• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
CECIL ODONGO: Mwelekeo anaochukua Rais Ruto mwishowe utamponza mwenyewe

CECIL ODONGO: Mwelekeo anaochukua Rais Ruto mwishowe utamponza mwenyewe

MATUKIO yanayoendelea kisiasa nchini sio mazuri kwa utangamano wa taifa.

Mnamo Jumapili, nilisikiliza hotuba ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga akizungumza na halaiki ya raia.

Kilicho dhahiri ni kuwa, mara hii Waziri Mkuu huyo wa zamani huenda asilegeze kamba kuendeleza maasi dhidi ya serikali.

Bw Odinga akihutubia maelfu ya wafuasi wake mtaani Kibera, Nairobi, aliweka wazi masuala matatu ambayo ukiyapekua kwa kina yanaonyesha kuwa ameamua kupambana na utawala wa Kenya Kwanza vilivyo.

Kinara huyo alikariri kwa mara nyingine kuwa hatambui utawala wa Rais William Ruto na kuutaka ufunganye virago, akidai kuwa alipokonywa ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Pili, alimuonya Rais Ruto kuwa utawala wake usihangaishe familia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusiana na utata unaoendelea wa ulipaji ushuru.

Baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza wamedai kuwa kampuni za familia ya Mzee Jomo Kenyatta hazijakuwa zikilipa ushuru.

Rais Ruto mwenyewe alinukuliwa kule Mombasa akidai kuwa, mikutano ya upinzani inafadhiliwa na watu wasiotaka kulipia mali yao ushuru.

Tatu, Bw Odinga alikariri kwamba haogopi kukamatwa wala hajali iwapo serikali ina mpango huo.

Baada ya kumaliza msururu wa mikutano ya kushinikiza utawala wa Ruto uondoke, duru zinaarifu kuwa kinara huyo sasa atachukua hutua za kuendeleza maasi dhidi ya serikali kupitia ‘matendo’.

Iwapo kauli alizotoa Bw Odinga ni za kuaminika, basi serikali ya Kenya Kwanza itakuwa na kibarua kutimiza ajenda yake katika mazingira ya uhasama wa kisiasa.

Mwanzo, Bw Odinga si mwanasiasa wa kupuuzwa; kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, anaungwa mkono na nusu ya wapigakura nchini.

Maasi anayoendeleza huenda yakashika kasi hasa wakati huu ambapo Wakenya wamelemewa na ugumu wa maisha.

Raila ana historia ya kupigania mageuzi; sifa iliyokolea katika familia yao, ambayo ilianza na babake Jaramogi Oginga Odinga.

Jaramogi alipigania uhuru kabla mwanawe Raila kujiunga naye kupinga utawala dhalimu wa Kanu na kuleta mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.Ni dhahiri kuwa haogopi kukamatwa.

Aidha, amejenga imani ndani ya wafuasi wake kwamba ndiye alishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Yote tisa, iwapo serikali itamtia ndani, huenda wingu la maandamano na maasi likazidi.

Tawala zilizopita zimezuia makabiliano naye na kumpuuza.

Rais Ruto aache kukabiliana na Bw Odinga kwani hilo linapandisha joto la kisiasa nchini.

Aidha hatua ya Raila kuitaka serikali isihangaishe familia ya Kenyatta ina maana kuwa sasa amechukua vita hivyo kama vyake binafsi.

Hii inazua kumbukumbu ya jinsi alivyowazima baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya ambao walitaka kulipiza kisasi dhidi ya Rais Mstaafu marehemu Daniel Arap Moi baada ya utawala wa Narc kuingia mamlakani mnamo 2003.

Kuna haja ya Rais Ruto, Raila na hata viongozi wote kulegeza kamba kwenye msimamo wao mkali la sivyo itakuwa ni cheche kali na maandamano kwa miaka mingine mitano.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Nyong’o adai Jalang’o na wenzake 8...

Jopo lashauri Ruto amtimue Jaji Chitembwe

T L