• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
CHARLES WASONGA: Matamshi ya Ruto, Raila yasivuruge mazungumzo

CHARLES WASONGA: Matamshi ya Ruto, Raila yasivuruge mazungumzo

NA CHARLES WASONGA

NI unafiki mkubwa kwa Rais William Ruto na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kukutana Mombasa na kukubaliana kuhusu haja ya mirengo yao kushiriki mazungumzo kisha wanaanza kuweka masharti makali kuhusu mchakato huo.

Mnamo Jumamosi Julai 29, 2023 iliripotiwa kuwa Rais Ruto na Bw Odinga walikutana katika mkahawa mmoja jijini Mombasa pamoja na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

Duru zilisema kuwa watatu hao waliafikia kuwa kamati ya watu 10; watano kutoka mrengo wa Kenya Kwanza na watano kutoka Azimio la Umoja-One Kenya ibuniwe kujadili masuala yaliyochangia upinzani kuitisha maandamano tangu Machi mwaka huu.

Duru zilisema kuwa Bw Obasanjo, ambaye alihudumu kama Rais wa Nigeria kuanzia 1999 hadi 2007, aliteuliwa na jamii ya kimataifa kupatanisha pande hizi mbili za kisiasa nchini.

Hii ni baada ya mabalozi wa mataifa ya kigeni kujitokeza na kulaani maandamano ya Azimio kwa kusababisha maafa na uharibifu wa mali ya umma na ya kibinafsi yenye thamani kubwa mno.

Fujo zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano hayo pia zilichafua mazingira ya kisiasa nchini na kuogofya wawekezaji kando na kuhatarisha masilahi ya mataifa mengi ya kigeni, yakiongozwa na Amerika.

Kwa hivyo, inavunja moyo kwamba hata kabla ya mazungumzo hayo kuanza, Rais Ruto ameanzisha kampeni kali ya kukashifu mchakato huo akiunasibisha na juhudi za upinzani kupigaji ugavi wa mamlaka, almaarufu handisheki.

Akiongea na wananchi katika ziara yake ya eneo la Mlima Kenya wiki jana, Dkt Ruto alisisitiza kuwa hatakubali handisheki yoyote kwani alishinda katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa njia halali.

Naibu Rais Rigathi Gachagua na wabunge Kimani Ichung’wa na Ndindi Nyoro waliendeleza msimamo huo huo wakipuuzilia mbali mchakato huo wa mazungumzo.

Sasa swali langu ni je, nini haswa kilimsukuma Rais Ruto kukutana na Bw Odinga mjini Mombasa kujadili suala hilo ikiwa yeye na wandani wake hawataki mazungumzo?

Mbona alikubali kwamba Mzee Obasanjo awe mpatanishi katika mchakato huo ikiwa wandani wake kama vile Nyoro hawathamini kibarua cha kiongozi huyo?

Nadhani Rais Ruto aliamua kuzuru eneo la Mlima Kenya ili kutuliza joto la kisiasa baada ya wanasiasa wa eneo hilo kukerwa na uamuzi wake wa kukutana na Bw Odinga mjini.

Nakumbuka kuwa siku chache kabla ya Rais kukutana na kiongozi huyo wa upinzani, wandani wa Bw Gachagua wakiongozwa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga walisisitiza kuwa endapo mkutano huo utafanyika basi sharti Naibu huyo wa Rais awepo.

Kwa kweli ikiwa Rais Ruto ni mtu muungwana jinsi anavyojisifu, kile angetumia kwenye ziara hiyo ya Mlima Kenya ni kuelezea viongozi na wakazi kuhusu sababu zilizochangia yeye kukutana na Bw Odinga bila kumwalika Bw Gachagua.

Kwa upande wake, Bw Odinga hafai kutoa makataa ya siku 30 kwa Rais Ruto kuhakikisha kuwa mazungumzo yamekamilishwa na makubaliano kufikiwa.

Ikiwa kweli Bw Odinga anajali kuhusu masilahi ya Wakenya wanaozongwa na makali ya kupanda kwa gharama ya maisha, basi akome kabisa kutoa makataa hata kabla ya mazungumzo kuanza.

  • Tags

You can share this post!

Hii ni kwa wanaonyonyesha na inawabidi kuenda kazini

Mwanamume anayedaiwa kuwaua kwa kuwachinja wanawe akamatwa

T L