• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
CHARLES WASONGA: Mawaziri watekeleze agizo la Rais kukumbatia utoaji huduma kidijitali

CHARLES WASONGA: Mawaziri watekeleze agizo la Rais kukumbatia utoaji huduma kidijitali

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto anastahili pongezi kwa kuagiza mawaziri na makatibu wa idara zote za wizara 22 kukumbatia mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya kidijitali.

Aliwaagiza kushirikiana na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi Kidijitali ili kufanikisha mpango huo.

Dkt Ruto alisema hayo kwenye mkutano wa mawaziri na maafisa wengine wakuu wa serikali ulioandaliwa mkahawa wa Fairmont Mount Kenya Safari Club mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Kulingana na Rais, mfumo huo utawezesha Wakenya kupata zaidi ya huduma 5,000 za serikali haraka na rahisi pasina bughudha za urasimu uliokolea katika afisi za serikali.

Nakubaliana na Dkt Ruto kwamba mfumo huo wa utoaji huduma kidijitali ni njia moja ya kupambana na kero la ufisadi, ambalo limekita mizizi miongoni mwa baadhi ya maafisa wa serikali.

Hamna haja kwa mlipaushuru kulazimishwa kutoa hongo ili apate stakabadhi muhimu kama vile pasipoti.

Sasa ni wajibu wa mawaziri kutii agizo la Rais na kushirikiana na Wizara ya ICT yake Bw Eliud Owalo ili waondolee Wakenya usumbufu wanaposaka huduma za serikali.

Aidha, mfumo huo wa kidijitali utachangia kuokolewa kwa fedha nyingi ambazo serikali hutumia kununua vifaa vya ofisini, kama vile mabunda ya karatasi, kalamu na mashine za kutoa chapa.

Kwa mfano, Wakenya wenye simu za kisasa zenye intaneti watahitaji tu kununua data ili kutuma maombi ya leseni za uendeshaji magari, pasipoti, cheti cha mienendo bora, cheti cha ulipaji ushuru na kadhalika.

Hii itapunguza gharama ya kufika ofisi za serikali kila mara kupata huduma hizo.

Ikiwa huduma kidijitali utakumbatiwa kote serikalini katika miezi sita ijayo kama alivyoagiza Rais Ruto, hilo litaimarisha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Wawekezaji watakuwa na motisha kuanzisha biashara mpya na hivyo kutoa nafasi za ajira kwa Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Gachagua si Naibu Rais wa eneo la Mlima Kenya...

Niongeleshe chemba, Sakaja aambia Rigathi

T L