• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
CHARLES WASONGA: Ni picha mbaya Sonko kushambuliwa katika mkutano wa Azimio Mombasa

CHARLES WASONGA: Ni picha mbaya Sonko kushambuliwa katika mkutano wa Azimio Mombasa

NA CHARLES WASONGA

TUKIO la hivi majuzi ambapo aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko alifurushwa kutoka kwa mkutano wa kisiasa ulioongozwa na mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga mjini Mombasa linaonyesha kuwa hali sio shwari ndani ya muungano huo.

Mkutano huo ulisitishwa kwa muda baada ya vijana kumpapura Bw Sonko ambaye aliwasili katika uwanja huo wa Mkomani, eneo bunge la Nyali, baada ya Bw Odinga na viongozi wengine kuketi.

Baadhi ya vijana walimzuia mwanasiasa huyo machachari kupanda katika jukwaa ambako walikuwa wameketi viongozi wakuu kabla ya gari lake kushambuliwa kwa mawe na akatokomea.

Iliwalazimu maafisa wa usalama kufyatua risasi kadha angani ili kutawanya vijana hao walioaminika kuwa wafuasi wa wanasiasa ambao wanakerwa na uamuzi wa Bw Sonko kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa.

Sonko anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Wiper ambacho ni mojawapo wa vyama tanzu katika muungano wa Azimio.

Azma yake hata hivyo haijapokelewa vyema na viongozi wa ODM katika kaunti ya Mombasa wakiongozwa na Gavana Ali Hassan Joho anayemuunga mkono mwaniaji wa ODM Abdulswamad Sheriff Nassir.

Kimsingi, vurugu zilizoshuhudiwa katika mkutano huo hazikufaa kutokea kwa sababu vyama vya Wiper na ODM ni miongoni mwa vyama 26 vinavyomuunga mkono azma ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu.

Sonko alikuwa na kila haki ya kuhudhuria mkutano huo kwa msingi kwamba mgeni rasmi alikuwa ni mgombea urais wa Azimio, japo alifika kuchelewa wakati ambapo viongozi walikuwa wameanza kutoa hotuba zao.

Haikuwa jambo nzuri kwa Bw Sonko kuchukuliwa kama adui au mgeni ilhali Katiba ya inawapa Wakenya uhuru wa kuzuru maeneo mbalimbali nchini na kutangamana; kwa amani bila vurugu.

Viongozi ambao wanaendeleza dhana kwamba Bw Sonko ni “mgeni” na hivyo hafai kuwania ugavana kaunti ya Mombasa wanafaa kuelewa kuwa kipengele cha 38 cha Katiba kinatoa uhuru kwa Mkenya yeyote kuwania kiti cha kisiasa popote nchini.

Hii ndio maana chama cha Wiper kilimdhamini Bw Sonko kama mwaniaji wake wa kiti cha Ugavana katika kaunti ya Mombasa licha ya kwamba amewahi kuwania nyadhifa mbalimbali katika kaunti ya Nairobi.

Isitoshe, japo Bw Sonko amekuwa akiendesha siasa zake maeneo ya bara haina maana kuwa hapaswi kujaribu bahati yake katika kaunti ya Mombasa, ambako anamiliki biashara nyingi.

Ikiwa Bw Hezron Awiti Bolo ambaye pia ni mfanyabiashara kaunti ya Mombasa, na ni mzawa wa bara, amewahi kuwania na kushinda kiti cha ubunge katika eneo la Nyali, sembuse Bw Sonko.

Mwaka huu, Bw Bolo ni miongoni mwa wanasiasa wanaong’ang’ania kiti cha ugavana wa Mombasa akidhaminiwa na chama cha Vibrant Democratic Party (VDP).

Uongozi wa Azimio unafaa kupalilia moyo wa undugu na utangamano kati ya vyama tanzu katika muungano huo ili uweze kufikia lengo lake la kushinda kiti cha urais.

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la muungano huo anafaa kuhakikisha kuwa vita vya ndani kwa ndani miongoni mwa vyama tanzu vinazimwa.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool kuipa Manchester City taji ikipigwa leo

Jumwa akataa kukatwa miguu UDA

T L