• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Jumwa akataa kukatwa miguu UDA

Jumwa akataa kukatwa miguu UDA

NA VALENTINE OBARA

MZOZO umeibuka katika Kaunti ya Kilifi, kuhusu usimamizi wa kampeni za urais za Naibu Rais William Ruto, saa chache baada ya Gavana Amason Kingi kutangazwa kuwa mmoja wa waratibu wa kampeni hizo Pwani.

Viongozi wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) tawi la Kilifi, wamesisitiza kampeni hizo zinafaa ziendelee kusimamiwa na afisi ya chama hicho ambayo imekuwa ikipokea ufadhili kutoka kwa chama na Muungano wa Kenya Kwanza.

Afisi hiyo imekuwa ikiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, akisaidiana na wanachama wengine wa UDA akiwemo mwenzake wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya.

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto ambaye ndiye kinara wa UDA na Kenya Kwanza, alimjumuisha Bw Kingi katika kikosi cha kupanga mikakati ya kampeni za Muungano wa Kenya Kwanza ukanda wa Pwani.

Bw Kingi anayeongoza Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) alitakiwa kushirikiana pamoja na Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, ambaye ndiye alikuwa amepewa jukumu hilo awali pamoja na Mbunge Mwakilishi wa Taita Taveta, Bi Lydia Haika.

Hata hivyo, wakiongozwa na Bi Jumwa, maafisa wa UDA katika Kaunti ya Kilifi jana walisema ni sharti Bw Kingi ajitolee kushirikiana nao.

“Tunataka kumkumbusha Kingi kwamba heshima inalipwa kwa heshima. Kama vile ulituambia chama chako kiheshimiwe, pia wewe heshimu uongozi wa UDA ndani ya Kilifi Kaunti,” akasema Bi Jumwa.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari, alisema pia hawatakubali kuachia PAA kiti chochote katika kaunti hiyo.

Dkt Ruto alikuwa amethibitisha mipango ya Kenya Kwanza kutafuta upatanishi wa wagombeaji ili muungano usiwe na ushindani wa vyama tanzu, ambapo kikundi kile kile cha viongozi aliowataja ndicho kinatarajiwa kuongoza mashauriano hayo Pwani.

Bw Baya ambaye aliandamana naye katika kikao hicho, alimtaka Bw Kingi kuelekeza kampeni za kumpigia debe Dkt Ruto katika kaunti nyingine za Pwani, akidai kuwa tayari kampeni hizo zilishapiga hatua kubwa Kilifi na kile kilichobaki kumwongezea naibu rais ufuasi kinaweza kufanikishwa hata bila Bw Kingi kuwepo.

“Kama anataka kuwa spika alivyoahidiwa, atakuwa spika wa serikali ya UDA, atachaguliwa na wabunge wa UDA kwa hivyo lazima aanze kuheshimu UDA. Usimamizi wa kampeni za Ruto utafanyika katika afisi hii ya Kituo cha Hasla wala si kwingine,” akasema Bw Baya.

Kulingana na wawili hao, mkataba ambao viongozi wa UDA eneo la Pwani waliweka na Dkt Ruto ulikuwa tayari umegusia masuala yote ambayo Bw Kingi aliwasilisha kupitia kwa chama chake cha PAA.

Mwaka 2021, Dkt Ruto alikutana na wafuasi wake kutoka Pwani ambapo walimkabidhi ripoti kuhusu masuala ambayo walitaka aahidi kuyatatua endapo atashinda urais, kama alitaka waunge mkono azimio lake.

Bi Jumwa alisema walishangaa wakati Bw Kingi alipowasilisha masuala yale yale kama sharti la kumuunga mkono Dkt Ruto kwa urais katika uchaguzi ujao.

Masuala hayo ni kama vile utatuaji wa migogoro kuhusu umiliki wa ardhi, kurekebisha usimamizi wa bandari ya Mombasa ili kuongeza mapato Pwani na nchini kwa jumla, kuboresha mandhari ya kibiashara Pwani ili kuongeza nafasi za ajira, uwakilishi sawa wa jamii za Pwani katika nyadhifa za kiserikali, miongoni mwa mengine.

Zaidi ya hayo, Bi Jumwa alishikilia msimamo wake wa kukashifu utawala wa Bw Kingi akisema itabidi ‘ajitakase’ mbele za wananchi anapomtafutia kura Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Ni picha mbaya Sonko kushambuliwa katika...

Tunisia waandamana kuhusu bei za vyakula

T L