• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
CECIL ODONGO: Wanasiasa waasi waende tu, ODM ni kubwa kuliko yeyote

CECIL ODONGO: Wanasiasa waasi waende tu, ODM ni kubwa kuliko yeyote

NA CECIL ODONGO

SENETA wa kwanza wa Homa Bay marehemu Otieno Kajwang’ aliwahi kutoa kauli maarufu, aliposema kuwa iwapo uaminifu wa yeyote kwa chama cha ODM unashukiwa, basi mtu huyo hawezi kuruhusiwa kushikilia uongozi wa chama.

Bw Kajwang’ alikuwa mfuasi sugu wa chama na kati ya wandani waaminifu wa kinara wa chungwa Bw Raila Odinga.

Alitoa kauli hiyo kuelekea uchaguzi wa kitaifa wa ODM mnamo 2014, ambapo kulikuwa na mirengo tofauti iliyokuwa iking’ang’ania uongozi wa chama.

Kajwang’ alikuwa mrengo wa Dkt Agnes Zani, ambaye alikuwa akiwania kiti cha katibu wa ODM.

Naye alitaka kuwa naibu mwenyekiti wa chama huku Bw Paul Otuoma akisaka uenyekiti.

Mrengo mwingine ulikuwa ukiongozwa na Ababu Namwamba, ambaye alikuwa akimezea mate wadhifa wa katibu mkuu na Josephat Nanok (mwenyekiti).

Bw Kajwang wakati huo alisisitiza kuwa, watu wa mrengo wa Namwamba walikuwa fuko wa Jubilee ndani ya ODM.

Akashikilia kwamba kamwe hangewaruhusu wachukue uongozi wa chama.

Mwishowe uchaguzi wa ODM ulivurugika na haukufanyika kutokana na rabsha zilizozuka katika ukumbi wa Kasarani.

Aidha, kauli ya Kajwang’ ilitimia kwani baadhi ya viongozi kama Bw Namwamba waliishia kujiunga na serikali wakati huo.

Nimerejelea kisa hiki kutokana na misukosuko ambayo imeanza kuonekana ndani ya chungwa.

Mwenyekiti Bw John Mbadi wiki jana alisema hana tatizo kuacha uongozi wa chama, wadhifa ambao ameshikilia miaka tisa.

Bw Mbadi alidai kuwa amechoka kulaumiwa na baadhi ya viongozi wa ODM kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita.

Isitoshe, aliweka bayana kuwa ana njia nyinginezo za kuwasilisha malalamishi dhidi ya serikali badala ya kujiunga na wanasiasa katika msururu wa mikutano inayoandaliwa na mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya nchini.

Mwanzo, huyu si Bw Mbadi ambaye alifahamika kama mfuasi kindakindaki wa ODM na jemedari wa Raila Odinga.

Kutokana na kauli zake, ni wazi roho haipo tena ODM. Vyema chama kimpe mwingine nafasi hiyo.

ODM haistahili kuongozwa na mtu vuguvugu mwenye machungu na kisasi cha kisiasa.

Bw Mbadi alianza kuasi ODM Gavana Gladys Wanga alipopewa tikiti ya moja kwa moja ya kuwania kiti hicho mwaka 2022.

Pia hana raha Mbunge wa Ugunja, Bw Opiyo Wandayi, kuwa Kiongozi wa Wachache Bungeni.

Badala ya majivuno na kujitapa eti hawezi kuhudhuria mikutano ya maasi na halipwi mshahara kama mwenyekiti, ajitoe ODM kwa upole. Madai yake kuwa hakuna mtu anaweza kushikilia nafasi hiyo, ni hadaa tupu kwani Babu Owino ashajitokeza na kuitaka.

  • Tags

You can share this post!

‘Afrika bado ingali nyuma katika utoaji wa chanjo...

Mchungaji Ezekiel Odero amlipia mwanafunzi Sera Kauchi karo...

T L