• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Amerika, China zisisukume mataifa mengine kwenye vita vya kishenzi

DOUGLAS MUTUA: Amerika, China zisisukume mataifa mengine kwenye vita vya kishenzi

NA DOUGLAS MUTUA

MBONA ninahisi Uchina imetazama juhudi za mataifa ya magharibi katika kuisaidia Ukraine – ambayo inapigwa vita na Urusi – na kutabasamu?

Vita vya Ukraine vimetoa fursa kwa Uchina kukadiria uwezo wake wa kuyakabili mataifa kadha ikiwa yataijia ikizua vita popote duniani.

Tabia zake zimeiweka mkabala na Ameriika na washirika wake wa kijeshi na kiuchumi, hali ambayo inaweza kuleta vita vya tatu vya dunia isiposhughulikiwa kwa makini.

Uchina imezidi kwa uchokozi na kiburi kwa kuzikabili ndege za mataifa mengine angani huku ikidai kuingiliwa mipaka yake na nchi hizo.Imeizuia ndege ya kijasusi ya Australia iliyokuwa ikishika doria baharini, kisha ikaitishia nchi hiyo kwamba ‘isipojibeba kistaarabu’ itakabiliwa na ‘matokeo mabaya sana’.

Vilevile, Uchina imetishia ndege za kivita za Canada kwa kuziandama kwa namna hatarishi zilipopaa karibu na Korea Kaskazini zikitekeleza vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Hata kabla ya vita vya Ukraine kuzuka, Uchina ilikuwa ikirundika silaha kwa minajili ya kukivamia Kisiwa cha Taiwan ifikapo 2025.

Kisiwa hicho kilichojitenga na Uchina kinajitawala, lakini hakitambuliwi rasmi kama taifa huru, hivyo Uchina inanuia kukirejesha kwenye kwapa lake kikamilifu.

Nchi ambazo ndizo watenzi wakuu katika masuala ya kimataifa zinajua ni lazima uvamizi huo ufanyike, isiyojulikana kwa hakika ni tarehe.

Ni jambo linalozikosesha usingizi nchi hizo kwani dunia itakabiliwa na changamoto mbaya mno iwapo kutakuwa na vita kwenye mabara ya Uropa na Asia wakati mmoja.

Ni kwa sababu hiyo ambapo hivi majuzi, Rais Joe Biden wa Amerika, alijikwaa ulimi alipozuru bara la Asia: alikariri kuwa Amerika itaitetea Taiwan ikiwa Uchina itaivamia!

Tamko hilo linashtua mno likitolewa na rais wa Amerika, ndiposa Ikulu ya White House ilikimbia kusema sera ya Amerika ya kutambua mamlaka ya Uchina kwa Taiwan haijabadilika.

Kushtua kwa kuwa Amerika na Uchina zikiingia vitani, dunia itajigawa mafungu matatu: moja liiunge Amerika, jingine Uchina na la tatu lisifungamane na upande wowote.

Bila shaka watundu kama Urusi, Korea Kaskazini na mataifa mengine yenye kichaa yatajiunga na Uchina, nayo ya Muungano wa Kijeshi wa NATO na mengineyo yaungane na Amerika.

Labda makundi hayo mawili yatakuja Afrika kusajili makurutu wa kwenda kuyapigania kama ilivyotokea wakati wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.

[email protected] 

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi ahofia kubaki kwa mataa kisiasa baada ya Agosti 9

GUMZO: Arsenal inamtaka beki wa Dortmund

T L