• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:55 AM
Mudavadi ahofia kubaki kwa mataa kisiasa baada ya Agosti 9

Mudavadi ahofia kubaki kwa mataa kisiasa baada ya Agosti 9

NA SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, ameingiwa na hofu ya kujipata kwenye baridi ya kisiasa baada ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kudhamini wagombea katika ngome yake Vihiga.

Hii ndio maana kiongozi huyo amewataka wapiga kura wa hapo kutochagua wagombea viti mbalimbali wa tikiti ya chama cha UDA, kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Bw Mudavadi amemshutumu Dkt Ruto hususan kwa kuwadhamini wagombea ubunge katika eneobunge la Sabatia.

UDA imemdhamini Clement Siloya kuwania kiti hicho cha ubunge ambacho Bw Mudavadi amewahi kushikilikia kwa miaka 15.

Kinara huyo wa ANC alisema mnamo Alhamisi kwamba hatua hiyo ya UDA inahujumu chama chake, ambacho ni miongoni mwa vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA).

“Viti vyote eneo hili ni muhimu zaidi kwangu na kiongozi mwenzangu wa Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula,” alitanguliza kinara huyo Alhamisi katika mkutano wa siasa.

“Kwa hivyo, chama cha UDA na vyama vingine ndani ya Kenya Kwanza havifai kudhamini wagombeaji katika maeneo haya,” Bw Mudavadi akaongeza katika mkutano huo eneobunge la Vihiga.

Kaunti ya Vihiga na eneo pana la Magharibi mwa Kenya linachukuliwa kuwa ngome ya vyama vya ANC na Ford Kenya.

Kwa mujibu wa mkataba uliobuni muungano wa KKA, vyama hivyo viwili vina kibarua cha kuvutia asilimia 70 ya kura za urais kwenye kapu la Dkt Ruto; iwapo vinataka kutengewa asilimia 30 ya nyadhifa katika asasi zote za serikali ya KKA.

Malalamishi ya Bw Mudavadi yalionekana kushinikiza yale ya awali ya Seneta Cleophas Malala wa Kakamega.

Bw Malala aliitaka UDA kutomwasilisha Bw Siloya kama mgombea wa kiti cha ubunge cha Sabatia, akisema hatua hiyo itaathiri masilahi ya chama cha ANC.

Bw Malala alidai kuwa eneobunge la Sabati linafaa kuachiwa ANC ili kuboresha nafasi ya Bw Mudavadi katika serikali ijayo endapo Dkt Ruto atafanikiwa kushinda urais.

Bw Siloya anapania kurithi mbunge wa sasa Bw Alfred Agoi, ambaye alichukua nafasi ya Bw Mudavadi kama mbunge mnamo 2002.

Kinara Mudavadi alisema kwamba kwa kuwa muungano wa Kenya Kwanza umeachia chama cha UDA nafasi mbili kubwa za urais na unaibu rais, Dkt Ruto hafai kuingilia ngome za ANC na Ford Kenya katika eneo la Magharibi mwa Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Mkuu wa shule ya msingi kizimbani kwa kupora Sh2 milioni

DOUGLAS MUTUA: Amerika, China zisisukume mataifa mengine...

T L