• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:55 PM
CECIL ODONGO: Gachagua si Naibu Rais wa eneo la Mlima Kenya pekee

CECIL ODONGO: Gachagua si Naibu Rais wa eneo la Mlima Kenya pekee

NA CECIL ODONGO

KAMA ilivyo wadhifa wa Urais, ule wa Naibu Rais unastahili kuashiria umoja wa taifa na mshikilizi wake hafai kuonekana kuegemea upande fulani wa nchi.

Tangu Kenya ijinyakulie uhuru, imekuwa na Makamu wa Rais 10 kabla ya William Ruto (sasa Rais) na Rigathi Gachagua kushikilia wadhifa huo, ambao sasa unafahamika kama Naibu Rais katika Katiba mpya ya 2010.

Walioshikilia nyadhifa hizo miaka ya nyuma walijizatiti kudhihirisha kuwa wao ni viongozi wa kitaifa, na walikuwa na utendakazi ulioenzi uadilifu si ubaguzi.

Ilikuwa vigumu sana kuona chembe yoyote ya mapendeleo kwa jamii zao nyakati za Moody Awori na wendazao Michael Kijana Wamalwa, Profesa George Saitoti na Mwai Kibaki.

Hata hivyo, katika utawala huu wa Kenya Kwanza Naibu Rais anaonekana kumakinikia zaidi kuwa kiongozi wa Mlima Kenya badala ya kuwa kiunganishi cha Wakenya wote, kama walivyodhihirisha watangulizi wake.

Bw Gachagua amekuwa akijisawiri kama kiongozi wa eneo la Mlima Kenya kila mara anapopanda jukwaani kuzungumza, hata katika hafla za kitaifa ambazo zinafuatiliwa na Wakenya.

Wikendi iliyopita kwenye ibada ya makanisa mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, Bw Gachagua alipopanda jukwaani alilonga Kikuyu kwa karibu nusu ya hotuba yake katika hafla iliyohudhuriwa na maafisa wengi wa ngazi za juu serikalini.

Hii ni licha ya kuwa maombi hayo yalikujia baada ya kongamano la siku tatu la kutathmini utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza na kutoa mapendekezo jinsi ya kuboresha huduma kwa Wakenya.

Katika hotuba zake nyingi anazotoa kwa lugha ya Kikuyu, Naibu Rais anaonekana kama aliyejawa na roho ya kulipiza kisasi dhidi ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye anasema uongozi wake ulimnyanyasa kwa sababu yake kuunga azma ya Rais Ruto.

Umoja au uwiano wa kitaifa upo wapi kama kazi ya kiongozi anayeshikilia mamlaka baada ya Rais, kuzoea kuhutubu kwa lugha ya kijamii kwenye hafla za kitaifa.

Aidha, inaonekana Bw Gachagua amelenga kutumia mbinu zote kutaka kuwa kigogo wa siasa za Mlima Kenya; kutokana jinsi anavyopendelea jamii hiyo hususan katika masuala ya kibiashara jijini Nairobi.

Ni mwezi Desemba tu ambapo Naibu Rais alimkaripia Gavana Johnson Sakaja baada ya wahudumu wa matatu kutoka Mlima Kenya kulalamikia mpango wa kuzuia magari yao yasiingie katikati mwa jiji kuu ili kuepuka msongamano.

Kinachojitokeza wazi ni kwamba kiongozi huyo ameonyesha maslahi ya jamii yake ndiyo muhimu wala si ya Wakenya wengine.

  • Tags

You can share this post!

Kagame akataa zigo la wakimbizi wa DRC

CHARLES WASONGA: Mawaziri watekeleze agizo la Rais...

T L