka ujao au 2027 ni kupitia ushirikiano wake na Kinara wa ODM Raila Odinga.Viongozi hao wawili wamekuwa wakilumbana vikali, Bw Mudavadi akionekana kuwa na uhasama zaidi dhidi ya Bw Odinga kutokana na hatua ya waziri huyo mkuu wa zamani kutangaza kuwa atakuwa debeni ilhali inaaminika aliahidi kuunga mmoja wa waliokuwa vinara wa Nasa waliomvumisha 2017.

Wiki hii, Bw Mudavadi alionekana kulegeza kamba kidogo wakati wa hafla ya mazishi ya mamake wa kambo eneobunge la Sabatia, hafla ambayo ilihudhuriwa na Bw Odinga pamoja na wanasiasa wa ANC na wale wa ODM.Bw Mudavadi ambaye yupo katika mrengo wa One Kenya Alliance alisema tofauti kati yake na Bw Odinga ni za kisiasa wala hazifai kuvuruga urafiki wa karibu kati ya familia zao.

Kauli na mapokezi aliyotoa Bw Mudavadi kwa Bw Odinga, ni tofauti na hali ilivyokuwa siku za nyuma ambapo amekuwa akimkashifu waziri huyo mkuu wa zamani vikali katika hafla mbalimbali.Akiwa kwenye ziara, magharibi na viongozi wenzake wa OKA mwezi uliopita, Bw Mudavadi alinukuliwa akisema hatashurutishwa kumuunga mkono kiongozi yeyote bali atakuwa debeni liwalo na liwe.

Kauli hii ilionekana kumlenga Bw Odinga, kutokana na kuenea kwa madai kuwa Rais Uhuru Kenyatta anampigia debe amrithi kwa kuwashawishi vinara wa OKA wafute azma yao.Aidha, Bw Mudavadi alionekana kukerwa na uwepo wa Bw Odinga kwenye hafla ya uzinduzi wa azma ya kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka mwezi uliopita.

Kando na kumsalimu Bw Odinga shingo upande, Bw Mudavadi alikosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa azma ya Bw Odinga mapema mwezi huu katika uwanja wa MISC Kasarani, akisema alikuwa na majukumu ya kibinafsi.Ingawa hivyo, kauli yake kuwa tofauti zao hazijavunja urafiki wao inaweza kufasiriwa kuwa ameanza kuchangamkia kambi ya Bw Odinga licha ya msimamo mkali wa baadhi ya wanasiasa wa ANC wakiongozwa na Cleophas Malala (Seneta wa Kakamega) na mbunge wa Lugari Ayub Savula.

Yamkini Bw Mudavadi ametambua kuwa ni afadhali kujiunga na mrengo wa Bw Odinga kuliko ule wa Naibu Rais Dkt William Ruto. ambako hakuna nafasi ya miungano.Kwa kuwa si rahisi kuondoa kiongozi anayelenga kipindi cha pili uongozini, ni kama kwamba Bw Mudavadi ameona ni heri ajiunge na mrengo wa Bw Odinga, ambaye duru zinaarifu huenda akaongoza kwa muhula mmoja kutokana na umri wake mkubwa kisha kuachia wanasiasa wengine.

Vilevile, matokeo kwenye chaguzi za 2007 na 2017 zinaonyesha wawili hao wakishirikiana basi ni rahisi kura za Magharibi na Nyanza kuelekezwa kwenye kapu moja.Na hata Bw Odinga asiposhinda na wawili hao washirikiane, ni rahisi sana amtaje Bw Mudavadi kama mwaniaji wa Urais 2022 kuliko wawaniaji wengine watakaojitokeza.

You can share this post!

Kisura azua fujo kwa kalameni akidai Sh5,000 zamshusha bei

Kizaazaa EFL Cup leo soka ikisonga mbele

T L